Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Jonas Van Zeeland

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nianze kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uzima. Pili, nimshukuru sana ndugu yangu Mheshimiwa Aweso pamoja na Naibu wake, kwa kazi nzuri wanazozifanya kwenye Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Spika, sisi Mvomero, tuna miradi ambayo inaendelea ya zaidi ya shilingi bilioni 12. Nichukue nafasi hii pia kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mvomero, kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa kutupa fedha nyingi za Miradi ya Maji. Haijawahi kutokea kupata miradi mingi ya maji kwa pamoja kama ambavyo tumepata sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, yako mambo machache ambayo tutaomba utusaidie kwenye hii miradi ambayo wakandarasi wapo site wanaendelea na kazi. Mfano kule Kibogoji na Pandambili, mlitupatia milioni 530 na mradi ule umekamilika. Lakini kuna tatizo baadhi ya vituo havitoi maji na mradi huu hauna hata miezi mitatu, minne.

Mheshimiwa Spika, tuna Kijiji kimoja pale Dibuluma kipo katika Kata ya Kibati hakina maji kabisa. Tunaomba mtusaidie ili ili tuweze kuunganisha vijiji vyote vya kata ya Kibati viweze kupata maji. Tuna vijiji vya Ndole kule Kinda, Matale pale Mvomero mmetupatia milioni 978, tatizo pale bado kitongoji kimoja ambacho kipo kwenye mkataba wa mkandarasi, kitongoji kile hakijapata maji na mkandarasi hataki kuweka maji kwenye kile kitongoji. Nimekwisha zungumza sana na engineer wetu wa Mkoa na engineer wa wilaya lakini bado tatizo hili halijaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, kwa mara ya kwanza Tarafa ya Mgeta ambayo ina vyanzo vyenye uhakika vya maji, haikuwahi kupata miradi mingi kama ambavyo umetupatia safari hii. Mwaka 2021 nilismama hapa nikakuomba miradi mingi sana nashukuru sana mmetupa ile miradi. Tuna miradi kule Chenzema, Luale, Kibuko, Londo, Masalawe na Kibagala, mkandarasi anaendelea kazi ya shilingi bilioni 2.2 mkandarasi yuko kwa asilimia 60. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna changamoto hapa Mheshimiwa Waziri, mkandarasi huyu anapo rise certificate kwenu mnachelewa sana kumlipa. Kazi hii itachukua muda mrefu kama atacheleweshewa malipo yake. Naomba anapoleta certificate alipwe kwa wakati ili kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna mradi kule Lusungi – Mwalazi wa shilingi bilioni 2.3 mradi huu unakwenda kwenye vitongoji vya Nyabeni A na Nyabeni. Niliomba mwaka 2021 tunashukuru mmetupatia hizi fedha mkandarasi yuko kwa asilimia 25 na yeye anasuasua, ukimuuliza nini anasema malipo hajapata.

Mheshimiwa Spika, tuna mradi mkubwa na Mheshimiwa Waziri ulikuja Mvomero, wananchi wamefurahi sana ujio wako uliokuja kule Mvomero. Kazi kubwa ambayo tunaifanya ya kutoa maji kule Bunduki - Maguruwe yanapita Homboza – Mlali halafu yanakwenda Kipela, Kinyenzi, Mkuyuni, Lukuyu, Mgeta. Vijiji vingi vitapata maji kutokana na huu mradi isipokuwa kuna vijiji viwili ambavyo viko kwenye kata ya Mlali, Kijiji cha Vitonga na Lugono hamjaweka kwenye huu mradi.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, nikuombe sana ule mradi haiwezekani watu wa Kipela wapate maji, watu wa Mkuyuni wapate maji lakini watu wa Vitonga na Lugono wasipate maji wakati maji yatakuwa yamefika karibu kabisa na maeneo yao. Mheshimiwa Waziri, niombe sana tufanye marekebisho kidogo, mkandarasi aongezewe fedha aweze kufikisha maji kwenye hivi vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, Mheshimiwa Waziri, Tuliani tuna mradi mkubwa wa maji wa shilingi bilioni 3 na milioni 600, mkandarasi yupo site. Lakini nina wasi wasi na huyu mkandarasi atakuwa ni msanii mjanja mjanja. Kwa sababu mpaka sasa hivi amefanya kazi chini ya asilimia 10. Mradi wa bilioni 3.6 atamaliza mwaka gani? Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri, Wizara yako imchunguze huyu mkandarasi nina wasi wasi nae.

Mheshimiwa Spika, pia kwenye Mradi wa TUILIWASA ambao huyu mkandarasi wa bilioni 3.6 anakwenda kusambaza maji kwenye Tarafa nzima ya Tuliani. Tatizo la ule Mradi wa TULIWASA bili ambazo wananchi wanalipa, wanaletewa bili mwisho wa mwezi baada ya kutumia ni kubwa sana. Huu mradi haya maji ni ya mseleleko sio maji ya kuvuta na umeme. Hayana gharama kubwa sana kuyapata haya maji.

Mheshimiwa Spika, kwa mwezi wanapewa bili kubwa kiasi kwamba wanashindwa kulipa, wengine sasa hivi wanaanza kutumia visiwa. Watu wa TULIWASA wanaanza kuwakamata watu ambao wanataka kuwasaidia wananchi kuwachimbia visima. Sasa kama wao wanashindwa kuja na bei ambayo mwananchi wa kawaida ataweza kulipa mwisho wa mwezi, wawaache hawa wananchi wakitaka kutumia visima watumie visima. Kama wanataka washushe unit moja ya maji iende mpaka 840 ili wananchi waweze kulipa mwisho wa mwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia tuna mradi mkubwa pale Dakawa wa bilioni 2.3. Mkandarasi amesaini mkataba huu mwezi wa pili anasuasua tu hatujui tatizo ni nini? Leo nimezungumza na Injiania wa Mkoa amenihakikishia wiki ijayo ataanza kazi wako kwenye makabidhiano. Sasa miezi miwili fedha za Mheshimiwa Rais zimeletwa ziko pale mkandarasi haeleweki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunashukuru sana mmetupatia fedha za kuchimba vizima tisa kwa milioni 378, tumechimba kule Msongozi. Kata ya Msongozi ina tatizo kubwa sana la maji. Pia pale Magali, Melela, lugono, Makuyu kule Mvomero, Milama, Manza na Sokoine.

Mheshimiwa Spika, kipekee nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri, nilikuomba utusaidie kutupatia fedha kwa ajili ya kutatua tatizo la Maji pale Sokoine. Wananchi wa Sokoine walikwa wanakunywa maji na Wanyama. Ziko clip ambazo nilikutumia Mheshimiwa Waziri na nilikuomba utusaidie, ukatupatia mitambo imechimba visima virefu na sasa hivi wanaendelea na ujenzi, wanajenga chumba kikubwa kwa ajili ya kuhifadhi mashine lakini wanajenga pia na tank kwa ajili ya kuhifadhia maji waanze kusambaza kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, niombe sana msukumo wako kwa sababu wananchi wa Sokoine wameteseka kwa muda mrefu kwenye adha ya maji. Niombe msukumo wako kwa huyu ambae anasimamia pale mradi, ahakikishe kwamba mradi huu ikiwezekana mwezi wa saba kama ulivyotuahidi ulivyokuja Mvomero ili wananchi waanze kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda Mvomero tuna shida ya gari. Mheshimiwa Waziri, hatuna gari, injinia wetu ana gari bovu halijapata kutokea. Tunaomba utupe gari ili injia aweze kukimbia kimbia. Kwa sababu ya jiografia yetu nafikiri unaijua vizuri…

SPIKA: Mheshimiwa Jonas, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana naunga mkono hoja.