Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Maji. Kwanza kabisa niweze kuipongeza Wizara kwa kazi nzuri inazofanya. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo anahakikisha Wizara hii ya Maji anaipatia nguvu na kuiangalia kwa jicho la pili zaidi. Vilevile Waziri wetu Jumaa Aweso, Mheshimiwa Waziri hongera sana kwa kazi pamoja na dada yangu Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri unazozifanya. Mmekuwa ni viongozi mahiri na wenye usikivu zaidi.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na sifa hizo nzuri lakini vile vile watendaji wa RUWASA napenda kuwapongeza watendaji wa RUWASA walioko mkoa wa Tabora hususan injinia wetu Eng. Kapufi, hongera sana kwake kazi zinafanyika na zioneonekana.
Mheshimiwa Spika, pamoja na sifa hizo bado Mkoa wetu wa Tabora una changamoto ya maji. Mnamo mwaka 2021 Februari, Hayati John Pombe Joseph Magufuli alikuja mkoani kwetu kuzindua mardi wa maji ya Ziwa Victoria, na akasema Mei 21, maji yatakwenda katika Wilaya tatu ambazo hazijaenda.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wetu una Wilaya saba. Kati ya Wilaya saba nne zimefikiwa na maji ya mradi wa Ziwa Victoria ni pongezi sana kwenu hiyo ni hatua nzuri, lakini Wilaya hizi ambazo ni tatu hazijafikiwa na mradi huu wa maji zilionekana Mei 21 maji yataweza Kwenda katika Wilaya hiyo; lakini mpaka hivi sasa maji hayajaenda. Na wakasema, kuna bilioni 25 ambazo zimebaki kwenye mradi wa maji ya Ziwa Victoria kutoka Nzega na Igunga ndizo zitakazopeleka maji katika miji hii mitatu ya Urambo, Kaliua na Sikonge.
Mheshimiwa Spika, mradi huo ni miaka miwili sasa hakuna chochote kinachoendela. Wananchi wanasikiliza hotuba zinazosomwa, na ndicho wanachokiweka kichwani. Hawajui kama maofisini watu wamekaa na Mkandarasi michakato inaendelea wao hicho kitu hawajui. Wanachokitaka ni kumuona mkandarasi yuko site anafanya kazi wako watu na makoleo na nondo sio hizi mambo za maofisini wao hawajui.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri unapokuja kuhitimisha hotuba yako hapo tunaomba utueleze wananchi wa Urambo, Sikonge na Kaliua ni lini? ni tarehe ngapi? ni mwezi gani? na mwaka gani? mkandarasi huyo ambaye ameshapatikana anasubiriwa yeye aingie site ataanza kufanya kazi ili wananchi hawa wa miji hii mitatu waweze kunehemeka na maji? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kwa muda mrefu sana tangu mimi nazaliwa wilaya ya Urambo tunahangaika na maji, tunaita maji ya mlindiko, tunalindika maji mpaka sasa hivi ninvyorudi nyumbani bado naendelea na heka heka ya maji ya mlindiko. Hatujui kufungua koki, wananchi wa Urambo, Kaliua na Sikonge. Tunaomba Mheshimiwa Waziri ukija hapa utueleze. Usipotueleza leo hiyo siku unayohitimisha mimi nitashikilia shilingi yako. Kwa sababu wananchi wanahitaji kujua hatma yao ya shida ya maji ili tuweze Kwenda na sera ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mwanamke ndoo kichwani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile sambamba na haya maji ya mradi wa ziwa Victoria, kaka yangu Jumaa Aweso. Maji haya ya mradi wa Ziwa Victoria hayawezi kuhakikisha kufika katika Mkoa mzima wa Tabora. Mkoa wenye kata 206, tukisubiri hayo maji ya Ziwa Victoria ndiyo yafike kote huko tutafika mpaka miaka 200 ya uhuru watu bdo hawajafikiwa na mradi wa ziwa Victoria. 2021 nilisimama hapa kuchangia katika bajeti yako, nikaomba kwamba maji tuwe na mabwawa ya kuvuna maji ya mvua. Nikushukuru mmeshatenga maeneo katika miji hii mitatu ambayo bado inahangaika sana na maji kwa mfano Ichemba wako kwenye hatua za manunuzi tunaomba hizo hatua ziharakishwe.
Mheshimiwa Spika, unaweza kukuta manunuzi tu yanachukua miaka miwili. Haya maji watu watafikiwa lini? Maji yanatuhama Tabora tuna mvua nyingi, sasa tunajikuta tunaingia kwenye adha ya kuharibu miundombinu ya barabara, tunalia na TARURA madaraja yameharibika. Watu wako visiwani, inapofika kiangazi maji watu wanalia hawana maji. Sasa hiki ni nini? Kwa nini tusiharakishe hii michakato ambayo mmefanya.
Mheshimiwa Spika, tunashukuru milioni 75 amabzo mmeweka kwa ajili ya Ichemba, lakini vilevile Kizengi mmeweka milioni 300 kwa ajili ya mabwawa haya ya kuvuna maji. Nikuombe hizi michakato ziendelee kwa haraka hizi ndizo zinazoturudisha nyuma kwenye kufikia asilimia 85 ya upatikanaji wa maji vijijini na asilimia 95 ya upatikanaji wa maji mjini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tukifanya haya kwa uhakika na kwa uharaka Zaidi, haya mambo yataenda pesa zipo, nini kinachochelewesha? Mkandarasi haendi site kwa wakati, mnamvuta vuta kwa ajili ya nini? Kama hafai atolewe aje mtu mwingine.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja, ahsante.