Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii jioni ya leo kuchangia katika Bunge hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, MSD wanaomba wapatiwe mtaji wa bilioni 593, bilioni 592.9, hiyo ndiyo tunasema bilioni 593. Mimi sina shida, hata mimi naunga mkono wapatiwe ili waweze kutekeleza majukumu yao, maana yake watakuwa wamejipima, wame-discuss wakaona wakipatiwa hii fedha wataweza kutekeleza majukumu yao vizuri. Shida yangu kubwa, wakati ule wa taarifa za Kamati tuliona ripoti ya CAG inaeleza dawa nyingi zinafika vituoni zikikaribia kuisha muda wake (ku-expire).

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakati MSD wanaomba kuongezewa fedha na Bunge hili na Kamati imeongea maana yake tunaunga mkono, hata mimi naunga mkono, lakini na wao MSD wanapaswa wajitathmini, wanapaswa wafanye kazi yao kwa weledi. Wanapaswa wawe waaminifu, wapeleke dawa huko zinakohitajika katika Mikoa yetu na Halmashauri zetu wakati zina muda mrefu kabla ya kufikia muda wa ukomo wa matumizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanaumwa katika hospitali, wanaumwa majumbani wanashindwa kwenda hospitali lakini unaambiwa dawa zinateketezwa. Kwa hali ya kawaida hilo jambo halifurahishi. Kwa hiyo, wakati Bunge linataka kusema MSD ipewe fedha na watumishi wa MSD nao wajione wana jukumu na wana dhamana waliyoibeba kwa nchi yetu hii ya Tanzania, hilo jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kule kwetu Mtwara tunasumbuliwa sana na ugonjwa wa Malaria, hilo linajulikana. Miongoni mwa Mikoa ambayo ni hatarishi kwa ugonjwa wa Malaria, kuna mmbu wengi sana ni pamoja na Mikoa ya Mtwara na Lindi. Sasa naomba niiulize Serikali, kama Zanzibar imeweza kudhibiti mmbu na kudhibiti Malaria, huku Tanzania Bara ni kitu gani kinashindikana? Katika hali ya kawaida tunasema kinga ni bora kuliko tiba, sasa hivi tungekuwa tujadili zaidi kukinga kuliko tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunacho kiwanda pale kila siku nikichangia Wizara hii ya Afya naongelea kile kiwanda chetu cha Kibaha. Kila siku ukikisikia kina-underperform, kwa nini kina-underperform wakati matatizo bado ni makubwa? Sisi watu wa Mtwara giza likianza kuingia mmbu wanang’ata utasema wana meno. Sasa Serikali ione namna. Hapo Zanzibar ukienda kuna unafuu wa hali ya juu na Mheshimiwa Waziri unajua, kwa nini huku Tanzania Bara na hii yote ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Zanzibar wamefanya miujiza gani iwezekane na huku Tanzania bara kinashindikana kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naiomba na kuiomba Serikali iangalie jambo hili, maisha ya watu yanateketea sana kwa ugonjwa huu wa Malaria. fedha za Serikali, za walipakodi, zinatumika sana kwa sababu ya ugonjwa huu wa Malaria. Tujitahidi sana kuweka kinga kuliko kusubiri tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine la mfumo. Bado hii mifumo katika hospitali zetu inasumbua. Unajua ukimwona mtu ametoka nyumbani amefika hospitali anaumwa na Mtanzania ukimwona amekwenda hospitali walio wengi maana yake ameshindwa, yaani anaumwa. Anachotamani yeye akifika hospitali atibiwe arudi nyumbaji. Unafika hospitali unaambiwa cheti hawawezi kukata kwa sababu mfumo haufanyi kazi, sijui network iko chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafikiri hili katika Hospitali yetu ya Mkoa Ligula pale Mtwara linatokea, ingawa ndiyo hivyo mkiwasiliana na wahusika wanasema tunaandika pembeni tutakuja kuingiza na vitu kama hivyo. Kwa hiyo mimi nafikiri kuandaliwe utaratibu, mgojwa akifika atibiwe hayo mengine ya mfumo mnayajua ninyi. Mimi nikiumwa nahitaji nitibiwe, sihitaji kuambiwa habari za mfumo kutokufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali yetu ya Kanda ya Kusini, wananchi wa Kanda ya Kusini, ukiwemo Mkoa wa Mtwara, tunashukuru hospitali ipo, imefunguliwa. Lakini hospitali ile bado inahitaji iendelee kutengewa fedha na fedha zitolewe. Kuna ujenzi ule wa awamu ya pili, bilioni mbili bado hazijapelekwa, tunaomba zipelekwe. Pia hakuna ambulance, Hospitali ya Kanda ya Kusini haina ambulance, hakuna gari la Mkurugenzi, naye yupo tu, yaani ndiyo ile tunasema anaazima azima.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia karibia asilimia 80 ya watumishi wanaohitajika katika Hospitali ile ya Kanda ya Kusini hawapo. Kwa hiyo, tunaomba Serikali ione umuhimu, sisi tunafurahi na tunapenda wananchi wa Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara tukitaka kwenda Dar basi tuende kwa mambo mengine siyo kwenda kutibiwa, tukitaka kwenda kutibiwa tuende tukatibiwe katika Hospitali yetu ya Kanda ya Kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali ambayo sasa hivi ipo bado kuna changamoto ambapo tunaomba Mheshimiwa Waziri, tunaiomba Serikali iangalie kwa jicho la upekee hospitali ile ya Kanda ya Kusini ili sisi tusilazimike. Unapokwenda Dar es Salaam wakati unaumwa bado unafikiria huduma zingine za malazi na chakula ambazo ni ghali ukiwa nje ya mji wako. Kwa hiyo, tunaomba Serikali ichukulie jambo hilo kwa uzito wake na kwa umuhimu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la mwisho jioni ya leo nataka niiombe Serikali ukikaa ukisoma kwenye mitandao mingi, unakuta watu wanapostiwa wanaumwa magonjwa makubwa makubwa yakiwa katika stages za mwisho sana. Mtu utaona anaumwa cancer, anaumwa ugonjwa gani, unajiuliza huyu mtu imekuaje alikaa nyumbani mpaka amefikia stage hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali – sielewi labda ni elimu kwamba Watanzania hatuna ule uelewa zaidi wa kwenda hospitali, sielewi. Naiomba Serikali itilie mkazo, kwa sababu kila sehemu kuna watumishi wa Serikali, waone wanawashauri vipi wananchi. Mwananchi yeyote anapopata tatizo la kiafya sehemu ya kwanza iwe hospitali, tusikae tukasubiri hali imekuwa mbaya ndiyo unakwenda hospitali, hata kutibiwa inakuwa ni vigumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nashukuru sana, MSD wawe makini wananchi wanaumwa na wanahitaji dawa, hatutaki kuona dawa zinachomwa kwamba zime-expire. Nakushukuru sana. (Makofi)