Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini mimi na Mheshimiwa Ummy Mwalimu kuiongoza Wizara ya Afya. Sisi tunachomhakikishia ni kwamba hatutamwangusha.
Mheshimiwa Spika, namshukuru Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa miongozo yao ya wakati wote ambayo imekuwa ikitusaidia mimi na Mheshimiwa Ummy Mwalimu katika kazi zetu.
Mheshimiwa Spika, nikushukuru wewe kwa usimamizi mzuri na ushauri mzuri kwa wakati wote ambao tunafanya shughuli zetu za kibunge hapa. Wabunge wamesema hapa, wakaniona mimi ni sawa wamemwona Mheshimiwa Ummy Mwalimu, na wakimwona Mheshimiwa Ummy Mwalimu ni sawa wameniona mimi. Maana yake ni kwamba, niwaambie tu ukweli, sisi Wizara ya Afya tunajigamba sana, tunaye Waziri wetu, dada yetu, mshauri wetu, lakini ni mtu ambaye hata kabla wewe hujasema, tusitaje sana majina ya Mawaziri, yeye tayari alishaniambia hakuna sababu ya kulitajataja. Sisi tupige kazi, hudumia Wabunge, twendeni mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo niseme machache na mnisikilize kwa umakini nioneshe tuna Rais wa namna gani, na ni kwa namna gani kwa kipindi kifupi ameweza kufanya kazi kubwa ambapo kwa upande wangu mimi, matatizo yote ambayo mnayaona hapa, yeye Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupandisha mlima, na sasa tunachokiona mbele yetu ni kichuguu, na kichuguu hatutakipanda, tutaenda kukivuruga.
Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye hospitali zetu za kanda, ukianza hospitali za kanda na za Taifa, kwa mwaka huu mmoja, zimepelekwa zaidi ya shilingi bilioni 51.4. Ukienda kwenye hospitali zetu za mikoa peke yake, ujenzi tu, zimeenda shilingi bilioni 54.2. Ukirudi kwenye hospitali zetu hizi za mikoa pamoja na za Taifa, fedha zilizokwenda kwa ajili ya vifaa tiba ni shilingi bilioni 290.9, ni fedha nyingi sana. Maana yake ni nini? Hizo fedha zimefanya mapinduzi makubwa sana ambayo mmeyaona hapa. Waziri wetu ameonesha mtoto ambaye ametibiwa hapa na ni huduma ambayo tulikuwa tunaenda kuipata nje kwa zaidi ya shilingi milioni 250. Leo anatibiwa ndani ya Tanzania kwa shilingi milioni 30 na kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukienda kwetu pale Muhimbili, Hospitali ya MOI utakuta leo tulikuwa tunaenda kwa zaidi ya shilingi milioni 80, wenzetu wanapokuwa na vivimbe chini ya ubongo, tunawapeleka India kwa ajili ya kuwatibu hivyo vivimbe kwa zaidi ya shilingi milioni 80. Leo wanapona ndani ya Tanzania kwa shilingi milioni saba, bila kufungua kichwa, wanaingiza mashine kwenye pua na wanatoa vivimbe chini ya sakafu ya ubongo na mtu anarudi nyumbani kwake amepona.
Mheshimiwa Spika, maana yake nini? Hizo fedha zimeokolewa, ni fedha ambazo zilikuwa ziende nje, halafu sasa zimebaki ndani ya Tanzania zipo kwenye mzunguko wetu ndani ya Tanzania zinasaidia wananchi. Ndiyo maana umeona leo wamekuja Zambia, Rwanda na Malawi juzi mmeona watu wetu wamekwenda kule. Maana yake Rais wetu amepunguza rufaa kwenda nje kwa asilimia 97. Maana yake sisi na wenzetu waliokuwa wametuzunguka, tulikuwa tunaenda kupanga foleni India kwa pamoja. Rais wetu amefanya kazi kwa asilimia 97, leo tunabaki ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, na wenzetu tuliokuwa pamoja tunapanga foleni nje kule India, leo amewarudisha, wanatibiwa ndani ya Tanzania. Ni kazi kubwa sana imefanywa na Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maana yake ni nini? Ndiyo maana nasema, nawaambia tusiwe na wasiwasi kwa sababu bado tuko na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, tuko naye, tutakuwa naye mpaka 2025 na tunakuwa naye mpaka 2030 na ataendelea kupiga kazi kubwa ya namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yamezungumziwa masuala ya upatikanaji wa dawa kwenye vituo vyetu na zahanati zetu. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge, hili suala la upatikanaji wa dawa lina sehemu nyingi. Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshafanya kazi yake, ametoa fedha kwa ajili ya dawa kusambazwa kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Spika, nitoe mfano wa Ngara. Mbunge wa Ngara hapa alikuja akamlalamikia Mheshimiwa Waziri wa Afya, akamwambia kwamba kuna shida ya wizi wa dawa kule. Mheshimiwa Waziri wa Afya akanituma na Mbunge wa Ngara akatoa Press kwenye wilaya yake akilalamika kwamba kuna wizi wa dawa. Mheshimiwa Waziri wa Afya akanituma niende Ngara, nilipofika Ngara, Mheshimiwa Mbunge wa Ngara akanionesha summons ya kutoka Mahakamani. Akaniambia; “amenishtaki DMO, amenishitaki Mfamasia, wananiambia nimewachafua kwamba wameiba dawa.” akaniambia, “wamemwambia nikiongea na wewe usiwaguse, wana-withdraw hii summons ya shilingi milioni 600 wanayokudai.” Nikamwambia, usiogope, sisi tutaenda mbele. Hata kitendo cha kutishia Bunge kwa kutumia mwanasheria, hicho kinatosha kuwaondoa hapa.
Mheshimiwa Spika, tulipoingia kwenye kikao, wataalamu wetu walifanya kazi, tukatoa mikoba kwenye Kamati ya Ulinzi na Usalama, na Ushahidi. Wote pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama tukakubaliana kwamba DMO na Mfamasia watoke kwenye Wilaya ya Ngara. Wametoka, na leo ukimwuliza Mbunge wa Ngara, anakwambia dawa zipo kwenye wilaya yake.
Mheshimiwa Spika, ninachokisema hapa ni nini? Anakwambia dawa zipo kwenye wilaya yake. Ninachosema, suala ni kwamba mafisadi wana ushirikiano. Sisi watu wema tunakosa kushirikiana. Ninawaomba Wabunge, suala la kupambana na wizi wa dawa tusaidieni. Amesema Waziri wa Afya, ameshatoa maelekezo kwamba kuanzia sasa tukienda kujenga uwezo wa timu zetu za mikoa na wilaya tutajenga uwezo pia wa timu za ulinzi na usalama za wilaya ili waweze kufanya. Hata hivyo, Waheshimiwa Wabunge, tushikane mkono, tushirikiane pamoja tutandike wezi. Wangapi wananikubalia hilo? Piga makofi. Tuko pamoja? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, haiwezekani Wilaya ya Siha wezi waibe, haki ya Mungu siji kulalamika Bungeni, namalizana nao huko, kama ni Serikali itanikuta Siha nikishughulikia majambazi. Kwa hiyo, nawaomba leo Wabunge wote tukitoka hapa, sisi ni Madiwani tusikubali dawa yoyote ipotee. Tusingojee kuja kulalamika Bungeni.
Mheshimiwa Spika, kuna eneo lingine linaloitwa Mshitiri. Hili eneo la Mshitiri ni kijiwe kingine cha kuiba. Nimewaambia Wabunge na kote ninakopita kwa ma-DMO, nawaambia mkiona Mshitiri analeta bei kubwa mwondoeni. Nimekwenda Nzega kwa Mheshimiwa Bashe, Mshitiri amehonga watu huko ndani, dawa ndani ya hospitali ni bei ghali kuliko nje kwenye duka la Mshitiri aliyechaguliwa. Tulichokisema, tukamnyoosha Mshitiri, sasa hivi kule kwa Mheshimiwa Bashe mambo yanaenda vizuri. Ninachowaomba Waheshimiwa Wabunge, twendeni tukashirikiane pamoja kwenye eneo hili la kushughulika na wezi.
Mheshimiwa Spika, Ndugu zangu niwaambie kitu kimoja. Wengine mmetaja masuala ya ambulance hapa, lakini amesema Waziri wetu, Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha, zimenunuliwa ambulance 727. Wakati huo, Waziri wetu alipoona kulikuwa na taratibu za kimanunuzi zinazotuletea mambo ya ajabu, akakataa, akasema hatununui kwa kufuata hizi taratibu za kimanunuzi, twendeni tukatafute mtu wa kutuuzia moja kwa moja na matokeo yake tukaongezewa kutokana na kuokoa zile fedha, zikaongezeka ambulance 168. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maana yake ni nini? Wote pamoja tukiungana kupambana na ufisadi kuanzia kwenye eneo la manunuzi na kuanzia tunapotoka majimboni haki ya mama hizi fedha mama yetu anayopeleka kule zitafanya kazi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilikuwa naulizwa na mtu mmoja ananiambia kwanini fedha za afya zimepelekwa kwenye maji wakati ule wa corona? lakini nikamwambia Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anajua hesabu. Alijua ukipeleka dola moja kwenye maji, unapunguza dola nne upande wa afya na ukipiga mahesabu ya teknolojia aliyoileta hapa Tanzania halafu ukapiga hela zilizotolewa dola zilizookelewa kwenda nje unajua huyu ni Rais anaejua nifanye nini? Niokoe dola, wakati wenzangu nje dola zimewaishia yeye ana dola ndani.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana wenye akili walikaa wakasema huyu astahili tena kuitwa Samia Suluhu Hassan aitwe Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa sababu amepiga mahesabu ikaonekana wenzetu sasa wanapita kwenye ugumu mkubwa sana wa kiuchum, lakini sisi tuna nafuu kwa sababu Rais wetu kila kitendo anachokifanya kinabakiza dola nyingi ndani ya nchi badala ya kutoa dola nyingi nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema kimoja, Mheshimiwa pale Mbeya kwako tulikuwepo na Kamati ya Bunge, tukawa tunatembelea na wananchi walikuwepo, tukawa tunatembelea majengo ya hospitali ya mikoa zaidi ya bilioni saba. Tumekwenda lile jengo la mama na mtoto ambalo limegharimu zaidi bilioni 19 pamoja na vifaa kuna MRI, kuna CT – Scan.
Mheshimiwa Spika, wananchi wakaniambia kabla ya wewe kuwa Mbunge, walikuwa wanaota sugu kutoka huku kuja Muhimbili kutafuta huduma. Lakini baada ya wewe kuwa Mbunge leo wananchi wa Mbeya Mjini wanabaki wanapata huduma za kinamama za kibingwa bobezi ndani ya Mbeya wanapata MRI ndani ya Mbeya, wanapata CT – Scan ndani ya Mbeya na tunataka kuwataarifu watu wengine wananchi wa Mbeya Mjini hawataota tena sugu kutoka Mbeya kwenda Dar es salaam wanataka kutulia na Dr. Tulia wao, waanataka kutulia na Dr. Tulia wao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie la mwisho kwamba leo ndani ya Tanzania Afrika kuna nchi nne tu, ambazo zina kiwanda cha kuzalisha mionzi dawa. Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan amejenga kiwanda Ocean Road na sasa tunaenda kuwa nchi ya tano Afrika kwa kuzalisha mionzi dawa na mionzi dawa hiyo kila mwaka ilikuwa inatusababisha tutoe bilioni tano nje ya nchi sasa zinabaki ndani ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nakushukuru sana. (Makofi)