Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Afya. Nakushukuru sana. Nianze kwa kupongeza Serikali na hasa kwa jinsi ambavyo imekuwa ikileta fedha nyingi katika eneo hilo la huduma ya afya. Kwa kweli namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anaangalia kwa ukaribu afya za wananchi, lakini Mheshimiwa Ummy pamoja na Ndugu yangu, Mheshimiwa Dkt. Mollel, nawapongeza kwa kazi nzuri sana wanayoifanya pamoja na timu yao ya Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa pongezi hizo hizo, sisi Mkoa wa Tabora na hasa Hospitali yetu ya Kitete ambayo ni ya Rufaa na sisi ni miongoni mwa waliopata ile CT-Scan ambayo inagharimu karibu shilingi bilioni 1.8. Tunawashukuru sana Wizara na imeshaanza kufanya kazi na inategemewa na wilaya zote kuanzia Kaliua, Nzega, Uyui na sehemu zingine katika eneo hilo, kwa kweli tunaishukuru sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze pia Serikali kwa kuweza kuona ule udanganyifu ambao umekuwa ukifanywa na wenzetu wa NHIF na zile hatua ambazo wamechukua, Mheshimiwa Ummy na timu yako tunawashukuru, lakini wasiishie hapo. Katika hotuba ya Waziri amekiri bado kwenye zahanati kuna upungufu mkubwa wa dawa. Waangalie kwa nini MSD wanaongezewa bajeti na dawa wanapeleka, lakini kwa nini kuendelee kuwa na upungufu kwenye zahanati na hospitali zetu za mikoa na za wilaya nazo zina matatizo ya upungufu wa dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika yale maduka ambayo Mheshimiwa Ummy kipindi fulani alisema mita 500 na nini, anafuatilia na vitu kama hivyo, maduka haya ya dawa yamejaa dawa siku zote. Ukichunguza sana sio kwamba wale wa maduka ya dawa wote wanaagiza hizo dawa, wanazipata hapa hapa nchini na hatuelewi wanazipataje, wakichunguza mtajua. Nina imani hizo dawa kuna mahali zinachepuka, badala ya kwenda kwenye hospitali, wanazipata hawa wa maduka binafsi. Umekuwa ni mtindo wa kawaida mwananchi hata kidogo tu anaumwa anaambiwa akachukue dawa kwenye duka la dawa, naomba wafanye uchunguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo ambalo ulilisema hapa kuhusu gharama za mtu wa kawaida kwenda kutibiwa. Wiki iliyopita tu Mheshimiwa Ummy hata akitaka kuona ninayo hapa meseji ya Benjamin Mkapa, consultation fee kwa mtu ambaye hana uwezo kabisa, yaani ule ushauri tu 630,000 ninayo hapa. Consultation fee narudia yaani ule ushauri tu 630,000 ninayo bill yake hapa na imeandikwa ina-expire within 24 hours. Ndani ya masaa 24, huyu tena hapati tena hiyo huduma, awe amelipa hiyo 630,000. Sasa anawezaje mtu wa kawaida kupata matibabu. Kwa kweli hicho ni kitu kigumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mara kwa mara nimekuwa nikisimama kwa ajili ya Hospitali ya Kitete kuhusu upungufu wa Madaktari. Madaktari Bingwa ambao wanahitajika kwa mujibu wa ikama ni 21, lakini tuna Madaktari Bingwa watano tu. Kwa mujibu wa taarifa za Wizara ni kwamba sita sasa wamekwenda kusoma, kwa ajili ya Udaktari Bingwa lakini bado mashaka yako pale pale. Kwanza hawa sita wote watarudi Hospitali ya Mkoa wa Kitete? Kwa sababu wanaweza ku-diverge wakatoka pale wakaenda kwingine, wameshakuwa mabingwa. Madaktari Bingwa wengi wanapenda kufanya kazi katika mikoa ambayo, kwa mfano Dar es Salaam, wamefurika wako wengi ni kwa sababu ya maslahi. Sasa wana mkakati gani kama Wizara kuhakikisha hata hawa ambao wanawasomesha wanarudi kufanya kazi pale kitete ili na sisi tuanze kuona sasa kwamba tunaanza kupata Madaktari Bingwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mwenzangu mmoja jana, Mheshimiwa mmoja alikuwa ananiambia kwa nini huchangii Wizara ya Maji, mbona ni muhimu sana. Nikamwambia nitawapotezea muda wenzangu bure, mimi maji ninayo ya kutosha, kwa hiyo nitachangiaje? Sana sana kule Tabora Mjini sisi tuna maji ya Ziwa Victoria, tunaishukuru sana Serikali na tuna maji in excess. Sasa kilichobakiwa ni ile distribution na nini, ndio maana nikasema siwezi kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata kwenye huduma ya nishati sisi tuko vizuri sana na huduma zingine, kasoro tu Kitete. Ndio maana kila nikiinuka Kitete, Kitete na Tabora Mjini haiitwi Toronto hivi hivi Mheshimiwa Ummy ameshafika mara nyingi. Shida yetu sisi kwenye afya hapa. Naomba atusaidie ile Toronto sasa isiwe mtu anatoka Toronto halafu anaenda kutafuta huduma zingine za afya sehemu nyingine ni eneo tu la Mheshimiwa Ummy, akitusaidia basi atakuwa kwa kweli ametutendea haki sana. Vinginevyo Waziri anafanya kazi nzuri sana, tunamshukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kitete hospitali hiyo hiyo ya mkoa, kuna wanaojitolea katika kada mbalimbali wako 91, hao wanajitolea 91 ni watu wengi sana. Sasa tunarudi kule kule kwamba pale watakapotoa ajira wasianze kuwaleta watu ambao wametoka huko, hatukatai kuleta watu wengine, lakini wawape kipaumbele hawa ambao wanajitolea kwa sababu kazi ya uuguzi ni kazi ambayo kwa kweli ni ya kujitolea na kweli wanajitolea, 91 ni wengi sana. Kwa hiyo watakapotoa nafasi zile ambazo wataanza kuajiri naomba waweze kuwakumbuka hawa ambao wanajitolea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna sera ya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano kwamba wanapewa matibabu bure. Hiki kitu kwenye sera kipo, lakini kiuhalisia sehemu nyingi hakifanyiki. Mwaka mpya nilikwenda kutembelea Hospitali ya Kitete tena nilikuwa na timu pia nilikwenda na baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi kwa ajili ya kuona wagonjwa lakini na kuweza kutoa vifaa mbalimbali. Tulimkuta mtoto wa miaka mitano ambaye alikuwa amepataa referral, sio tu rufaa lakini pia alikuwa anatakiwa kulipia matibabu. Sasa nikawa namuuliza kwa sababu tuliongoza na Muuguzi Mkuu kwamba imekuaje hawa watoto ambao ni chini ya miaka mitano, sera inasema matibabu ni bure. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, akaniambia kuhusu ugonjwa wake. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri kwenye hili suala la watoto wa umri wa miaka mitano wawe wawazi kama kuna magonjwa ambayo hayawi covered kwenye hiyo sera ya kwamba matibabu ni bure kwa mtoto wa chini ya miaka mitano, wayaeleze wazi bayana, watu wawe wanafahamu. Vinginevyo wakienda pale akinamama na watoto wao wanajua tu kwamba mtoto wangu kwa sababu yuko chini ya miaka mitano atapewa matibabu bure, anapofika pale anapewa bill ya kulipa, inawachanganya sana wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Ummy lingine ni kuhusu suala la udhibiti wa hizo dawa. Kama dawa zinapelekwa kwa mfano hospitali fulani, inajulikana kabisa kwamba package ni hii, mnadhibiti vipi hizi dawa? Maana yake tumeona sehemu zingine baadhi ya Manesi siyo wote na baadhi ya watumishi wa hospitali ambao wamekuwa wakikamatwa na hizo dawa wakipeleka kwenye maduka ya madawa binafsi? Hizi dawa wanazitoaje? Udhibiti wa dawa ukoje? Naomba eneo hilo muweze kuliangalia kwa ajili ya kudhibiti upotevu wa dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia madirisha ya wazee na watu wenye mahitaji maalum. Bado kuna hospitali nyingi hapa nchini ambazo hazina madirisha ya wazee wenye umri mkubwa ambao wanahitaji huduma za afya lakini pia na wale wenye mahitaji maalum kwa mfano, wenzetu ambao wenye ulemavu kwamba waweze kupata huduma hizo haraka kutokana na mahitaji yao ya kimwili.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mimi kusema haya na kushukuru sana naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)