Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami kwanza nimshukuru Mheshimiwa hapa Ole-Sendeka amenisaidia kushukuru kwa niaba, kwa hiyo mimi nitaenda moja kwa moja kwenye point. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana ya Waziri nikushukuru, kule Mpanda tumepokea zaidi ya shilingi bilioni tatu kuboresha kilometa 38 lakini kuna mtandao wa kilometa 105 ambazo tunategemea kupata shilingi bilioni 4.7, lakini nishukuru sana Mheshimiwa Waziri tumepatiwa kwa maana Miji 28 tumepatiwa kilometa 42. Niseme ukilinganisha miji mingine yote naona Mji wa Mpanda jinsi ambavyo Mheshimiwa Waziri umeufikiria katika eneo hilo ili tuweze kuongeza mtandao wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu tuna miradi ya Kakese na Milala ambapo kuna fedha kutoka National Water Fund. Naomba fedha hizo zipelekwe kwa haraka Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo ya shukrani na mimi niendelee kusema nafahamu siku zote Waziri amekuwa akituambia hakuna mbadala wa maji, nakubaliana na wewe katika hilo na ukiongelea maji kwa maana maji ni usalama wa nchi ni usalama wa Taifa. Watafiti mbalimbali wanakwambia yawezekana vita vya tatu vya dunia vikatokana na tatizo hasa la maji katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa hiyo, hayo yote yanaonyesha umuhimu wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu najua tunaambiwa mpaka itakapofika mwaka 2025, kutakuwa na upungufu wa maji kwa maana ya 8,083 lakini mimi nataka kusema nini? Siku zote nikichangia hapa nimekuwa nikitoa mifano mpaka ya China, mito mbalimbali, vyanzo mbalimbali ambavyo vimekuwa ikiunganisha Kusini kuja Kaskazini, Mashariki kwenda Magharibi kwa maana ya Tanzania hii. Niombe sana sana sana, najua wakati nikiingia hapa uliniambia Kapufi mimi najua utakapoingia pale wazo lako ni moja tu kuhusu Gridi ya Taifa. Umeniambia pale, kwa hiyo maana yake suala hili wewe na Wizara yako mnalo akilini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie kwa maana ya nchi yetu hii njema, nafahamu umuhimu wa visima, nafahamu tumepeleka magari lakini twenda kushoto twende kulia, Waziri wa Kilimo juzi ameongelea namna ya kuigawa nchi hii kwenye kanda za kilimo. Nakuomba na wewe Mheshimiwa Waziri wa Maji igawe nchi hii kwenye kanda za maji. Kwa mfano, ukitumia tu Ziwa Victoria nilikuwa nikipiga mahesabu hapa kwa maana ya Mikoa yetu 26, Ziwa Victoria peke yake zaidi ya Mikoa 10 inakuwa covered. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Ziwa Victoria tu lime- cover zaidi ya Mikoa 10, Ziwa Tanganyika? Hebu chukulia Mikoa mingine mitano, Ziwa Nyasa Mikoa mingine mingapi? Ziwa Rukwa Mikoa mingine mingapi? Kwa hiyo, tukiigawa nchi hii katika Kanda hatuna sababu ya kuyatafuta maji kwa tochi. Kisima ambacho hauna uhakika nacho wakati maji yale pale unayaona kwa wingi wake. Iwe ni Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria, Ziwa Rukwa na ninajua Rais wa nchi hii ameongelea habari ya kutumia vyanzo hivyo. Kupanga ni kuchagua, naomba tuje na vipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu zilizopita tuliwahi kuambiwa tuna omba tuiunganishe nchi hii kwa barabara za lami na hili naliona likienda kuwa limetimia. Leo unaweza ukatoka Mtwara ukafika Bukoba kwa taxi au bajaji! Andika historia, Mheshimiwa Waziri aandike historia. Mimi niendelee kusema sibezi shughuli nyingine zote zinazofanyika, ununuzi wa magari, uchimbaji wa visima. Tugawe nchi hii, ukiigawa nchi hii nakuhakikishia kwa maji tu hayo tuliyonayo visima iwe ni ziada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hayo mabwawa tunayokusudia kukinga maji ni ziada. Maji tuliyonayo Victoria tu sisemi kwamba yamalize nchi nzima lakini hebu angalia kama Victoria imefanya miji 10, Tanganyika ikafanya mingine 10. Katika mikoa 26 tumebakiza mingapi? Najua Zanzibar watakuja na utaratibu mwingine kama ni visima tuseme sawa lakini bado ungeweza kuyavusha maji hata huko. Kwa hiyo mimi niendelee kusema naomba naomba, mimi sitaki kwenda mbali zaidi, katika hili hatuna sababu ya kulalamika, kupanga ni kuchagua na lazima tuje na vipaumbele. Tukisema tunakusudia kwenda kuiunganisha nchi kwa maji, kuwa na mtandao wa maji hilo linawezekana, hivi vyanzo vingine iwe ni ziada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshukuru kama ambavyo tumesema hapo mwanzo ukizungumzia maji hata wenzako wengine wote awe ni mtu wa kilimo na wengineo, kwanza tuanze na maji. Ukizungumzia kilimo kwa maana ya umwagiliaji, so long as maji tumeyafanyia kazi, wewe ukienda ukaya-tap hata hayo maji mengine yanayotiririka ya mvua na mambo mengine ambayo yanapotelea baharini na kwingineko, sisi tuamue sasa kwamba haya maji mengine ndiyo yaende kwenye kilimo, haya ambayo ni mengine yaende kuwenye huduma za jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kwenda mbali zaidi ambako kuna nchi za wenzetu ukifungua tu maji ya bomba una uwezo wa kuyanywa. Sitaki kwenda huko kwa sababu kwanza tu ile mgawanyo wa maji hatujafika hapo lakini nilitamani pamoja na huduma hizi za maji tuendelee kuangalia ubora wa maji yenyewe. Nchi za watu huhitaji hata kwenda kununua maji dukani, unafungua tap yako unachota maji unakunywa. Kwa hiyo, mimi naamini tukianza kwanza na ufumbuzi huo wa kupatikana kwa maji hayo mengine yatafuatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana na wengine wote kuhusu suala zima la majitaka. Nilisema hapa majitaka wala siyo maji ya kubeza. Unaweza ukapitia majitaka yakakusaidia kufanya majukumu mengine. Miji mingi duniani inapendezeshwa kwa kupitia majitaka. Kwa hiyo, kwa kuzalisha majitaka ukaya-purify, maji hayo yanarudi kufanya shughuli hizi nyinginezo kupendezesha Miji kama hivyo, badala watu kupita na kusema kwamba mji ni mchafu, wapite wakiuona mji umependeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa misingi hiyo niombe kwa maana ya huduma ya majitaka kutolewa kwa mfumo wa magari na kama siyo magari tu hata kwa maana ya hayo mabwawa mengine ambayo ni ya kutibu maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la udhibiti wa uchimbaji holela wa visima ndiyo maana nakusudia ni bora tukaendelea kuangalia vyanzo hivyo tulivyonavyo tayari kwa sababu study zinasemaje? Hili nilikuwa naomba sana kwa maana ya muda mrefu haswa katika ile miji ya wenzetu tafiti zako zijielekeze pia. Unaweza ukafurahia kwa maana ya kuyachimba maji yaliyopo ardhini lakini ukazalisha tatizo jingine.
Kwa hiyo, naomba sana hilo likifanyika liende sambamba na tafiti. Sehemu nyinginezo duniani miji imekuwa ikizama kutokana na suala hilo hilo la uchimbaji visima bila kufanya tafiti. Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri katika eneo hilo tuendelee kuyazingatia hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini siyo kwa umuhimu kwa maana ya Chuo cha Maji kuzalisha wataalam. Haya yote tunayoyatamani naendelea kuomba tusiache kuboresha watu wetu katika fani hii ya maji ili waendelee kutoa huduma iliyotukuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru kwa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)