Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyopo mezani. Kwanza kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa sababu naamini Watanzania wengi wanajua hili neno la kumtua Mama ndoo kichwani, yeye ndiye Muasisi aliyeasisi alipokuwa Makamu wa Rais. Sasa hivi yeye anaitekeleza akiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na anatekeleza kwa kasi. Kwa hiyo, nadhani wote tuna kila sababu ya kumpongeza kwa sababu hata tumeona kwenye bajeti hii imeongezeka kwa asilimia saba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Aweso kwa kazi nzuri anayoifanya, Mheshimiwa Naibu wake Engineer Maryprisca Mahundi, Katibu Mkuu Engineer Nadhifa na Naibu wake Watendaji wote lakini bila kusahau Mameneja wa RUWASA hasa Meneja wa RUWASA wa Mkoa wa Mtwara Engineer Primy Damas na mameneja wetu wa wilaya kwa kuwa nafanya kazi Mkoa wote wa Mtwara. Kwa nini nampongeza Mheshimiwa Waziri? Kwa sababu ni kweli kabisa kwamba amekua akijua mihemo ya wagonjwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana wakati nachangia hapa nadhani moja ya Wabunge waliyolia hapa kuhusiana na maji ya kuokota nilikuwa ni mmoja wapo na hasa nilipowapa ile hisroria ya kwamba watu walikuwa wanatumia maji ya tikitiki wakati fulani kwa sababu ya shida ya maji katika Mkoa wa Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu nimshukuru Mheshimiwa Aweso, kwa sababu waswahili wanasema kushukuru ni kuomba tena. Namshukuru sana Waziri kwa sababu kuna miradi kadhaa ambayo imetekelezwa kwenye Mkoa wetu wa Mtwara. Hivyo nitakwenda kuishukuru hiyo nianze kwanza kwa kuunga mkono mapendekezo yote, ama maoni ya kamati kwa kuwa ni mjumbe wa kamati na yeye amekuwa ni msikivu na timu yake yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye yale maoni kumi naomba nisisitize kwenye mambo mawili; la kwanza, ni Wizara haina namna nimuhimu sana ikatengeneza mpango kabambe wa maji hii tunayosema kwa kilugha chetu cha kimakua National Water Master Plan, hili lazima lipatikane lakini pia Wizara lazima iwe na gridi ya maji na hili linawezekanaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge hapa wamesema; Mheshimiwa Waziri, unganisha vyanzo vikubwa vya maji kwa maana ya Maziwa, Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na mito mikubwa kama Mto Ruvuma na Mto Rufiji na hapo sasa utaona namna ambavyo mambo ama azma ile ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mama ndoo kichwani itawezekana. Kwa sababu utakuwa tumeweza kuya–tap hayo maeneo muhimu na unakuwa na gridi ikinyofoka huku unawasha huku, hilo ndiyo jambo ambalo litakutoa na nadhani utaweka historia katika maisha yako ya kuwahudumia watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili kwenye yale mapendekezo kumi ya kamati, nisisitize kwenye kutumia watalamu wa ndani. Tulipokuwa kwenye kamati tumetembelea miradi, tumeona ule wa Babati pale namna ulivyokuwa mzuri na umetekelezwa na watalam wa ndani sina shaka watalamu wa ndani wa wizara yako wanaweza wape nafasi wakatekeleze miradi mingine kule ambako Waheshimiwa Wabunge wanakuomba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niendelee kukushukuru Mheshimiwa Waziri nakushukuru kwa kipindi kirefu sisi mradi wetu wa Makonde tangu enzi hizo ulivyojengwa ulikuwa unaingia kwenye vitabu lakini ulikuwa hautekelezeki. Kwa mara ya kwanza safari hii wewe na Naibu wako na Katibu Mkuu pale mmeweka alama, kwa nini? Kwa sababu mradi ule wa bilioni 84.7 tayari fedha bilioni 12 ikiwa ni malipo ya awali zimeishakwenda na mkandarasi yuko site kazi ya kusafisha maeneo ya kujenga matenki kwenye majimbo manne inaendelea. Newala Mji, Newala Vijijini, Tandahimba na Nanyamba hapa ninaomba tu kama nilivyotangulia kukushukuru na ninakuomba tena kwamba phase one ya mradi huu ni muhimu ikaunganisha maji katika maeneo yote muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye ule mchoro wa maji utakuta kwa mfano pale Nanyamba inapitia kata kumi lakini kata tatu ndiyo zinaonekana zitakwenda hali kadhalika Tandahimba. Kwa hiyo, ni muhimu phase one hii ikaenda maeneo yote ya mradi ili RUWASA waje kuwa na kazi ndogo. Kwa sababu unajua fedha zao pia haziwatoshi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ya pili kwa sababu umeweka alama na unakusudia kutuwekea alama ili mimi mwakani nisije tena kusema habari ya kuokota maji hapa ni vizuri mradi ukatekelezwa kwa kasi na fedha ikaenda ili tuone matokea ya kazi yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ninalo kushukuru Mheshimiwa Waziri sisi tuna Mamlaka pale MANAWASA Masasi kwa fedha za 2021/2022 tayari umepeleka milioni 434 kati ya 738 nikuombe kwa zile fedha za 2022/2023 milioni 940 peleka kaka wakaweze kusambaza maji mjini Masasi na Nachwingea lakini na vijijini ambako ndiyo tunatoka sisi kule vijiji ambavyo vinazunguka kwenye ule mradi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu; ambalo namshukuru Mheshimiwa Waziri kweli umejua shida za watu wa Mtwara. Kwa sababu jambo ambalo lilikuwa linaniliza mwaka jana la kutekeleza mradi wa Mto Ruvuma angalau umeonyesha kwa hatua za awali kwenye bajeti hii ipo miradi inayotekelezwa.
Pia ukuachia hapo kuna mpango wa kuchimba mabwawa, sasa ninakushukuru kwamba kwenye usanifu kwenye miradi ya kuchimba mabwawa yatakayohifadhi maji ya mvua yale 27 kwenye ukurasa wako wa 77 umeonyesha kuna usanifu katika Lukuledi – Masasi, Namasobo – Nanyumbu, Chilunda – Nanyumbu, Mikangaula – Nanyumbu. (Makofi)
Mheshimiwa Mweyekiti, kwa sasa mradi unaoendelea Sengenya – Nanyumbu tunakushukuru sana lakini yatakayojengwa kwa force account Namasobo – Nanyumbu. Nakushukuru kipekee unajua Lukuledi imezungukwa na kata nyingi ambazo hazina maji. Ule Mradi wa Manawasa hautatosheleza kwenye zile kata ambazo inazunguka lakini utafanya usanifu na utajenga umenihakikishia hivyo niseme nini ninakushukuru Mheshimiwa Waziri kwamba kwa bilioni 1.7 na ushehe uko ukienda kutekeleza ile hata Mwenyezi Mungu ataendelea kukubariki kwa sababu umewatibu waliyo wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru pia kwamba kwenye ule utaratibu wakuchimba visima. Visima vilivyochimbwa na bonde kwa mwaka huu uliopita 2022 lakini vile visima vyako vitatu kwenye kila jimbo, kwenye majimbo kumi ya Mkoa wa Mtwara tayari umechimba na bado nane una uhakika utakwenda kumaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa niombe, sasa vile visima ambavyo vimechimbwa tayari ni muhimu sasa wananchi wakayanywa yale maji hasa kwenye maeneo yote nawaombea lakini nimeona kwenye vijiji kadhaa kule Sululu ya leo, Masiku, Chingulungulu umechimba lakini maji hawajaanza kuyanywa maana yake ni kwamba wataenda kule kuyaokota maji sasa na maji haya wanaenda kuyaokota mbali mtoni. Ninajua unajua adha za mama zako na sasa una Naibu mwanamke, nimruhusu kwanza kipindi hiki mwezi ujao ule twende akaone adha ambayo inapatikana katika Mkoa wa Mtwara ili tuweze kwenda sambamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niseme kuna suluhisho la kudumu la upatikanaji wa maji katika Mkoa wetu wa Mtwara na lenyewe si jipya ni suala la kutumia maji ya Mto Ruvuma. Kuna mambo mengi watalamu wanasema maji yanapungua, sijui yanafanyaje? Lakini kama utatengeneza master plan ile inamaana unaweza kuunganisha Ziwa Nyasa na Mto Ruvuma kwa hiyo, wananchi wa Mkoa wa Mtwara, wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, wananchi wa Mkoa wa Lindi hii changamoto ya upungufu ama kukosa maji safi na salama tutakuwa tumeondokana nayo. Ukifanya hivyo kwakweli utakuwa si tu kwamba umesikiliza mihemo ya wagonjwa sisi lakini utakuwa umetutibu hata kama ujasomea udaktari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ninawatakia kila kheri, chapeni kazi nyingi wote ni vijana na kazi endelee. (Makofi)