Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara yetu ya Maji.
Mheshimiwa Spika, wakati naanza kuchangia na mimi niwapongeze timu ya Wananchi kwa ushindi mkubwa sana na jambo zuri ambalo wamelifanya, hizi ni baraka zinazotokana na Waziri wetu kuhudhuria mechi hii, pamoja na mfadhili wetu GSM, Mwenyezi Mungu awabariki kutupa raha hiyo kiasi hicho. Hapo nje ya Bunge nimekutana na Naibu Waziri wa Michezo, Mheshimiwa Mwana FA, ananiambia amehamia rasmi timu ya Wananchi na ametangaza kwenye page yake kwamba amehamia timu ya Yanga. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, naanza kwa kuchangia Wizara yetu ya Maji kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kama mnakumbuka tulikuwa tuna suala la miji 28 na Wabunge wote ambao tunahusika na miradi ya maji katika miji 28 tulikuwa kila mara tukimsumbua Mheshimiwa Waziri kuhusu miradi hii na tulipopata nafasi ya kukaa na Mheshimiwa Rais katika kikao, Waheshimiwa Wabunge walipomuuliza Mheshimiwa Rais alisema subirini tutalifanyia kazi jambo hili na baada ya miezi sita tumeona matokeo yametoea. Nami katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara mradi wangu wa maji wa Kiburubutu Mkandarasi amefika kwa bajeti ya shilingi bilioni 42 na sasa hivi wanapima udongo pale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, nawashukuru sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, wote mmefika Jimboni kwangu mmepanda milimani kule mmeona hali halisi, nawapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watumishi wote wa Wizara hii ya Maji pamoja na Engineer wetu wa RUWASA Wilaya ya Kilombero, Eng. Mlelwa. Kwa kweli mradi ule wa Kiburubutu ni muhimu sana katika Halmashauri ya Mji wa Ifakata ambako utasambaza maji katika Kata Tisa za Tarafa ya Ifakara, ni mradi muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ni aibu sana Mji maarufu kama Ifakara wenye wajanja wengi, unapita barabarani unakutana na mabomba ya mdundiko. Ifakara water base yetu ipo juu ndiyo maana tunapata mafuriko kila mara. Kwa hiyo, mwananchi akichimba tu mita tatu chini anapata maji. Watu wanakunywa maji ambayo hayajapimwa, hayana viwango. Kwa hiyo, huu mradi unasubiriwa kwa kiasi kikubwa sana na kwa hamu kubwa sana ukamilike.
Mheshimiwa Spika, kuna wananchi ambao wanapanda kwenda Kiburubutu kule kuangalia kweli Mkandarasi yupo na kweli jambo hili litatokea? Maana yake ni mradi ambao umetangazwa tangu wakati wa Mwalimu Nyerere. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan wameleta fedha na kwa mara ya kwanza tunaona Mkandarasi. Wizara na Mheshimiwa Waziri tunakuomba, umefika Ifakara umeona presha ile ya watu ilivyo kubwa wakisubiri mradi huo. Tunakuomba sana utusaidie mradi huu uweze kukimbizwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na kweli tuna imani na ile Kampuni ya LNT kwa sababu imekuwa ikiwaita viongozi wa Wilaya na viongozi wa wananchi, mimi mwenyewe Mbunge kila mara wanani-update kinachoendelea, kinachofanyika, kwa hiyo na mimi nikipita kwenye mikutano ya wananchi ninasemea. Jimbo letu la Kilombero, Halmashauri yetu ya Mji wa Ifakara unaweza ukafanya mambo yote, lakini kwa kweli Mradi huu wa Kiburubutu ndiyo namba moja kuliko vitu vyote. Kwa hiyo, ukikaa na watumishi wako wa Wizara huko muangalie muwe mnagusia jambo hili, ni kila kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, tunaomba wakati tunaendelea na mradi huu wa maji wa Kiburubutu, gari la Wizara lilipita kwenda kuchimba visima Jimbo jirani la Mlimba kwa ndugu yangu Mheshimiwa Kunambi na likapita pale Ifakara, tuliomba kwamba kuna visima ambavyo tulichimba tunaomba tupatiwe pesa ili visima hivi vianze kufanyiwa kazi. Vijiji cha Kanyenja, Mikoreko, Iyanga na Mtaa wa Jangwani pale Ifakara.
Mheshimiwa Spika, kwa vile mradi huu wa Kiburubutu utatumia miaka miwili mpaka mitatu, kwa haraka basi tupatiwe fedha katika maeneo haya yenye visima hivi, miradi ya maji ya matenki iwekwe pale kama ulivyotusaidia Sagamaganga na Ungongole wananchi waendelee kutumia maji haya katika miaka hii miwili au mitatu wakati wakisubiri huu mradi wa miji 28.
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, Kata zangu kumi kutokea Zinginari, Kiberege, Kisawasawa, Mwaya, Mang’ula A, Mang’ula B, Sanje, Mkula mpaka Kidatu, wananchi hawa wako kandokando ya Milima ya Udzungwa na Hifadhi ya Udzungwa, Hifadhi ile ya Udzungwa inaporomosha maji kwenda kwenye mashamba ya miwa, huko nyuma wananchi walitengeneza miundombinu yao wenyewe, walichangishana wakapeleka matenki kule juu wakajenga wakatega maji kwenye maporomoko yale ya udongo na maji yakawa yanateremka wanatumia majumbani kwao.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi imekuja system ya mita, hatukatai kwamba lazima tuchangie maji. imefungwa system ya mita kwamba tunatakiwa kuchangia. Wananchi wanauliza swali kwamba miundombinu hii tulijenga sisi, tunaweza kuzungumza na Serikali, na RUWASA tukakubaliana tupate bei hata ya chini sana ya kuchangia bili za maji, kwa sababu wanaenda kutoza sehemu ambako RUWASA haikuweka fedha. RUWASA wanasema kwamba huko mbeleni ikitokea miundombinu imeharibika watakarabati, lakini tayari wanatumia maji miaka yote. Kwa hiyo, tunaomba sana suala la bili kwa wananchi wetu ambayo miundombinu ilikuwa ya kwao, ipitiwe upya, hasa elimu kabla ya kutoza ifanyiwe kazi, vinginevyo hali itakuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Spika, mwisho ni suala la mafuriko. Tumeona Ifakara juzi tumepata mafuriko na kila mwaka karibu tunapata mafuriko. Nami nilisema suala la mafuriko katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara ni suala mtambuka. Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji na Wizara ya Nishati mnaweza mkakaa mkajadili kuhusu yale mafuriko. Mamilioni ya lita za maji kila mwaka yanapotea kwenda kwenye mashamba ya watu na makazi ya watu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amefika mpaka kwenye kile kichaka cha Mto Kilombero ambacho kilikuwa kimezibwa. Namshukuru sana Engineer Bonde Emmanuel anafanya kazi nzuri, wamefukua pale, maji yanapita. Tuliomba Wizara ya Nishati, tunaomba Wizara ya Kilimo, na ninyi mfukue ule mto. Kwanza utaongeza maji. Fifty percent sasa hivi inachangia kwenye mto Kilombero ambao Mto kilombero, ambao unachangia sixty five percent kwenye Bwawa la Nyerere. Kwa hiyo, tutapelaka maji kujaza Bwawa la Nyerere; pili, kwenye kilimo watapata maji yale ambayo yanapotea kwenye mabwawa ya kilimo; tatu, maji yale yanaweza yakafanyiwa utaratibu mzuri, ninyi Wizara ya Maji mkayatumia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunasisitiza sana Mheshimiwa Waziri, mafuriko ya Ifakara haiwezi kuwa historia ya mazoea. Siyo kweli. Hata wazee wetu zamani walikuwa wanaboresha tuta na mafuriko yanapungua. Sasa msizoee yale mafuriko, naomba mkae kama Wizara tatu kwa pamoja na mkisaidiana katika jambo hilo, mfikirie, na Ifakara inaweza kuondokana na mafuriko.
Mheshimiwa Spika, mwisho, nawashukuru sana, naishia hapa. Mheshimiwa Wazri nakushukuru sana. Naomba Kiburubutu, naomba suala la bili za maji na mafuriko mnisaidie. (Makofi)