Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, na mimi nishukuru kwa kupata nafasi hii jioni ya leo. Nikupongeze wewe binafsi kama ambavyo Wabunge wenzangu wamekupongeza, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anazozifanya pamoja na kusimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri, Naibu wake, Katibu Mkuu Wizara hii na Katibu Mkuu aliyeondoka, lakini na watendaji wote wa Wizara ya Maji wakiwemo injinia wetu wa mkoa pamoja na injinia wa Wilaya Ndugu Juma. (Makofi).
Mheshimiwa Spika, ukiangalia tone ya Waheshimiwa Wabunge, mimi nimepata nafasi ya kuchangia mwishoni kabisa, tunaelekea mwisho sasa. Ukiangalia tone ya Waheshimiwa Wabunge wote humu ndani sioni kama kuna mashaka kwa Mheshimiwa Waziri kupitishiwa Bajeti yake, tena naamini kwa kishindo kikubwa sana. Kwa sababu ukiangalia tone ya leo na miaka mitatu, minne, mitano iliyopita nyuma Waheshimiwa Wabunge wengi sana wameridhika, na nimeona kila mkoa kuna mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa, ikiwemo pamoja na Mkoa wetu wa Mtwara.
Mheshimiwa Spika, Mzee Mkuchika angepata nafasi ya kusema hapa Bungeni kama wangekuwa wanatoa ruhusa mawaziri kuchangia nafikiri angedondosha machozi kwa furaha. Kwa sababu katika kipindi chake chote cha uongozi alipokuwa anafanya mikutano Newala, huyu Mzee wetu sikumbuki vizuri lakini walikuwa wanamuita kwa kimakonde Nangudyamedi kitu kama hicho, yaani wakiwa na maana kwamba wakati wa mkutano wananchi wasilmuulize swali linalohusiana na mambo ya maji kwa sababu hataweza kulijibu sababu Newala ilikuwa haipatikani maji kabisa. Ndiyo maana Mheshimiwa Hokororo jana hapa alisema kuwa Newala ndiko ambako wananchi walikuwa wanapika chakula kwa kutumia maji ya matiki maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kwa mradi huu mkubwa unaokwenda kutekelezwa sasa hivi wa Makonde utakaohudumia Wilaya zile nne, ninaamini ni ukombozi mkubwa sana kwa sisi watu wa Mtwara.
Mheshimiwa Spika, nimuombe pia Mheshimiwa Waziri, kwamba mradi huu wa Makonde ni mkubwa sana, utekelezwe kwa wakati, fedha ziende kwa wakati lakini tuangalie na mipango ya muda mrefu. Pamoja na sisi watu wa Ndanda na Masasi, Ruangwa, Nachingwea na wengine wote waliosema, tunajivunia maji ya Mbwinji lakini mradi wa Makonde ungeweza kuleta pia maji maeneo haya, kwa sababu Mto Ruvuma maji yake yamekuwa ya kuhama hama. Pamoja na kwamba mradi unakwenda kutekelezwa lakini chanzo cha maji cha Makonde ni cha uhakika zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna miradi inayotekelezwa Jimbo la Ndanda; kuna mradi wa Chija Chiwata, Chija Mbemba, Ndanda hadi Nangoo, Mradi wa Nanganga Momburu, mradi wa Nambawala ambako mafundi wako wanachimba mitaro sasa hivi, pamoja na mradi wa Namalembo. Niombe sana pesa ziende sasa kwa wakati, kwa maana ya kwamba uangalie cash flow miradi hii itekelezwe ili wananchi waweze kupata maji. Lakini pia tuna maombi. Kuna visima ambavyo vilishachimbwa tayari kwenye vijiji vya Mpanyani, Chilolo, Masiku, Namichi Pamoja Sululu ya leo. Mruhusu Meneja wa Mkoa na Meneja wa Wilaya waweke pale solar pans ili wananchi waweze kuanza kupata maji wakati michakato hiyo ya kutaka miradi hii iwe mikubwa ya kuhudumia eneo kubwa iweze kukamilika.
Mheshimiwa Spika, tuna mradi pia wa Mwena Lihoya, umekuwa unasua sua, lakini tunaziona hatua za kuboresha mradi huu. Mheshimiwa naomba ukafanye marejeo kwenye mradi ule, ili wapelekewe fedha mradi huu ukamilike ili uweze kutoa maji ya uhakika kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, kuna miradi inayoendelea Jimbo la Tandahimba na Mheshimiwa Katani hujamuona unakumbuka, nafikiri unaamini tone yake ile ya mwaka jana lakini anasema anajipanga kwenye Wizara ya Miundombinu kwa sababu ya barabara zetu kule, mpaka sasa hatuna jibu la uhakika. Wizara ya maji ameamua apumzike kwanza kwa sababu miradi ya maji jimboni kwake inaenda vizuri sana. Vilevile tunangalie cash flow tuweze kuwapelekea maji watu hawa na fedha kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na mazuri yote unayoyafanya, mimi binafsi niombe tumsaidie Meneja wetu wa Wilaya kutekeleza majukumu yake vizuri Eng. Juma kwa kumpatia gari litakalofaa. Tunapokwenda kufanya ziara kwenye Wilaya ya Masasi yenye miradi mikubwa zaidi ya kumi, yenye zaidi ya fedha bilioni 15 ndugu yetu huyu kuna wakati anafika kwenye ziara akiwa kwenye pikipiki kwa sababu gari lake ni bovu, halitengenezeki na liko beyond repair. Tunaomba apatiwe gari jingine ili aweze kusimamia majukumu yake sawasawa na tufanye nae ziara kwa uhakika.
Mheshimiwa Spika, nakumbuka siku moja nimeenda kwenye mkutano wa hadhara na kulikuwa kuna masuala yanayohusiana na masuala yanayohusiana na mambo ya maji Chibya. Tuko katikati ya mkutano namuona Injinia wangu anakuja na pikipiki, bodaboda. maana gari lake imeharibika kwenye milima huko chini, ameshindwa kufika kwenye mkutano kwa wakati, kwa hiyo nikuombe umsaidie.
Mheshimiwa Spika, bado tuna mahitaji makubwa sana ya visima, unafahamu jiografia ya Jimbo la Ndanda kuna eneo la upande wa Magharibi wa jimbo kunashida sana ya maji. Pamoja na mafanikio mazuri hivyo visima alivyovitaja vipo maeneo hayo lakini bado tuna mahitaji ya visima kwenye Vijiji vya Migombani, Pangani, Pachani, Miwale Namatutwe, Natepo, Mihima, Makulani ya Leo pamoja na Chimbo. Niombe sana kwenye Bajeti hii ijayo, tuone watu hawa wanakwenda kupata maji, na kwa kutekeleza miradi hiyo kwa kuchimba visima virefu kwenye maeneo haya, tafsiri yake itakuwa tumemaliza kabisa tatizo la maji kwenye ukanda wa Magharibi wa Jimbo la Ndanda.
Mheshimiwa Spika, na Mheshimiwa Waziri ni msikivu sana. Mara nyingi sisi kama Wabunge wa Mtwara tukwenda kwake tukiwa tuna malalamiko, lakini nadhani safri hii mpaka tunakuja hapa ndani hatuna tena malalamiko yale na wala hatujakaa kikao maalumu na yeye ili aweze kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunachoomba sasa miradi hii ikatekelezwe kwa wakati. Kama unavyofahamu, mwakani kuna uchaguzi mkuu, maeneo haya yamepata shida kwa kipindi kurefu sana, tangu wakati wa uhuru. Newala hawajawahi kuwa na maji ya kutosha, Nanyamba hawajawahi kuwa na maji ya kutosha na Tandahimba hawajawahi kuwa na maji ya kutosha. Ndiyo maana maeneo haya kulikuwa kuna dominance kidogo ya watu wa opposition. Tunakwenda kwenye uchaguzi wa ndani, kwa maana ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, lakini pia tunakwenda kwenye uchaguzi mkuu. Tunaomba miradi hii ikamilike kwa wakati ili wananchi wapate maji wasije wakatulaumu, tusije tukapoteza maeneo yetu kwa sababu ya kiu kuu inayotamalaki katika maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilisema tangu mwanzo, nimesimama hapa, na Waheshimiwa Wabunge wengi wameongea kwa kipindi kirefu wakimpongeza Mheshimiwa Waziri. Nimsisitize tu, kwamba akamilishe miradi hii ili tukae hapa ndani kwa amani kiabisa. Ninaamini mpaka tutakaporudi kwenye bajeti ijayo Mungu akimjalia kuwa hai na sisi kuwa hai basi mambo yatakuwa mazuri. Miradi itakuwa imetekelezwa kwenye Jimbo letu na Ilani ya chama chetu chama tukufu, Chama cha Mapinduzi tutasimama kifua mbele tukikitetea kwa sababu tayari tutakuwa tumepunguza baadhi ya kero kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo na mimi niungane na wabunge wote waliopita kuunga mkono bajeti hii kwa asilimia 100. Ahsante sana kwa kunisikiliza.