Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Wizara ya Afya. Nampongeza Waziri, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu kwa namna alivyoweza kutupatia fedha za kutosha. Zahanati tumeweza kupata fedha za kutosha, hatuna shida huko, vituo vya afya tumepata fedha za kutosha, lakini kubwa zaidi namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa namna nilivyoweza kumwomba ile hospitali yetu ya mkoa ili iwe hospitali ya manispaa na hivi sasa tayari ile hospitali ni ya kwetu kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa Jimbo langu la Musoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru sana kwa huduma ya hospitali yetu ya rufaa sasa, ile ya Kwangwa kwa huduma inazozitoa. Kwa hiyo leo maana yake ni kwamba tunaanzia kule kwenye kata, tunaenda wilayani na hatimaye kwa yale magonjwa ambayo yanashindikana basi tunaweza kwenda kwenye hospitali yetu ya rufaa, tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kusema kweli leo sina mambo mengi, ya kwangu namwomba Mheshimiwa Waziri machache tu tena yote ni mepesi ambayo naamini kwamba hata utekelezaji wake wala hautamsumbua sana. Moja, tunashukuru kwamba wameweza kutuletea CT scan pale kwenye Hospitali yetu ya Kwangwa, lakini kwa bahati mbaya sana sasa yapata miezi isiyopungua mitatu haijafungwa. Kwa hiyo sasa maana yake ni kwamba watu wetu wanapata tabu, lakini tayari Serikali ilishaweka fedha mashine iko pale. Kwa hiyo, tunaomba kwa haraka kabisa hiyo huduma iweze kupatikana kama huduma zingine zinavyopatikana leo pale, watu wetu walikuwa wa kusafishwa figo walikuwa wanasafiri leo mambo yote yanaishia pale. Habari ya mifupa watu walikuwa wanasafiri leo hizo huduma zote zinapatikana pale kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ndio maana nimesema nampa Waziri yale mepesi mepesi. Baada ya kuwa vifaa vingi vimefungwa pale, ile transformer iliyoko pale ni ndogo. Sasa vifaa vingi vinashindwa kufanya kazi. Sasa tukisema vifaa vingi vinashindwa kufanya kazi, maana yake ni kwamba kuna watu wanaendelea kukosa huduma kwa sababu ya shida ya umeme na tatizo ni transformer iliyoko pale ni ndogo. Hilo nalo naamini kwa Waziri wala si suala kubwa, alishughulikiwe mara moja kwa maana ya aidha azungumze na Waziri mwenzake Mheshimiwa January atupatie transformer kubwa, basi kama vipi waweze kununua ili tuweze kupata huduma hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo kwetu ni la muhimu sana, ambalo na lenyewe nalo liko kwenye uwezo wa Waziri. Mji wetu wa Musoma kama nilivyokwisha sema ni mji ambao uko pembezoni. Kwa hiyo lazima tuwe na mikakati ya kuufanya mji ule ukue. Sasa liko suala ambalo mimi binafsi toka ile hospitali inajengwa pale nilianza kuomba kwamba angalau iweze kuwa sehemu ya chuo kikuu kwa ajili ya kufundisha wauguzi pamoja na Madaktari. Baada ya kuwa nimeliomba hilo Serikali imeendelea kuchelewa, lakini bahati nzuri tumekuja kivingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo Kikuu chetu sasa cha Mwalimu Nyerere kimeleta ombi pale kwamba lile eneo la hospitali yetu ya Kwangwa kwa sababu ni kubwa watukatie pale hekari 20 ili tuweze kujenga pale Tawi la Chuo Kikuu ambacho kitakuwa kinatutolea wataalam kwa ajili ya magonjwa mbalimbali. Kwa hiyo naamini hilo ni suala ambalo liko kwenye uwezo wa Waziri. Akishalitolea hilo uamuzi, basi mara moja kile chuo kikuu kitajengwa pale na Mji wetu wa Musoma na wenyewe nao sasa utakuwa miongoni mwa miji mizuri iliyoko hapa kwetu Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni ushauri, Mheshimiwa Waziri sisi wote hapa tumezaliwa na wazazi na kwa sababu tumezaliwa na wazazi, wale wazazi wetu sasa wameshakuwa watu wazima wanahitaji huduma zetu na hata ukiangalia katika nchi zingine zimeelekeza zaidi katika afya au kwenye kuwatunza wazazi. Sasa sisi tulikuja na sera nzuri kwamba wazazi wale ambao wana umri zaidi ya miaka 60 waweze kutibiwa bure. Mpaka sasa wazazi wetu wengi wanataabika, maana akienda mara aombwe kitambulisho hiki, akipeleka hicho kitambulisho mara anaambiwa hizi dawa hazipo. Kwa hiyo wanapata shida sana. Kwa hiyo, ombi langu la kwanza ni kwamba, kama kuna watu tunahitaji kuwapa bima ya afya ni pamoja na wazazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwombe tu Waziri kwamba katika yote hilo ujitahidi ulifanyie sana kazi.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Manyinyi.
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)