Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Maji. Ninaomba nikupongeze sana kwa namna ambavyo, unajua watu wengi wanafikiri tunakupongeza kwa kuendesha Bunge, kwa namna unavyotuongoza sisi Wabunge ndani ya Bunge na nje ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wameshazungumza, tumetoa pongezi na ahsante nyingi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo anamwaga pesa kwenye miradi mbalimbali, hususan kwenye miradi ya maji.

Mheshimiwa Spika, ukitazama hata namna ambavyo Mheshimiwa Rais anaipanga kiuongozi Wizara ya Maji unaona nia ya Rais ni kuongeza speed ya utendaji katika Wizara hiyo. Tumeona juzi hapa Mheshimiwa Rais amemteua Eng. Luhemeja kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji. Tunaona nia nzuri ya Rais ya kuifanya Wizara iwe imara katika utendaji. Waziri amekaa sawasawa, Naibu yuko sawa, sasa mnaongezewa nguvu, Katibu Mkuu amekuja ili mtoke pale alipoishia Eng. Sanga kwenda mbele kwa spidi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wabunge wamepiga kelele sana kuhusu maji kwa sababu maji hayana mbadala. Hata wale ambao hawakupata nafasi ya kuzungumza bado ungewasimamisha wote wangetaka maji kwenye Majimbo yao. Kwa hiyo, tunamuomba sana Mheshimiwa Waziri kuigawanya rasilimali maji.

Mheshimiwa Spika, unajua tumemaliza sensa juzi. Sensa itupeleke kuona wingi wa watu na namna ya kujenga matenki makubwa, tuondoke tena kwenye yale matenki madogo ya lita 50,000, lita 60,000. Tuanze sasa kujenga lita 200,000 na kuendelea ili yaweze kusaidia kusukuma maji kwa wingi katika vijiji.

Mheshimiwa Spika, leo kuna miji imekua. Ukiangalia sasa hivi kwa mujibu wa sensa iliyopita Kijiji kama cha Mkwayungu katika Jimbo langu, kina watu 19,000, Mvumi Mission kuna watu 19,000, ukienda Mlowa kuna watu 18,000. Hapa huwezi kutengeneza tena tenki la lita 50,000 likatosha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo rai yangu kwa Wizara, ikiwezekana tubadili sasa ujenzi wa matenki tuende tujenge matenki makubwa kwenye vijiji vyote ambayo mengine yatabaki kama reserve. Kama kijiji kina watu wachache, watakapoongezeka tenki tusijenge tena kwa sababu lipo la kutosheleza kusukuma maji kwa ajili ya kijiji hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa Dodoma tunapongeza sana uongozi wa maji wa Mkoa wa Dodoma, wanajitahidi sana. Nanyi Wabunge ni mashahidi na wengi muda mrefu tuko hapa. Lakini tunaona bado maji hayatutoshi. Kulikuwa kuna mpango wa kuyachukua maji kutoka Mtera kuyaleta hapa Dodoma Mjini. Nataka kupata majibu ya Mheshimiwa Waziri mmefikia wapi? Kwa sababu maji yale yakichukuliwa kwenye Bwawa la Mtera kuyaleta hapa Dodoma yatanufaisha vijiji vyangu vingi kule njiani yatakakopita. Kwanza tutambue kwamba kuna vijiji kuanzia kwenye Jimbo la Kibakwe kwa Mheshimiwa Simbachawene, ukanda ule wote, vijiji vile vina maji ya chumvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ukitupitishia maji kutoka Bwawa la Mtera maana yake Vijiji kuanzia Fufu, Isima kwa Mheshimiwa Simbachawene, Chipogoro kwa Mheshimiwa Simbachawene, ukija kwangu Manzase, ukija Mlodaa, Mlowa, Ng’wenda, wote watapata maji safi na salama. Kwa hiyo, naomba majibu utakaposimama Mheshimiwa Waziri utusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna vijiji tumefanya utafiti na kuchimba maji hayapatikani. Kijiji kama Chinoje tumechimba zaidi ya mara tatu maji yako mbali. Tumechimba maji kwenye Kijiji cha Ng’wenda, zaidi ya mara tano, maji hayapatikani. Ni nia yangu kuiomba Wizara tutoe maji kwenye vijiji jirani kupeleka huduma ya maji. Kumbe wale wananchi wahame wote, waende wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nataka kuiomba Wizara ni ukamilishaji wa miradi mikubwa ambayo imeanza kujengwa mingi imesimama kwa sababu ya kukosa pesa. Pale Mvumi Mission tunao mradi wa milioni 988. Mkandarasi ameshajenga, ame-raise certificate Wizarani ya milioni 522 mpaka sasa hivi hamjampatia, matokeo yake mradi umesimama.

Mheshimiwa Spika, vilevile ukienda Handali kuna tatizo pale. Mkandarasi yule pale tangu mmempa ile kazi ameweka mabomba halafu ameingia mitini. Mtusaidie, hii miradi kadri inavyochelewa inaongeza gharama ya utendaji. Ukienda Mlowa Bwawani pale tulikuwa tunatengeneza tenki, mifuko 200 ya simenti imekauka. Kwa hiy,o tunapata gharama inakuwa kubwa inazidi ile ya mwanzo ambayo mlikuwa mmeikisia kwa ajili ya kujenga mradi.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Chamwino ndiyo Wilaya yenye Ikulu. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri utupatie gari, meneja wetu pale hana gari. Na ile Wilaya ndiyo Wilaya ya kimkakati wewe unajua na Mama anakaa pale. Mimi sitaki kuwasemea kwa Mama, hebu tupatieni gari jipya ili yule Meneja aweze kukimbia kwenye Majimbo yote mawili kwa wakati muafaka na aweze kutupatia maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu bei ya maji. Wakati mwingine wanakurupuka tu watu wanajipangia bei ya maji. Maji siyo biashara, maji ni huduma. Kwa hiyo tumuombe Mheshimiwa Waziri, hebu elekeza mameneja wako hawa bei ya uhakika ya maji ni ipi, kwa sababu maji ni huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda huku unit ni shilingi 2,000, kwingine unit ni shilingi 2,500, kwingine unit ni shilingi 3,000, haiwezekani! Tuwe na bei moja maana maji ni ibada, maji ni uhai. Yakiwepo maji ya kutosha, safi na salama, yatapunguza hata bajeti ya baadhi ya Wizara, magonjwa ya maji haya kama typhoid yote yatatoweka tukiwa na maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia akina mama ukiwapunguzia muda wanaopotoza wa kutafuta maji, nikuhakikishie kwamba uchumi wa nchi yetu utakua kwa sababu akina mama ni jeshi kubwa, likishiriki kwenye maendeleo na kuacha kupoteza muda kwenye maji, mambo yetu yatakwenda kwa speed sana kwenye kuiendeleza nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri wataalam wakuletee idadi ya visima vya maji vya zamani ambavyo mitambo yake ni chakavu ili muweze kutu-boost kama mlivyofanya kwenye elimu. Umesema kwenye hotuba yako kwamba tunataka tutengeneze utaratibu wa kuvuna maji. Hebu tuanze na Serikali, kwanza hapa Bungeni tunavuna maji kutoka wapi kuja hapa? Bunge hili linavuna maji kutoka wapi?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo miundombinu ianzie Serikalini, majengo yote ya shule yawe na namna ya kuvuna maji. Kwenye Wizara zenu tukija tukute mifumo ya kuvuna maji, halafu wananchi ndiyo wataiga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mkituambia tu sisi tutengeneze structures za kuvuna maji wakati tukienda kwenye Wizara zenu, kwa Mheshimiwa Jenista pale, hakuna mfumo wa kuvuna maji, ndiyo wanaanza kuweka juzi hapa. Tukienda kwa Mheshimiwa Doto pale, hakuna mfumo wa kuvuna maji, kwa Mheshimiwa Simbachawene hakuna, sasa tunajifunza wapi? Tuanzie kwenu, ninyi muanze kuonesha njia ili sisi tufuate. Majengo yote ya Serikali yatengenezewe mfumo wa kuvuna maji halafu sisi wananchi tutaiga. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii. (Makofi)