Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nampongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kuendelea kujali kabisa tasnia hii ya Afya, lakini nimpongeze Mheshimiwa Waziri Ummy pamoja na Naibu Waziri Mollel pamoja na timu nzima ya Wizara kwa kazi nzuri njema wanayoendelea kufanya. Kwa kipekee sana niwapongeze watoa huduma wote wa afya Tanzania kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nianze kwa kuunga mkono hoja asilimia 100. Mnamo Tarehe 05 Februari, 2021 nilisimama katika Bunge lako Tukufu kuzungumzia suala zima la Hospitali ya Mirembe. Nikaelezea ukongwe wake ilikuwa ni mwaka 1993 by then, nikaelezea miundo duni dhaifu na mikongwe, miundo duni ya watumishi kufanya kazi iliyo dhaifu, nikazungumzia uzito wa kazi wa eneo lile walikuwa wana-bed state kama wagonjwa 500 kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia walikuwa wanatumia shilingi milioni 280 kwa mwezi. Nikashauri miundombinu irekebishwe japo wana tatizo la akili lakini wanahitaji kuhudumiwa katika sehemu nzuri, nikashauri pia ikiwezekana iwe Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya Akili iwe Taasisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama kuipongeza Serikali sikivu ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan chini ya Waziri Ummy Mwalimu jinsi ambavyo jambo hili limetekelezwa kwa umakini mkubwa sana. Pia ninashauri suala hili pia liendelee kuzingatiwa na kufikiriwa kwa Hospitali yetu ya Kibong’oto kuwa taasisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo Tarehe 11 Februari, 2021 nilisimama humu ndani pia kuzungumzia suala zima la matibabu mbalimbali ya aina mbalimbali ikiwepo na mazoezi tiba, kwamba wataalam hawa wako wachache na pia Tanzania nzima Shahada inapatikana Chuo cha KCMC tu. Nikashauri ikiwezekana vyuo vingine kama Muhimbili, Bugando, UDOM hii taaluma ianzishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali sikivu sana ya Mama Samia Suluhu Hassan imekuja na shahada hii ya mazoezi tiba na vitendo mbalimbali vya matibabu katika Chuo cha Muhimbili. Ninaipongeza Serikali ya Mama Samia kuwa sikivu chini ya uongozi wa Waziri wetu Ummy Mwalimu na Watendaji wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Serikali imekuwa sikivu sana, leo mimi nakuja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ina Upanga na Mloganzila. Kwa siku wagonjwa wa nje tu kwenye hospitali hii ni 2,500. Muhimbili wanaona wagonjwa 2,000 kwa siku, Mloganzila 500 na nusu ya wagonjwa hao ni wa msamaha yaani hawana uwezo wa kulipia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sivyo tu, katika wagonjwa wa msamaha tuna wagonjwa ambao ni wafungwa. Hospitali ya Muhimbili peke yake inatumia shilingi milioni 72 kwa mwezi kuhudumia wafungwa, kwa maana ya kumuona Daktari, vipimo na dawa bure. Hospitali ya Muhimbili inatumia shilingi milioni 300 kwa wagonjwa wafungwa waliolazwa. Chai ya asubuhi, chakula cha mchana na jioni kwa mwezi shilingi milioni 300.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, Hospitali ya Muhimbili kwa mwezi kwa umeme na maji shilingi milioni 450 inalipa. Siyo hivyo tu, kuna magonjwa mengi yasiyoambukiza lakini niende kwa matatizo ya figo. Wanaofanya dialysis kusafisha damu kwa Muhimbili kwa siku wanafanya dialysis kwa wagonjwa 110, Mloganzila 30 na nusu ya hao ni hawana uwezo wa msamaha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Muhimbili kwa mwezi inasamehe wagonjwa kwa gharama ya shilingi bilion 1.8 mpaka shilingi bilioni mbili msamaha. Nataka kusema nini? Hii Muhimbili magari yake yakiharibika, yakipata ajali, wakienda TEMESA wanatozwa fedha nyingi sana walipe. Wakienda ku- clear mizigo yao GPSA vitendeakazi mbalimbali vitendanishi wanalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwa wafungwa, kwa nini basi Wizara ya Mambo ya Ndani kama inawezekana hiyo bajeti ya kuwatibia wafungwa iletwe Wizara ya Afya au la, watibiwe lakini bili ile ipelekwe Mambo ya Ndani walipe. Hospitali kama Muhimbili ina uwezo gani kwa gharama zote hizo? Bajeti yake haizidi shilingi milioni 400 kwa mwezi kutoka Serikalini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna shida bajeti ni ndogo, keki ni ndogo, basi pamoja na hayo yote bajeti inatengwa mwezi Julai tunaipitisha lakini inafika Muhimbili Septemba. Wagonjwa hawangoji kuugua Septemba, wagonjwa wanaumwa kila siku na tukumbuke Muhimbili ni Hospitali ambayo wagonjwa hawapelekwi ambaye ameugua siku mbili labda ana malaria au UTI, infection ya mkojo ni wagonjwa ambao wameshatibiwa huko wanakuja gharama yao ni ya juu sana. Kwa hiyo, ninasimama hapa kusema leo kwa sababu Serikali imekuwa sikivu sana. Imekuwa sikivu kwa Mirembe na mambo mengine niliyozungumza, leo Muhimbili naomba bajeti itakapopita iende haraka sana na pia iangaliwe kwa jicho la tofauti sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nina hayo machache naomba Serikali sikivu ya Mama Samia Suluhu Hassan chini ya Waziri mahiri Ummy Mwalimu waangalie Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa jicho la tofauti sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru Profesa Janabi kwa kazi kubwa anayoifanya pale Muhimbili, imebadilika sana. Nilizungumza siku moja humu ndani pawe na stock center, naona Mloganzila wametenga, ka hiyo ina maana itakuwa kama Jakaya Kikwete, itakuwa wanapata huduma stahiki, hivyo tuwawezeshe tuwatie moyo, mazingira yawe safi pia wapate vitendeakazi kwa wakati, bajeti ije kwa wakati, wagonjwa hawasubiri muda, wagonjwa wapo kila siku tena wanaumwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo naomba kuunga hoja. Ahsante sana. (Makofi)