Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema aliye nijalia afya niweze kusimama tena kwenye Bunge lako tukufu. Niungane na Wabunge wenzangu kukushukuru sana kwa namna ambavyo unatuongoza sisi Wabunge wenzio. Binafsi kama Mbunge mwanamke najivunia sana napoona kazi unayoifanya hatutapata kazi ngumu sana sasa juu ya kutambua nafasi ya mwanamke kwenye uongozi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kusema uongozi ni pamoja na kuwasikiliza wenzio. Mheshimiwa Waziri wa Maji umekuwa unatuonyesha mfano kila siku, umekuwa ni mtu ambaye unasikiliza na unaamini kila mtu katika ushauri wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na usikivu huo kuna salamu kutoka kwa wana Nkasi Kaskazini, wanatambua ulipokuja ukiwa Naibu Waziri wa maji tukakueleza changamoto ya Maji ukatuambia ni namna gani utaanza kutekeleza mradi wa Kirando ukakamilika, wakakwambia kwa sababu umekamilika utaenda kuwa Waziri baada ya wiki mbili ulivyokuja ukawa Waziri. Siyo kwa sababu wanajua kuomba ni kwa sababu maneno ya kusema ubarikiwe huwa yanatoa baraka kwa watu wengi na jambo lako linafanikiwa. Tunatumaini kwamba kama umekaa muda wote huu ujabadilika huwezi kubadilika tunakushukuru kwa namna ambavyo unafikaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nianze na suala la Ziwa Tanganyika, leo nazungumza hapa nafikili ni zaidi ya mara tisa sasa. Kwa nini tunasema maji yatoke Ziwa Tanganyika? Natambua jitihada za Serikali kwenye jimbo langu juu ya kutatua changamoto ya maji. Mpaka sasa kwenye miradi inayoendelea, iliyopo kwenye matazamio na iliyokamilika kwa miaka mitano tu ni zaidi ya bilioni 18 lakini kata tano peke yake za pale mjini ambazo ndiyo sura ya Wilaya yetu ya Nkasi. Ukitaja hizo asilimia za upatikanaji wa maji vijijini watu wa Nkasi hawapendi hata kusikia hizo asilimia. Kwa sababu mpaka jana nawauliza watalamu wangu, mahitaji ya tano peke yake kati ya kata 17 ni lita 2,900,000 kwa siku yanayopatika ni lita 194 sawa na asilimia saba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa nini tunasema maji yatoke Ziwa Tanganyika? Serikali imesha onyesha jitihida ya kutatua changamoto ya maji lakini fedha nyingi zinatumika kwenye kutafuta vyanzo vya maji na vyanzo vyenyewe kwa kuwa siyo vya uhakika kwa fedha zinaonekana hazijafikia yale ambayo watanzania tunategemea, wana Nkasi tunarajia kupata maji.
Mheshimiwa Spika, mwaka jana Mheshimiwa Waziri alikuja kule, alivyokuja kuna mradi ulikuwa umekwama wa Bwawa la Mufindi, nikamwambia na mkandarasi amesimama kwa sababu hajalipwa. Siku hiyo hiyo Mheshimiwa Waziri aliagiza yule mtu amaliziwe fedha zake. Ule mradi baada ya kumaliziwa umefanya kazi miezi mitatu tu, maji hakuna Bwawa limekauka. Kwa sababu lengo letu ni kushauri kutoka Kilando kuja Namanyele, Kilando ndiko kwenye ziwa Tanganyika, kuja Namanyele ni kilomita 64 kuleta maji pale. Tunahitaji muujiza gani? Nchi yetu haina shida ya vyanzo kilichobaki ni uthubutu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano iliweza kuthubutu kutoa maji ziwa Victoria kufikisha mpaka Tabora ni umbali mrefu sana. Nini kinashindikana leo? Kilomita 64 tu wananchi waendelee kulia?
Mheshimiwa Spika, pamoja na yote anayoendelea kuyafanya Mheshimiwa Waziri, naomba nitoe mifano michache tu, kwamba kwenye hizi kata tano, Kata ya Namanyele peke yake hakuna kisima cha uhakika hata kimoja. Kijiji cha Mkangale wanatamani wapate majibu yao leo, kwamba na wao ni Watanzania hivyo wanahitaji kupata maji. Hakuna mbadala wa maji, huwezi kutumia soda badala ya maji, haiwezekani.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba hiyo dhamira inaonekana; najua kwamba Serikali ina mpango wa muda mrefu na mpango wa muda mfupi; mpango wa muda mfupi, wameomba fedha bilioni tano kwa ajili ya bwawa jingine; tunaomba kwenye hilo usisite. Lakini walichoniagiza leo wanaamini suluhisho la wilaya ya Nkasi Mkoa wa Rukwa, Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Kigoma ni kutoa maji Ziwa Tanganyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kata ya Kipundu Kijiji cha Kakomwa hawana mbadala. Yaani sasa hivi unaona hii pressure imepungua ya mimi kukusumbua ni kwa sababu mvua bado inanyesha, ikikata tu pressure inarudi pale pale. Mheshimiwa Waziri tunakuomba, kwa sababu umeshaonesha nia tangu mwanzo, tunaomba tuione dhamira kwa kuwasaidia wanawake, kwa kuwasaidia watu wa Nkasi.
Mheshimiwa Spika, aliyeanzisha kauli hii ya kumtua mwanamke ndoo kichwani ni Rais wetu akiwa Makamu wa Rais. Leo aliyeanzisha ile kauli ndiye Rais mwenyewe, mwanamke. Mbunge wa Jimbo mwanamke, Spika wa Bunge ambako nasema leo mwanamke, Katibu Mkuu Wizara yako mwanamke; sasa tunategemea hayo mambo yatafanyika vizuri ili neno hilo tuliishi kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, fedha zinazotumika kutafuta vyanzo vya maji ni nyingi sana, na hakuna sababu ya kufanya hivyo. Pamoja na kwamba kuna fedha ambazo zinatumika kwenye kuchimba visima; naomba nitoe mfano mdogo tu, mwaka wa fedha mwaka 2021/2022 DUWASA walidhamiria kuchimba visima 250. Katika visima 250, kwa sababu tunahangaika na vyanzo vya muda mfupi, asilimia 23 visima hivyo vilikuwa havina tija, kutokana na ripoti ya CAG, asilimia 18 havikufanyiwa majaribio, asilimia 16 havikuchimbwa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mazingira haya tumepoteza shilingi milioni 354.9 kwa ajili ya kuwalipa wakandarasi kwa kazi ambazo hazikufanyika. Wakati huo watu wanalipwa kuna maeneo ambayo upatikanaji wa maji ni asilimia saba. Jambo hili halifurahishi hata kidogo. Kama shida ni usimamizi kuna haja ya kuabdilisha ya approach ya usimamizi. Lakini kwa nini tuendelee kuchimba visima wakati vyanzo vipo vya uhakika? Kwa nini, tyuendelee kupoteza feha wakati vyanzo vya uhakika vipo?
Mheshimiwa Spika, Wizara walijiwekea malengo, pamoja na kwamba kiwango cha upotevu wa maji kipo katika kiwango kinachokubalika kwa asilimia 20, Wizara wamejiwekea malengo kufika 2022 angalau upotevu wa maji uwe asilimia 28. Kupitia ripoti ya CAG ya Machi, 2023 katika mamlaka za maji nane zilizokaguliwa ni mamlaka moja tu ambayo ilikuwa imefikia kiwango cha upotevu wa maji asilimia 20; Mamlaka ya Moshi. Hizi mamlaka saba zote bado tunarudi kulekule. Hii ni 2023, kwa hiyo hata Wizara malengo yenu bado hamjayafikia kwenye suala la upotevu wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni nini kinapelekea tufike huko? Kwenye upotevu kwa miaka miwili tu, hizo mamlaka nane ambazo zilikaguliwa tumepoteza kiasi cha shilingi bilioni 118.13. Hizo fedha kama ingekuwa si kupoteza kwenye kutafuta vyanzo zingesaidia maeneo mengine ikiwepo Nkasi ambao tuna uhitaji mkubwa wa maji.
Mheshimiwa Spika, kwa nini tumefikia huko? Aidha tunabahatisha au watalamu wetu wanashindwa kutimiza wajibu wao. Ninarudia tena, kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi mmesema mtatumia vyanzo vya uhakika kumaliza changamoto ya maji. Kama ndivyo tunasubiri nini kwenye hili jambo? Tutazungumza mpaka lini? Hivi kwa hali ya kawaida mtu akaja anasikia mimi nazungumza zaidi ya mara tisa kuhusu kutoa maji Ziwa Tanganyika, kilometa 64, tunahitaji muujiza gani kwenye hili jambo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, fedha ya dharura milioni 200 imekwenda mwezi wa tisa mwaka jana, hakuna hata kisima kimoja kinatoa maji nazungumza hapa. Tufanye nini? Haya mambo hayakubaliki, tunaomba ni bora fedha zikatengwa za kutosha tuanze kufikiria suala la maji miaka 100 ijayo kuhusu kufikiria hili jambo ambalo tunazungumza kila siku kwenye hili Bunge. Jana, leo, kesho na kesho kutwa changamoto ya maji. Vyanzo vipo tunaomba Wizara uthubutu ndio unaohitajika. Nakushukuru sana.