Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Iringa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote na mimi nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mchango wake mkubwa kwenye sekta ya afya, akisaidiwa na Waziri wetu Ummy, Waziri makini kabisa na Naibu Waziri Kaka yangu Mollel. Tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nami niungane na Kamati, nawashukuru sana kwa kuja Iringa na kuona changamoto zilizopo katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa. Tunawashukuru sana kwa ajili ya Digital X-Ray Scan na ukarabati wa lile jengo la Radiology ambalo mmetumia zaidi shilingi bilioni moja na milioni mia saba na tisini na moja, tunawashukuru sana pia kwa ukarabati wa ICU shilingi milioni 150, tunawashukuru sana. Tunawashukuru pia kwa ajili ya fedha nyingi mlizozileta kwenye hospitali yetu ya Wilaya ya Manispaa ya Iringa ambayo ni zaidi ya shilingi bilioni moja na milioni milioni mia mbili. Tunawashukuru kwa ajili ya fedha ya Kituo cha Afya Mkimbizi shilingi milioni 500. Tunawashukuru kwa ajili ya fedha katika Kituo cha Afya Ipogoro shilingi milioni 357. Tunawashukuru kwa ajili ya fedha mlizoleta kwenye zahanati zetu, Zahanati ya Mkwawa shilingi milioni 50, Zahanati ya Isakalilo pale shilingi milioni 150, Zahanati ya Nduli shilingi milioni 50, Zahanati ya Ugele shilingi milioni 50. Nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya changamoto zilizotokea tunaomba muendelee kutuongezea watumishi katika Hospitali yetu ya Referral ya Mkoa wa Iringa na pamoja na kwamba mmeshatupatia watumishi wengine karibu 26 lakini bado tuna upungufu. Mmetupatia watumishi 46 kwenye Hospitali yetu ya Wilaya bado tuna upungufu na katika vituo vyetu vya afya kwa mfano Mkimbizi mmetupatia watumishi Saba. Tunawashukuru sana na kwenye zahanati watatu, watatu tunawashukuru tunaomba muongeze.
Mheshimiwa Naibu Spika, Manispaa ya Iringa kwa geographical location yake inahudumia siyo Manispaa ya Iringa tu. Tunahudumia Jimbo la Kalenga, tunahudumia Isimani, tunahudumia Kilolo. Kwa sababu watu hawawezi kupita pale Mjini wakaenda kutibiwa Kilolo wakati pale kwenyewe kuna Hospitali. Hawawezi kutoka Kalenga wakapita mjini wakaenda kutibiwa Igodivaa wakati pale kuna hospitali. Hawawezi kutoka Ifunda wakaja kutibiwa huko Igodivaa. Kwa hiyo location yetu tunaomba sana mtusaidie. Mtuongezee kituo cha afya Kitilu, mtuongezee kituo cha afya Igumbilo kwa sababu huko ndiko kunakopokea watu kutoka kwenye Majimbo mengine na sisi tupo tayari kwa sababu kwa mfano Igumbilo pekeyake zahanati inahudumia zaidi ya watu 600. Sasa unaweza kuona mzigo unavyokuwa mkubwa. Kwa hiyo tunaomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufinyu wa eneo katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa ni changamoto ambayo kamati imesema. Mimi niwaombe rejeeni mapendekezo yetu na RCC ya Iringa, kwamba Hospitali ya Wilaya ile ina eneo kubwa sana na wala pale siyo mbali hazifiki hata kilometa Sita. Mnaweza mkaamua structure zenu nyingine mkaziweka pale na mkatenga kama mkoa ili tuendelee kupata huduma za referral kwenye hospitali yetu ya Mkoa kuliko kufikiria kuihamisha pale Wizara ya Mambo ya Ndani ianweza ikawa shida.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunaomba wataalamu wa mifupa. Mnaona geographical location ya Iringa, ipo kati kati pale, barabara kubwa zote zinapita pale, ajali ni nyingi. Kwa hiyo, wote wanategemea kuja pale kwa ukaribu wake. Tunaomba sana wataalam wa mifupa, masikio tupate ili watu wakipata ajali kuliko kuanza kuwakimbiza Benjamin kuwapeleka Muhimbili, na distance ni ndefu, basi pale tupate wataalam wa mifupa ili waweze kutusaidia lakini tunawashukuru kwa ajili ya wataalam mliotuletewa wanne kwa ajili ya viungo bandia kwa ajili ya wagonjwa wa ajali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niwashukuru sana pia kwa kuniteua kuwa Balozi wa Afya ya Akili Tanzania. Nakushukuru sana Waziri wa Afya na ninaona jambo hili linaongelewa kwa mapana yake. Sasa katika huo ubalozi naomba basi wale Isanga wanatibu tibasheria, kwa ajili ya wale wenzetu wanaoonekana kule kwenye sheria walipelekwa kimakosa kumbe ni matatizo ya afya ya akili wanapelekwa pale kusaidiwa kutoka Magereza. Wapeni basi hiyo shilingi bilioni moja na milioni 600 walizoomba changamoto ya kibajeti ili waweze kuwahudumia wenzetu wenye matatizo ya afya ya akili kutoka kwenye vyombo vya sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru pia kwa ajili ya Mirembe kuifanya kuwa Taasisi ya Afya ya Akili Nchini. Ilingane lingane basi sasa na taasisi ya afya. Tumesherehekea mwaka jana miaka 100 pale lakini bado hapaeleweki. Ilingane na taasisi ya afya ya akili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri kama Balozi nisipoongelea masuala ya afya ya akili nitakuwa sijaitendea haki nafsi yangu mimi mwenyewe. Masuala ya matatizo ya afya ya akili ni makubwa. Ninakushukuru umeweka katika vipaumbele vyako Namba Sita kuimarisha huduma za afya ya akili, huduma za utangamano na tiba shufaa. Tunakushukuru sana kwamba umeiingiza lakini ipe uzito unaowezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ummy, matatizo ya afya ya akili yanakuletea cost kubwa sana kwenye vifaatiba na matibabu. Kama WHO wanasema afya ya akili ni kutojitambua, ni kushindwa kupambana na changamoto, ni kushindwa kutoa msaada kwenye jamii, ni kushindwa kufanya kazi kuzalisha kwa faida, hiyo ilitakiwa ipewe kipaumbele cha kwanza. Tukiwapa watu wetu wakawa na uelewa mzuri kwenye akili zao. Kwanza mimi nataka ile pre copying kwanza. Kabla hujafikia kutupa dawa za afya ya akili, tujifunze kwanza masuala ya mambo yanayosababisha tukafikia kule kwenye kutumia dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, na hiii tuifanyaje? Tufanye kampeni maalum. Marekani tangu miaka ya 50 wana mwezi wa kampeni maalum kwa ajili ya masuala ya afya ya akili na wao wanaifanya Mei. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasi tuchague mwezi maalum ambao tutaongelea masuala ya afya ya akili, tutawaambia watu wafanye meditation, tutawaambia watu mwezi huu nendeni mkafanyiwe massage, tutawaambia watu mwezi huu walie wasiolia, tutawaambia watu mwezi huu ni wa kusema matatizo yenu ili watu waseme, watu walie, watu wapate nafasi ya kwenda kufanya massage, watu wapate nafasi ya kwenda kutembelea misitu, waende national parks, waka-relax akili zao. Wakirudi wawe salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri haya matatizo ya afya ya akili ndiyo yanakufanya wewe unakuwa na wogonjwa wengi wasio na magonjwa ya kuambukiza hospitali. Unatumia fedha nyingi, kumbe watu wanatakiwa kufanyiwa tu mazoezi, watu wakishachangamana humu kwenye ndoa wakashindana wakidundana ngumi wanakuja kushonwa kwako wewe. Wanapiga x-ray mzigo unaongezeka kwako. Watu wakishindwa kufanya maamuzi sahihi wanawasababishia wengine presha. Ndiyo unapata taabu kubwa wengine veins zina-fail ndiyo tunapata taabu kubwa ya kununua ma-CT Scan kumbe mambo mengine yangetibika. Hapa umetuambia umetibu watu milioni 35.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naongea na daktari mmoja akasema katika watu 10 wanaoenda hospitali, wagonjwa ni Watatu, Saba wote hawa wameenda kwa sababu tu ya afya ya akili. Mtu tu mke wake kaamua kumletea tatizo kwenye nyumba, mume amefyatuka presha iko juu, anahitaji CT scan anahitaji vitu kama hivyo. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunatakiwa sisi tuone kwamba kampeni ya afya ya akili ndiyo kitu cha mwanzo kuliko vitu vingine. Ukija mimi ukaniahidi hapa leo kama Jesca Mbunge, ukaniahidi kwamba chinga wa Iringa tunakwenda kuwaletea shilingi milioni 700 watengenezewe structure zao, halafu usipoleta zile fedha mimi umenifanya niwe chizi, na wale machinga wangu wote wamekuwa machizi, hivi hatueleweki afya zetu zimeyumba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii kampeni ianze kwenye Wizara za wenzio wasiwe motor behind kusababisha afya za akili waambie mnanivurugia watu afya zao. Ahadi ziwe zinatekelezeka, mipango itekelezeke ili watu wawe na afya nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, afya ya akili inakwenda kwenye masuala ya imani. Mtu akili ikishashindwa kufika mahali ikaamua jinsi ya kutatua tatizo lake anajipeleka sasa kwenye imani potofu, ndiyo kule wanafikia sasa mtu anaambiwa ukienda ukambaka mzee, ukambaka mtoto, ukambaka dada yako, ukambaka mama yako unapata utajiri. Sasa mwisho wa siku wakibakwa wanakuja kwako Waziri wangu Ummy wanahitaji dawa, wanahitaji huduma za afya, tunaongeza mzigo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo suala hili liweke mwanzo. Kampeni ifanyike kubwa ili watu wetu waelewe kwanza. Katika vitabu vya Mwenyezi Mungu vinasema watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Kitu cha kwanza kinachomuangamiza binadamu ni kiuchumi, kisiasa, kinachomuangamiza kwenye jamii ni kukosa maarifa. Kama mtu hana understanding ya kwamba kulia ni deal, kulia kutaniponya, kwenda National Parks kutembea Selous kutaniponya, anafikiri ni anasa peke yake inatupa shida, mtu aelewe kwamba kwenda National Park siyo anasa unakwenda kufanya healing. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenda na watoto wako kuogelea wakati mwingine kutembea na watoto wako porini wakasikia harufu tofuti tofauti, sauti za ndege badala ya sauti za magari peke yake, ile nayo ni healing ya kutosha. Wewe kuendelea kusema mimi leo namtoa outing mke wako na ukasema leo simtoi mchepuko outing, namtoa mke wangu outing umemfanyia healing akirudi hatakusababishia matatizo ya afya ya akili, lakini watu wanadhani ni anasa.!
Sasa hivi Mabalozi tuko well empowered, tunaweza kufundisha watu Mheshimiwa Ummy hapa sasa bajeti ya Balozi iwepo maana yake sasa hata bajeti ya Balozi haipo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mambo haya Mheshimiwa Ummy nimekuwa nayafanya mwenyewe kivyangu, hayawezi kwenda kwenye upana huo. Tengeneza timu sisi twende tukawaambie watu. Tukaongee na vijana wetu, tuwaeleze. Hii tabia ya mtu kujiona eti mimi mwanamke lakini I am feeling, I am a man yaani yeye ni mwanamke anajiona ni mwanaume, no! hatuangalii jinsia kwa kujihisi, tunaangalia kwa structure uliyonayo kwa physical appearance yako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo tunaongea hapa ushoga, tunaongea sijui usagaji kumbe watu wangekuwa vizuri tu, hana sababu ya kujiona mwanamke mwanaume, mwanaume mwanamke kwa sababu tayari akili yake inge- sense tu kwa kiungo nilichonacho mimi ni mwanamme sina sababu ya kujiona mwanamke. Kwa kiungo nilichonacho mimi ni mwanamke, sina sababu ya kujifanya mwanaume.
SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Balozi.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)