Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makambako
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kuniona na kunipa nafasi niweze kuungana na Wabunge wenzangu kuchangia katika Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, Wabunge wote hapa waliapata muda wa kuchangia wamezungumzia kwanza, kila aliyeanza anampongeza Rais. Kwa nini tunampongeza Rais? Tunampongeza Rais kwa sababu ana nia njema ya kuhakikisha anamtua mama ndoo kichwani. Ndiyo maana kwenye Wizara hii ameongeza fedha kutoka shilingi bilioni 708 za mwaka jana, mwaka huu ameongeza shilingi bilioni 756. Hizi tunazungumzia siyo milioni, haya ni ma-‘bi’ na ma-‘bi’ na ma-‘b’. Ndiyo maana tunampongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, vilevile tunampongeza aliyekabidhiwa hii Wizara, Amekabidhiwa kijana wetu, Waziri huyu anaitendea haki Wizara. Anaisimamia vizuri pamoja na Naibu Waziri wake. Vilevile wako watendaji wake, yupo Katibu Mkuu wa Wizara na Naibu Katibu Mkuu na Watendaji wote walioko Mikoani na Wilayani akiwemo wa Mkoani kwangu Njombe na Wilayani kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Aweso kweli wewe umekabidhiwa dhima hii ya kuhakikisha unamtua mama ndoo kichwani. Ombi langu Waziri, ma ‘B’ haya uliyokabidhiwa yanayokwenda huko kwenye Majimbo yetu yasimamie vizuri yasiliwe. Kazi hiyo unaiweza kwa sababu umedhamiria, tunakuona una nia njema, tunakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika miradi ile ya miji 28 na Mji wa Makambako umo. Katika Mji wa Makambako tumepewa katika miradi wa miji hiyo 28 ma ‘B’ 42. Sasa utakaposimama hapa Wanamakambako wana hamu kukusikia, miradi hii inaanza lini? Useme. Utakaposema waambie Wanamakambako kwamba sasa, maana mradi huu mkubwa wa Makambako unahudumia Kata Tisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, ombi langu utakaposema katika Kata tisa, Kata moja ya Mlowa imo katika hizi Kata Tisa. Katika fedha za kujenga tenki kubwa la kuhudumia, tenki moja linatakiwa liwe kule Mlowa ambalo litahudumia katika kiwanda cha dawa kilichojengwa Makambako, litahudumia katika Hospitali ya Halmashauri yetu iliyojengwa katika Kata hii ya Mlowa na wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, tuliomba fedha zaidi ya bilioni tatu na milioni mia tatu kwa ajili ya bajeti ya mwaka huu ili waanze kujenga tenki hilo kubwa la zaidi ya lita 300,000 ili wananchi wa Mlowa kule, Mkolango, Igumila, Idofi pamoja na kiwanda hiki cha dawa waweze kupata maji.
Mheshimiwa Spika, vilevile nikubaliane na ushauri wa Kamati ya Maji na Mazingira. Kamati hii imetoa mapendekezo yafuatayo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza imeomba mradi wa Bwawa la Mtera uanze ili uweze kuhudumia Dodoma, tatizo la maji Dodoma ni kubwa, kama alivyosema Mheshimiwa Lusinde pale, utakapokuwa unaleta maji Dodoma utahudumia na vijiji vilivyoko njiani. Vilevile Kamati ilishauri pia Dodoma, kwa sababu bado tatizo ni kubwa, vichimbwe visima vya kutosha ili wananchi wa Jiji la Dodoma na kwa sababu linakua kwa haraka waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile Kamati ilishauri uvunaji wa maji. Kamati imeshauri tuhakikishe kuna uvunaji wa maji. Lakini mwenzangu amezungumzia pale sasa elimu hii tuanzie kwenu, tuanzie kwenye majumba ya Serikali. Kamati imeshauri sana juu ya jambo hili. Tunampongeza Mwenyekiti wetu wa Kamati, Mheshimiwa Kiswaga na Wajumbe ambao wametoa ushauri mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, hili halihusiani na Kamati, linahusiana na watu wa Nishati, Naibu Waziri yuko hapa. Kwangu kumekuwa na tatizo kubwa la umeme wa upepo Makambako. Wananchi hawa zaidi ya miaka 14 wamechukuliwa maeneo yao, hawawezi kuendeleza kufanya jambo lolote. Serikali ilisimamisha kwa sababu walipata wawekezaji ambao watawekeza umeme wa upepo Makambako ni jambo jema, lakini mpaka sasa hakuna majibu.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri, leo nimemuunganisha ameongea na wananchi wangu Makambako. Naomba yale uliyowaambia Naibu Waziri yatekelezwe wapate majibu yale uliyowaambia ili kama imeshindikana basi waweze kuruhusiwa kuendelea na mipango yao.
Mheshimiwa Spika, tunapopongeza wote hawa ni lazima tugeuke tukuangalie Spika unayeongoza Bunge hili, tunakupongeza sana kwa kazi nzuri unayoisimamia Bunge, unavyoisimamia Serikali ukishirikana na Wabunge wenzako, tuko pamoja na wewe tutahakikisha shughuli za Bunge hili zinakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, hili namrudia Mheshimiwa Aweso. Unajua Mheshimiwa Aweso - Waziri pamoja na Naibu Waziri na timu nzima ya Wataalam, unapofanya kazi nzuri zipo changamoto, lakini katika chagamoto simamia, songa mbele, nyingine zitakuwa humu, songa mbele unapatia, kazi inakwenda vizuri. Huo ndiyo ukweli kijana. Kimbia hakikisha Majimbo yetu tunamtua Mama ndoo kichwani kama Rais alivyokukabidhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno haya, nakushukuru sana, ahsante sana. Wananchi wa Jimbo la Makambako baadhi ya maeneo maji tunapata tunaendelea vizuri, sitaki nitaje maeneo hayo, maji tulishapata. Ombi langu tu mradi mkubwa huu utakapokuwa unahitimisha uwaambie wananchi wa Makambako mradi huu utaanza lini kwenye Jimbo langu. Nakushukuru sana. (Makofi)