Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkenge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ambayo inagusa Maisha yetu. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Dct. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuiimarisha Wizara hii. Pia tunaona kazi nzuri ambayo inafanyika katika ujenzi wa hospitali za rufaa za mikoa ambazo ziko chini ya Wizara, na kazi kwa kweli imeboreshwa baada ya kuwa chini ya Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, dada yangu Mheshimiwa Ummy, kazi unaifanya nzuri pamoja na Naibu Waziri wako Mheshimiwa Dkt. Mollel, mnajitahidi sana, nafikiri pongezi nyingi mmezipata kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge. Hatupongezi kwa ajili ya kufurahisha; kazi ukiwa unafanya tunakuambia na kama mambo hayaendi vizuri pia tuna kushauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua viongozi hawa hawafanikishi bila kuwa na wasaidizi wao wa chini; Katibu Mkuu Kaka yetu Seif, Naibu Katibu Mkuu Grace Maghembe (Dkt.). Pia Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu na madaktari wote, naona jopo limekamilika. Nikiangalia Wakurugenzi wako hapa, naona akina Dkt. Subi, akina Dkt. Chandika, wapo wote, Prof. Lugajo, wote wapo. Kwa hiyo unayo timu nzuri ambayo inaweza kuleta mageuzi makubwa katika Wizara yako, na wengine ambao sikuwataja lakini nawaona hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitajikita katika maeneo kama manne, na eneo la kwanza nataka kushauri kwenye suala la NHIF. Tunajua Serikali ilichukua jukumu la kuboresha au kuona ni jinsi gani ya kusimamaia Mfuko wa NHIF, na ikaondoa form 2C. Form 2C ni fomu ambayo mgonjwa akikosa dawa katika kituo alichoenda kuandikiwa basi anapata fursa ya kuipata sehemu nyingine kwa utaratibu ambao Serikali iliuweka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo jema kwa Serikali, lakini mimi wasiwasi wangu, na sintofahamu yangu ni kuangalia maandalizi gani mazuri yaliyofanyika ili kitu hiki kisiathiri mfumo wa matibabu; na madaktari wapo hapa, niliowataja na ambao sikuwataja, wanajua basic practice ya medicine.
Mheshimiwa Naibu Spika, anapoenda mgonjwa kwa daktari akaandikiwa dawa inatakiwa apate dawa ile ile. Unless daktari abadilishe ile dawa, lakini akilenga zaidi katika matumizi ya dawa hii kumsaidia mgonjwa, asilenge katika upatikanaji wa dawa iliyoko stoo ili apewe mgonjwa; suala ambalo leo ndio linalofanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kwa kweli hilo suala linaniuma kama mtaalamu wa dawa ilhali nikijua wanaosimamia sera hii na upande huu ni madaktari ambao ni wabobezi, na ni wazuri, wanajua umuhimu wa mgonjwa kuandikiwa dawa fulani akaipata dawa hiyo ambayo daktari mwenyewe amemuandikia inamsaidia kiasi gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuishii kwenye form 2C, kupata ukakosa dawa stahiki, tunaenda na wale ambao ni watoa huduma wa kusaidia pale Serikali inapokuwa haijafikisha mkono wake. Pharmacy za watu binafsi ambazo zinatoa huduma hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tumeenda mbali, ikaonekana kwamba zile pharmacy ambazo ziko nje ya hospitali, kwamba zinauza dawa za wizi hazitakiwi kuwepo. Mheshimiwa Waziri mimi nakupenda sana, najua unachapa kazi, lakini mpaka leo hizo pharmacy hazina vibali; tulizinyima vibali. Sasa sijajua intention ni nini; kwamba tunataka zi-phase out au tunataka kuzifuta. Lakini ni kosa gani limefanywa na hizo pharmacy?
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nirejee tena, madaktari hawa tunaowaona sura, mimi nimesomea Muhimbili na hawa wote ni colleagues, tunajua jinsi ambavyo wamefaidi zile pharmacy zilizoko pale nje kupata dawa nje na ile ambayo inatakiwa labada kutoka nchi kama vile Ujerumani na Egypt. Yote hii inasaidia Serikali, pale ambapo inakuwa haijafikisha huduma Serikali yetu inaendelea kuonekana kwamba inafanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, niseme katika eneo hilo…
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
TAARIFA
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze mwenzangu, anachangia vizuri sana na input yake ni muhimu sana na ina hoja. Lakini natataka tu nimpe taarifa kwamba, kwenye hilo eneo la form 2C, kwenye fedha ambazo zimeokolewa na Bima ya Afya, bilioni 115, asilimia 80 zinatokana na form 2C. kuna watumishi ambao wamekamatwa wako mahakamani sasa hivi, na kuna maduka ya dawa ambayo sasa hivi yamefungiwa, yamenyang’anywa bima na wengine wako mahakamani yanatokana na form 2C. Kwa hiyo form 2C ndicho kichochoro chenyewe. Jana tu, wiki mbili zilizopita tulikuwa pale kutokana na form 2C, tuliokoa milioni 600, ahsante sana.
NAIBU SPIKA: Ahsante sana, Mheshimiwa.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naipokea taarifa, maana hapa tunajenga, wala hatubomoi. Serikali pale ambapo inaweza kusimamia vizuri rasilimali za Serikali isimamie vizuri. Mimi nilitaka kushauri, kama kweli inaonekana kuna pharmacy ambayo imeshiriki kuiba dawa za Serikali, penal code zipo. Ukienda section 302 unaweza kumpeleka na ukamfunga zaidi ya miaka saba. Ambacho hatujakiona, ambacho Serikali imetuonesha ni kwamba kuna mtua ambaye ameshapelekwa mahakamani amefungwa kwa sababu amekutwa na dawa za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa haya kama hayaonekani hatuwezi kusema kwamba hayafanyiki. Lakini kama Serikali inachukua hatua sisi tunawapongeza sana, hakuna ambaye ana kipingamizi na hatua mnazozichukua.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi niachosema ni kuhusu maandalizi mazuri ya mazingira. Leo mgonjwa akienda, watu wanatibiwa hapa, kwenye hospitali yetu nzuri kwa Dkt. Chandika, lakini ukienda pale dawa ukakosa unaishia kuambiwa bwana tafuta utaratibu unaowezekana. Sasa, ni suala ambalo mimi nafikiri ushauri muuchukue Dkt. Mollel yaani usiendeleze taarifa ili tuweze kuboresha kuona sasa ni namna gani ambayo tunaweza kuboresha eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni suala la bei, nafikiri Mheshimiwa Waziri wewe ni shahidi, nimekuletea vipimo ambavyo kipimo hicho kwa cash ni shilingi laki mbili lakini ukienda kwa Bima ni milioni moja. Vipo kwa evidence na kwa kuonesha wazi. Tukasema tuboreshe katika maeneo hayo. Fedha zinapotea kwa Bima ya Afya lakini na sisi wenyewe tumeweka bei ambazo si za soko. Kwa hiyo haya yote yakiboreshwa mimi nafikiri tunaweza kukaa vizuri na Serikali yetu ikaendelea kutoa huduma kwa wananchi kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili niongee suala la MSD. Mimi nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, alichukua hatua kuiboresha chini ya Wizara ambayo ni Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri wanaendelea kusimamia. Lakini kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri amesema Menejimenti bado; Menejimenti ndiyo inasaidia; hata kama Mtendaji Mkuu yupo, hata kama bodi ipo, iweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba nishauri, Mheshimiwa Waziri pale ambapo tumechelewa kidogo basi kimbiza hiyo Menejimenti ikamilike. Lakini na Wakurugenzi wako wote wa MSD wote wanakaimu. Sasa unapokaimu maana yake maamuzi ya kufanya pale huwezi kuyafanya kwa kujiamini. Hata kama mtu anataka kumshauri Mkurugenzi Mkuu wa MSD atakuwa anasita kwa sababu hajui kwamba kiti alichokikalia ni cha kwake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia pamoja na suala ambalo limejadiliwa na Waheshimiwa Wabunge wengi. Kwamba waongezewe MSD mtaji. Tunachotaka kuona ni ni kwamba dawa zinafika kwenye zahanati na vituo vya afya pamoja na hospitali, ili sasa MSD ionekane kwamba inafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine niishauri Wizara kuhusiana na masuala ya majukumu makubwa ya Wizara, ambayo ni Kinga na Tiba. Suala la Wizara pamoja na kututibu lakini lazima kinga iwe ni bora zaidi. Katika eneo hilo kuna suala ambalo Mheshimiwa Waziri analijua. Tuna suala la kemikali ambazo zinatumika katika jamii kwa mfumo wa vipodozi, kuna zinazotumika kwa mfumo wa chakula; lakini zimeachwa zinaendelea kuzagaa katika soko letu, na mwisho wa siku anayeathirika ni Mtanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi juzi nilikuwa naangalia taarifa ya Habari ya RPC Mwanza, watu saba wamekula chakula ugali na furu, wawili wakafariki saba wako hoi; lakini dalili anasema wametapika. Hizo zote ni dalili ambazo kwa daktari anajua kwa hiyo ni mycotoxin, ni sumu kuvu. Sasa, sumu kuvu unapoiacha ikadhibitiwa na watu ambao hawana taaluma ya udaktari sioni kama tunaisaidia nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi bado nimuombe Mheshimiwa Waziri mimi, nay eye ni mwanzilishi wa hili suala; bidhaa hizo mbili za chakula na vipodozi sisemi ziende wapi wala wapi lakini zirudi katika Wizara yake inaweza ikawa kinga kwa wananchi ili waweze kuzi-manage vizuri. Lakini anapoacha bidhaa huria vipodozi, dada zangu mtanisamehe, kuna vitu vingine ambavyo tunatumia kama wataalamu lazima tuseme ukweli, kwamba kesho na kesho kutwa tunapata Kansa ya Ngozi, tunaanza kuwa na magonjwa ambayo ni hormonal imbalance kwa sababu ya kutumia vitu ambavyo havitakiwi. Sasa ni nani ambaye anaweza kusimamia hili suala likaenda vizuri ni Waziri wa Afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niombe Wizara ijitahidi katika eneo hilo, na najua Mheshimiwa Waziri analifahamu basi aendelee kushauri kule kukubwa ili aweze kusikilizwa mpaka hili liweze kufanyika. Baada ya kusema hayo kuna la mwisho, Mheshimiwa Waziri umekuja Mkoa wa Kagera umetutembelea umeona jinsi tulivyo changanyikana na Uganda na…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Kyombo.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, niombe basi na sisi Mkoa wa Kagera tuweze kupata hospitali ya rufaa ya mkoa yenye hadhi ya mkoa ule ili tunapokuwa jirani na Uganda, Rundi na Rwanda tuweze kuwa na…
NAIBU SPIKA: Ahsante, muda wako umekwisha.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)