Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia katika hoja zilizo mbele yetu. Kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge hili Tukufu, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema, kwa kuniwezesha kuwa mwakilishi wa vijana katika Bunge hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite moja kwa moja kwenye mchango wangu. Naanza na asilimia tano ya mikopo kwa vijana kutoka kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri zetu. Naomba kuishauri Serikali kwamba hili jambo ni la kutilia mkazo maana limekuwa kama ngonjera. Kila siku watu wanaongelea kwamba kuna 10% Halmashauri zinatakiwa zitoe 5% iende kwenye vikundi vya akinamama na 5% ziende kwenye vikundi vya vijana lakini haifanyiki hivyo.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano na kasi yake iliyoanza nayo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi basi tunasema na hawa watu wa Halmashauri wajue kwamba huu ni wajibu, ni lazima watoe hizi fedha. Pia siyo kutoa tu zipangiwe utaratibu maana hii ni mikopo, lengo lake ni kwenda kuwasaidia hawa vijana waweze kufanya kazi, waweze kuinua kipato chao na vilevile hizi pesa zirudi ili vijana wengine wapate hiyo fursa. Kwa hiyo, uwekwe utaratibu mzuri wa kuzikopesha na kuzirudisha ili ziwe endelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri awaambie Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya walisimamie kwa karibu jambo hili. Huu ni mpango wa Serikali lakini tumeona kuna vyama vingine vya siasa sijui wanalewa madaraka, juzi tu wameanza kutoa hundi, ooh, mapesa ya UKAWA, mapesa ya UKAWA ya wapi? Basi na sisi wa CCM kwenye Halmashauri tunazoziongoza tuanze kusema ni hela za CCM. Kwa hiyo, naomba ifahamike kwa wananchi kwamba huu ni mpango wa Serikali na siyo mpango wa vyama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye elimu. Napenda kuipongeza Serikali hii, tangu tulipokuwa tunaomba ridhaa kwa wananchi tulisema kwamba tuko kwa ajili ya kuwasaidia wananchi. Mmethubutu na mmeweza kuleta elimu msingi bila ya malipo, kazeni buti mwende mbele. Kitu chochote chenye neema lazima kiendane na changamoto. Tumeona udahili umeongezeka baada ya kuwawezesha wananchi kwani ile Sh. 20,000/= tu ya kumpeleka mtoto wake shule ilikuwa inamshinda.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kutokana na neema hii kuna vitu vimeambatana nayo, kuna upungufu wa madarasa, Walimu, matundu ya vyoo halikadhalika na kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya hawa Walimu wetu. Nashauri katika kila Halmashauri waweke mpango mzuri wa kuweza kutatua matatizo ambayo yanaambatana na neema hii bila kusahau madawati. Pia niwakumbushe tu ameshaongea Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba kila Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi zile mbao mlizozikamata jamani ziende zikatengeneze madawati, ameongea bosi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niongelee kuhusu sekta ya afya katika upatikanaji vifaa tiba na dawa. Hii imekuwa changamoto ambayo najua Serikali inajaribu kuikabili kutwa kucha. Tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda, tukaeni chini tuna wataalam, Wizara yetu ya TAMISEMI ikishirikiana na Wizara ya Afya, Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara kwani hatuwezi sisi kama Tanzania kuwa na viwanda ambavyo vitatengeneza dawa? Nina uhakika malighafi za kutengenezea dawa zipo.
Mheshimiwa Spika, Watani zangu Wahaya mtu akiumwa kichwa hanywi panadol ana dawa zake anazitumia. Nina uhakika malighafi za kutengeneza dawa tunazo, hiyo itatuokoa kwanza tutakuwa tunazalisha dawa zetu hapa, tutapata kipato soko lipo na pia dawa zitakuwa zinapatikana kwa bei nafuu na tutawaepuka hawa matapeli ambao wanatafuta fursa ya kuleta dawa ambazo zimepitwa na muda na siyo nzuri kwa matumizi ya binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuzungumzia mradi wa uendelezaji miji ya kimkakati. Kwa Mkoa wetu wa Dodoma huu mradi umetusaidia sana kwenye maeneo ya Kisasa, Nkuhungu, Mjini Kati na Kikuyu. Kwa kweli mradi huu ulivyotekelezwa hapa mmetupa moyo, kweli mnatuheshimu kwamba hapa ni Makao Makuu ya Chama na Serikali. Kwa hiyo, naomba mradi huu uendelee kwenye sekta zingine za miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kugusia Tume ya Utumishi wa Walimu. Hiki kimekuwa ni kilio kikubwa sana kwa Walimu wetu. Tunajua mchango wao katika maendeleo ya Taifa letu kwa sababu aliyekuwa anaajiri Mwalimu ni mwingine, aliyekuwa anashughulika na kuwalipa Walimu ni mwingine, aliyekuwa anashughulika na kumpandisha cheo Mwalimu ni mwingine, aliyekuwa anashughulika na malipo ya Mwalimu ni mwingine, lakini Tume hii ya Utumishi itakuja kuwa mkombozi wa Mwalimu, hongera sana kwa Serikali yetu. Kwenye bajeti hii tumeona mmeshawawekea fungu lakini tunaomba kwa siku za karibuni muweze kukamilisha taratibu zote ili hii Tume ipewe meno ianze kazi haraka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nigusie kidogo mipango ya matumizi bora ya ardhi. Wataalam wetu katika Halmashauri wakishirikiana na Viongozi wa Vijiji, Kata, pamoja na Wilaya na Madiwani wapange mipango bora ya ardhi kwa sababu huko ndiko kwenye wananchi na wanajua changamoto zinazotokea na ambazo zinaleta ugomvi kati ya wakulima na wafugaji. Tukikazania huko hili tatizo litakuwa historia kwa sababu wananchi wanaumia jamani. Sisi tupo huku lakini wananchi wa Kongwa tunaumia sana kwa hii migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia napenda tu kugusia kwa hawa watumishi wa Halmashauri, kuna hawa Mabwana Kilimo, Mabwana Mifugo na Maafisa Biashara, majipu tusiangalie wale wanaofuja pesa tu tuwaangalie hata wale watumishi ambao hawatoi deliverance. Wananchi wetu wanajitahidi kujikwamua kwa kuendesha shughuli za kilimo na biashara lakini hawa wataalam hawawasaidii. Vijana wengi wapo hapa Dodoma wanafanya biashara ya uchuuzi wa mazao lakini hakuna Afisa Biashara hata siku moja kamfuata kumpa ushauri wa kitaalam. Vilevile Serikali ifike kipindi iwasaidie na kuwa-guarantee hawa vijana waweze kupata mikopo na wakopesheke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuongelea makusanyo ya mapato. Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshaongea, Halmashauri wasipofikisha 80% ya ukusanyaji wa mapato waliokadiriwa zitafutwa. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu hii kauli iwe ni ya kweli, kama Halmashauri haijafika hicho kiwango basi ifutwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kugusia kwa juu tu kuhusu TASAF III, TASAF inasaidia sana. Tumeona TASAF I, TASAF II na sasa hivi tupo kwenye TASAF III ni kweli inasaidia wananchi wenye kipato cha chini na kaya maskini. Tunaomba TASAF iendelee na moyo huohuo, kelele nyingi na matatizo tuliyokutana nayo huko ni ya kisiasa kwa sababu wenzetu walisema, ooh, hizi hela zinakuja kwa ajili ya kampeni, siyo kweli, zinasaidia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuongelea PCCB, tumeona utendaji kazi wao mzuri, wanashughulikia masuala ya rushwa lakini kwenye ripoti zao tumeona wakiongelea, ooh, tume-save fedha kiasi fulani lakini kuna rushwa fulani sijui kwa nini inafichwa. Rushwa hii inaumiza kweli kweli, inawaathiri watu kisaikolojia, inasababisha watu wapate magonjwa, wengine hata wakate tamaa za maisha, ni section 25, rushwa ya ngono hasa kwa mtoto wa kike.
Mheshimiwa Spika, mtoto wa kike tangu elimu ya msingi anasumbuliwa na rushwa ya ngono, kwenye elimu ya sekondari anasumbuliwa na rushwa ya ngono, akija chuo kikuu anasumbuliwa na rushwa hii ya ngono, akija kwenye kazi anasumbuliwa na rushwa ya ngono. Jamani kama kesi zipo tunaomba zielezwe ili hawa mabinti wasifiche na waseme haya matatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia mbili.