Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Liwale
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nami nikushukuru kwa jioni hii kunipa nafasi nichangie hoja iliyo mbele yetu. Nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyokwenda na kauli yake ya kumtua ndoo mama kichwani. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, lakini Mheshimiwa Waziri na Naibu wake wana sifa ya ziada, wanapokea simu za Wabunge na wanafikika, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimesimama hapa niombe, Mheshimiwa Waziri, tuna Mradi wa Maji kwa ajili ya Mji wa Liwale. Sisi Mji wa Liwale hatuna mitaa, tuna vijiji; tuna Kijiji cha Kuchocholokana, Kulia, Kongowele, Nganyaga, Msufini, Kilipwike, Kitamamui, Tepetepe, Msufini, Mbonde, Kinguruila na Laluleo, zaidi ya vijiji 12 havina maji Liwale Mjini. Chanzo pekee tunachokitumia ni cha Mto Liwale. Mto ule masika tu ndio unatumika, kiangazi mto ule hautiririshi maji unakauka. Tunapata shida sana Mji wa Liwale.
Mheshimiwa Spika, tunamshukuru Waziri na tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutupa fedha na tayari tumeshachimba visima vitatu pale Turuki na vina maji ya kutosha. Kinachosubiriwa ni kutupatia fedha na mradi ule nafikiri gharama yake kama sio bilioni moja ni kama bilioni mbili, lakini nimeongea na Mhandisi anasema akipata hata milioni 500 ule mradi unakwenda kuanza. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, hili ndio jambo ambalo limenisimamisha kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nimpe taarifa Mheshimiwa Waziri, tunapokwenda kufikiria kuyatoa maji Mto Rufiji kuyaleta Dar-es-Salaam, afikirie kuyatoa maji hayo hayo kuyapeleka mikoa ya Lindi na Mtwara. Isije ikatokea huko nyuma watu wa Mtwara na Lindi wakaanza kulalamika kama leo tunavyoilalamikia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwamba, Mkoa wa Lindi na Mtwara ulisahaulika. Basi, Wizara hii isiwemo kwenye list ya Mkoa wa Lindi na Mtwara kusahauliwa kwenye miradi hii ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri. Wilaya ya Liwale yenye vijiji 76, leo unasimama hapa havifiki vijiji 20 ambavyo havina maji. Asilimia zaidi ya 70 kama sio 80 vina miradi ya maji. Nimpongeze sana na hii nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutimiza kauli yake hii. Tunavyo vijiji vinane tayari wakandarasi wako site na tuna vijiji zaidi ya vinne tayari miradi imeshakamilika. Kwenye bajeti hii nimeona vijiji zaidi ya vinne vinakwenda kupata miradi mipya ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi langu, miradi hii iende ikakamilike kwa wakati. Kuna mradi wa Makata, mradi huu umesuasua kwa muda mrefu sana. Kuna Mradi wa Kiangara na Mradi wa Nangano, miradi hii ni ya muda mrefu inakwenda kwa kusuasua sana. Nimwombe sana Waziri, miradi hii iende kukamilika ili azma ya Mama ya kumtua mama ndoo kichwani iweze kukamilika.
Mheshimiwa Spika, kitu kingine ambacho nataka niseme kwamba, katika Wizara hii sio tu Mheshimiwa Waziri mwenyewe na Naibu wake na Katibu Mkuu wake wanafanya vizuri, lakini hata safu aliyonayo kuanzia ngazi ya Taifa mpaka Halmashauri. Ndiyo maana kila Mbunge akisimama hapa anasema Mhandisi aliyenaye kule kwenye Halmashauri yake asihamishwe anafanya vizuri na wanafanya vizuri. Kama kuna rehabilitation imefanywa kwenye Wizara hii, Wizara ya Maji wanafanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niliomba dakika tano nisema haya machache niliyosema, hivyo, naunga mkono hoja, lakini nahitaji maji kwenye Mji wa Liwale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)