Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Mohamed Lujuo Monni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi walau nichangie kidogo katika Wizara hii muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametujalia afya sote na tuko hapa. Nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo anaendelea kulihudumia Taifa hili kwa namna ambavyo anatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa hakika anafanya kazi kubwa sana. Mimi nafahamu kila Mbunge hapa kwa wakati moja au mwingine ameshawahi kwenda kuomba jambo. Mnafahamu namna ambavyo yuko rahisi na anafikika. Pia nimshukuru Naibu Waziri ni rafiki mzuri wa ndugu zangu wote mlioko hapa na mimi ninaamini wale ambao tunatoka kwenye Majimbo yenye shida nyingi, Majimbo ya Vijijini ambao watu hawana uwezo wa kutibiwa, mara moja au mara mbili tumeenda kwake na ametusaidia. Nichukue nafasi hii pia kumshukuru Katibu Mkuu na Watendaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nimshukuru Mtendaji Mkuu wa MSD. Tumekuwa na changamoto ya muda mrefu sana huko nyuma. Ninyi ni mashahidi huko vijijini dawa zilikuwa hazifiki lakini kwa sasa kuna flow nzuri ya dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri utakuwa ni shahidi Bunge lililopita moja ya ajenda kubwa iliyokuwa hapa ni MSD, ndiyo maana kila anayechangia leo, maneno yamekuwa machache kwa sababu dawa zinafika kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo la muhimu hapa la kuongea, kwamba kazi ya MSD imebaki kupelekewa fedha, kwenda kununua dawa na wale waliopeleka fedha kwenda kuchukua. Sasa hili jambo haliko sawa. Hatuna option nyingine, ni lazima MSD wapewe fedha. Kama tuna dhamira ya dhati ya kuhakikisha afya za Watanzania zinakuwa imara na kupunguza gharama za Serikali za kununua dawa, ni lazima fedha iliyoombwa na MSD wapewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na changamoto, wakati mwingine unaweza kujiuliza maswali, kwamba mbona MSD kila mwaka wanapewa fedha, lakini hawana capital ya kuagiza dawa wenyewe? Nimejaribu kufuatilia hili jambo nikaona ni kweli kwamba Wabunge wengi wanaweza wakafikiria hilo kwamba wale MSD pengine kuna fedha ambayo wanabaki nayo. Ukweli ni kwamba fedha wanayopelekewa ndiyo wanayotumia kwenda kununua dawa, na kafaida kale kadogo pengine ndiyo anakatumia kuendesha ofisi. Sasa ni lazima sasa tuangalie namna bora ya kutoka hapo walipo. Namna bora ni kuhakikisha Wizara ya Fedha imewapa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sijui kama tumewahi kufikiria, ni lazima tuamini kwamba katika kitu cha thamani kubwa hapa duniani ni uhai. Ni ukweli kwamba afya ndiyo uhai. Hapa nyuma kumetokea ugonjwa wa Uviko. Ilikuwa ni changamoto kubwa kwa sababu dawa zote tunaagiza huko nje, na viwanda vyetu vilikuwa vimefungwa. Kwa nini hilo halionekani? Maana yake kuna siku tutakosa dawa moja kwa moja, kwa sababu tumeshindwa ku-empower MSD. Bawaomba sana Wizara ya Fedha, waangalie kwa upana mkubwa changamoto hii kwa namna ambavyo ilivyo kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri tuna mtendaji mzuri wa MSD sasa hivi, tunaweza tukamwamini, tukampa fedha, tukaangalia baada ya miaka mitatu, nini kinaendelea? Ila tukiendelea kuwapa fedha ili waagize dawa, wataagiza dawa, watapeleka huko kwenye hospitali, nao hawana kitu, na hawana Development Plan ya aina yoyote, maana yake maisha yetu yatakuwa ni hayo. Nawaomba Wizara ya Fedha katika hilo la msingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hangamoto kubwa sana na ya kupindukia ya watumishi wa afya. Jimboni kwangu mwaka 2022 tumefungua zahanati nane kwa pamoja, lakini hizo zahanati hazina wahudumu. Mheshimiwa Rais ametoa fedha nyingi zinakuja vijijini, nikutolee mfano kwenye hospitali yetu ya wilaya, mmetuletea fedha, tumefunga X-Ray mpya, Ultra-Sound mpya, mashine ya macho mpya, ya meno mpya, lakini hakuna mtumishi hata mmoja. Maana yake zinachakaa. Mmetuletea mpya, zinachakaa, hakuna chochote kinachoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana, mwenzangu mmoja alisema tunavyoendelea kuweka hii miundombinu ya afya ni lazima tufikirie pia ni namna gani tutapata watumishi wa kwenda kusaidia kwenye vifaa hivi. Haina tija yoyote. Watu wangu pale Chemba wakiona kuna X-Ray mpya kweli, kuna Ultra-Sound, lakini hakuna chochote kinachoendelea. Mtu akitaka kufanyiwa Ultra-Sound, ni lazima aje Dodoma General. Namwomba Mheshimiwa Waziri sana katika hilo hebu tusaidie. Naamini sasa kwenye watumishi hawa, ajira mpya zilizotangazwa mtatufikiria zaidi katika Wilaya yetu ya Chemba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kada zote za afya, sisi tuna asilimia ishirini na kitu ya watumishi. Kwa hiyo, unaweza ukaona changamoto kwa ukubwa wake ilivyo kubwa. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuwaombeni sana, sana, sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la muhimu, miradi ya afya ambayo inatekelezwa, hii miradi ya World Bank,na Global Funds, kuna changamoto kidogo ipo. Kwa mfano, kuna jengo la Kata ya Msaada limeanza kujengwa mwaka 2007. Mwaka 2007 hapa wengine walikuwa bado wadogo, mpaka leo halijakamilika na limeishia njiani na watu wanaliona. Kila Mbunge akija, anaambiwa kama unataka tukupe kura, hebu malizia hilo jengo. Sasa kwa nini tunakuwa na mipango ambayo haikamiliki?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuna Kituo cha Afya Makorongo. Sasa hivi kinatumika na kilifunguliwa na Mheshimiwa Rais wakati huo Jakaya Mrisho Kikwete, hakina theater, hakina maabara, hakina mochwari. Kwa nini kiwe nusu? Nawaombeni sana, nimeandika barua mara kadhaa. Nilimwomba Mkurugenzi akaandika, tukaambiwa tulete BOQ lakini mpaka leo bado hakijakamilika, wala hakuna fedha yoyote ambayo imekuja kwa ajili ya umaliziaji wa majengo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niishukuru tena Wizara, niwashukuru watendaji, na Waheshimiwa Mawaziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga hoja mkono ahsante sana. (Makofi)