Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa na mimi ya kuchangia angalau kwenye Wizara hizi mbili niweze kusema maneno machache.
Kwanza nianze kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano, Mheshimiwa Rais pamoja na Baraza lake lote la Mawaziri kwa namna ya kipekee ambavyo wamekuwa wakifanya shughuli zao na kuwajibika kwa kiwango cha hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kuwashukuru sana wapigakura wa Jimbo la Nyamagana kwa kazi kubwa sana waliyoifanya. Niwahakikishie kwamba ninapokuja Bungeni hapa, nakuwa nimekuja kazini na kazi moja kubwa ni kusimamia na kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kuwalipa yale waliyoyafanya baada ya tarehe 25 Oktoba, 2015. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa shughuli nyingi za kimaendeleo ambazo imeendelea kuzifanya katika Jimbo la Nyamagana, lakini yapo mambo machache ambayo tunapaswa kushauriana na kuambizana ili tuweze kuyarekebisha na tuweze kuendelea vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze kidogo juu ya habari ya mapato, nizungumze juu ya habari ya ajira kwa vijana, lakini nizungumze juu ya namna ambavyo Halmashauri zinaweza kuongeza mapato kutokana na uwekezaji wa taasisi mbalimbali.
Sote tunafahamu, Jiji la Mwanza ni sehemu ya Mkoa wa Mwanza ambao ni mji wa pili kwa ukubwa Tanzania; lakini ni ukweli ule ule usiofichika kwamba Nyamagana na Jiji la Mwanza ndiyo mji unaokua kwa kasi zaidi Barani Afrika katika nchi yetu ya Tanzania. Tafsiri yake unaipata katika ongezeko la watu; 3% ya kuzaliana na 8.2% ya wahamiaji na wageni wanaoingia kila wakati kwenye Jiji la Mwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kuikumbusha Serikali yangu, Jimbo la Nyamagana ni sehemu ambayo ni kitovu cha Mikoa ya Kanda ya Ziwa. Unapoanza kuzungumza habari ya msongamano wa watu, habari ya msongamano wa vifaa wa vyombo vya usafiri, lakini habari ya msongamano wa wafanyabiashara ndogo ndogo ambao kwa kweli huwezi kuwaondoa kwa sababu ndiyo sehemu wanayoweza kupata fursa nyingi zaidi katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kuiomba Wizara ya TAMISEMI kwamba Halmashauri peke yake haiwezi kukabiliana na taizo hili, lakini kupitia masuala mbalimbali, kwa mfano, tunapozungumza juu ya uboreshaji wa Miji na upanuaji wa Mji, naiomba Wizara ya TAMISEMI kupitia kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene; mara kadhaa tumekuwa tunazungumza na unanipa ushirikiano wa kutosha, nakupongeza sana. Sina shaka Halmashauri hizi zimepata dawa ambayo kwa kweli ukiendelea hivi, naamini tutafikia kwenye lengo tunalolitazamia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko tatizo kubwa sana la wafanyabiashara ndogo ndogo na leo nitajikita hapa sana. Bila kutafuta ufumbuzi kutoka juu, bila kuisaidia Halmashauri kuweza kupanua Mji; tunapozungumza kupanua barabara ya kutokea Buhongwa kupita Kata ya Sahwa kwenda Lwanima, kutokea Igoma kuunganisha Fumagila kukamata barabara inayotoka Usagara kwenda Kisesa; tusipopanua Mji hatuwezi kuwaondoa machinga katikati ya Mji! Tusipopanua Mji hatuwezi kupanua fursa za vijana ambao wanapaswa kujitanua na kufuata yaliko makazi! Huwezi kuwaondoa machinga kuwapeleka sehemu ambako hakuna wakazi, hakuna watu, hakuna biashara! Inakuwa ni vigumu sana; lakini ndio wakwetu hawa, wanaingia kwa kasi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakumbuka miaka ya nyuma, ni miaka michache tu iliyopita, watu wengi walitumia nafasi hii kujinufaisha sana kupitia vijana hawa wanyonge na maskini wanaotafuta maisha yao ya kawaida. Kwa sababu waligundua ukweli na kuamini Chama cha Mapinduzi peke yake kupitia watu wake wanaweza kukisaidia, Nyamagana wameamua kufuta habari ya upinzani na wakakirudisha Chama cha Mapinduzi. Sasa ni lazima tuwatendee haki kwa kuwaboreshea miundombinu, kuimarisha maeneo yao ya biashara ili wafanye kazi zao vizuri na Mji ubaki unapumua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda naomba nizungumze juu ya uwekezaji. Tunafahamu Halmashauri hizi hazina mapato mengi. Nawashukuru sana LAPF kwa uwekezaji wao mzuri na mkubwa, nafahamu wamefanya Morogoro na baadaye wamekuja kufanya Mwanza. Tumefanikiwa kujenga Shopping Mall ya kisasa, Eastern Central Africa unaikuta Mwanza peke yake. Hii itatusaidia kuongeza ajira zaidi ya vijana 270.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni nini? Kuwepo kwa mall hii peke yake siyo tu kuongeza ajira, inaongeza kipato kwenye Halmashauri kwa sababu Halmashauri imewekeza kupitia ardhi yake, LAPF wamewekeza fedha. Kwa hiyo, tunagawana mapato siku ya mwisho na Halmashauri zinaendelea ku-generate income tofauti na kutegemea ushuru mchache ambao unatokana na kero mara nyingi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la afya. Sote tunafahamu namna ya kumlinda mama na mtoto wakati wanapojifungua. Tunapozungumza kuboresha zahanati na vituo vya afya, tunapozungumzia habari ya maduka ya dawa, tumeanzia ngazi ya juu sana. Hatukatai, ni vizuri hatua zimeanza kuchukuliwa, lakini unapoboresha kwenye Hospitali ya Mkoa ukasahau kuboresha kwenye Hospitali ya Wilaya, tafsiri yake ni kwamba mzigo wote wa Wilayani unaupeleka Mkoani; unaondoa chini huku ambako watu wengi wanahitaji msaada, hatuwezi kufanikiwa. Hii ndiyo maana tunasema, siyo rahisi sana, lakini tunajitahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi niwashukuru sana kwa kuanza kupeleka maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa. Hawa wakiwajibika na wao sawasawa Halmashauri zitapunguza mzigo kwa sababu watakuwa wanashirikiana katika kuhakikisha wanapeleka maendeleo kwa wananchi na mifano mizuri mnayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tu, kwenye Jimbo la Ilemela pale kwa mama yangu, Mama Angelina Mabula, iko zahanati moja ya muda mrefu, Zahanati ya Sangabuye. Zahanati hii imeanza kitambo, lakini mpaka leo inapata fedha za zahanati wakati ni kituo cha afya. Halikadhalika zahanati iliyoko kule Nyamuhungolo, hakuna wataalam lakini inavyo vifaa vyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie tu kwa kusema nikiwa naendelea na mimi nashangaa sana kwenye suala la elimu; tumesema elimu ni bure, watu wanalalamika. Wakati inaanzishwa, wakati tuko kwenye kampeni, watu walikuwa wanajinasibu kutoa elimu bure, leo wanashangaa Serikali ya CCM kutoa elimu bure, wanasema ni fedha za walipakodi. Unapozungumza elimu bure, tafsiri yake ni nini? Nani unataka atoe fedha mkononi kama siyo Serikali yenyewe? Na mimi nashangaa! Nilikuwa najiuliza, hawa watu ni kiumbe cha namna gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tukitaka kuangalia hapa; namshukuru sana Mheshimiwa Zitto Kabwe kwa kuona thamani na umuhimu wa elimu hii ambayo CCM imesema, elimu ya kuanzia chekechea, msingi na sekondari ni bure. Kwake kule kwenye Halmashauri akiwa na mwaka mmoja tu na Chama chake, amesisitiza kuanzia kidato cha tano na cha sita. Ninyi mna miaka 23 mmefanya nini kwenye elimu kama siyo kulalamika leo? Nimekuwa najiuliza, tunahangaika hapa, kila siku ni kutukana, kulalamika! Tunataka kujua! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ungetusaidia. Mara zote mimi nimejiuliza, hawa UKAWA ni viumbe wa namna gani? Ni chura au ni popo hawa? Maana ndiyo peke yake huwezi kujua! Chura anabadilika kila wakati, lakini kinyonga huwezi kujua! Kinyonga anabadilika kila wakati, lakini popo huwezi kujua kama ni ndege au ni mnyama? Kwa hiyo, hii tunaipata wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 22 Aprili, 2016 hapa Mwenyekiti wao alisema, katika mazingira kama haya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haiko tayari kuendelea kushiriki na uvunjaji wa Katiba, Sheria na haki za msingi za wananchi. Leo wanashiriki hapa, wameungana na sisi, hawajaungana na sisi? Ukishindwa kupambana naye, ungana naye. Hii ndiyo dhana halisi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hawa wameshashindwa kupambana na sisiā€¦
Nawashukuru kuendelea kuungana na sisi! Na mimi nakushukuru sana. Dhamira ya Chama hiki ni kuendelea kuongoza na kuweka maendeleo sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa namalizia, namshukuru sana Waziri wa Wizara ya Michezo, Habari, Sanaa na Utamaduni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Nyamagana tumehangaika kwa muda mrefu juu ya uwanja wetu wa Nyamagana, leo ninavyozungumza tayari nyasi ziko bandarini na muda mfupi kazi inaendelea katika uwanja wa michezo wa Nyamagana. Tafsiri yake, tunataka kuimarisha! Ukiimarisha michezo umekuza ajira kwa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.