Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa, nami nipongeze sana kwa kazi nzuri inayofanywa katika Wizara ya Elimu. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuyatenda hayo, nampongeza Waziri na watendaji wote na hasa Wakurugenzi wa taasisi mbalimbali katika Wizara ya Elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi zangu zinakwenda kwa sababu sasa hivi tunaona vyuo vya ufundi vinajengwa vya kutosha halafu kuna hii project ya HEET imesaidia sana katika kuboresha mitaala na pia ujenzi wa mashule. Pia hii bodi ya mikopo tulianza na shilingi bilioni 450, leo hii shilingi bilioni 654 ndiyo zimepelekwa kwa wanafunzi. Hili jambo Waheshimiwa Wabunge wenzangu limeleta utulivu mkubwa sana katika vyuo vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba tu hapo kwenye HEET, Mheshimiwa Waziri ananisikia, mmetoa mgawanyo mzuri sana wa Universities hizi za Serikali, sasa tupate hata mgawanyo wa fedha za HEET katika universities zile za binafsi, tunaziita private universities; ule mgawanyo mnasema kwamba wao wamepewa fedha kwa ajili ya kuwasomesha, lakini tupate mgawanyo unaoonesha kwamba, je, universities zitapata mgawanyo wa walimu wangapi kwenda kusoma, ili na wao watulie? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwa hawa watendaji wa kati. Watendaji wa kati ndio msingi mkubwa sana wa kuchochea maendeleo hasa kwenye uchumi. Vyuo vyetu vitano kama unakumbuka; DIT, MUST, ATC, NIT na kile Chuo cha Maji viliondoa kabisa malengo yake ya zamani. Yale malengo yaliondoka kabisa, kwa sababu vyuo hivi vyote sasa vilijikita katika kutoa shahada. Siyo vibaya, lakini naomba sasa vyuo hivi virudi kwenye malengo yake ya zamani, ndiyo tutapata hao mafundi tunaowaita mafundi mchundo na wahandisi. Wajikite pia katika yale malengo ya zamani kama nilivyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kozi za kati kwa sasa hivi kwa wasichana ni asilimia 25 tu kwa taarifa, sasa tuangalie, tuongeze juhudi za kuona wasichana pia wanajiunga katika hizo kozi za kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Tanzania uwiano wa watendakazi kwa sasa, nina maana ya mhandisi, fundi mchundo na mafundi stadi ni kumi kwa tisa kwa saba (10:9:7). Sasa hii haikubaliki, tumegeuza. Sasa muundo au uwiano unaotakiwa kidunia au kiulimwengu ni moja kwa tano kwa ishirini na tano (1:5:25). Yaani unapokuwa na mhandisi mmoja, basi uwe na hao mafundi mchundo watano, uwe na mafundi stadi Shirini na tano, lakini sisi tunafanya vice versa na ndiyo maana tunapata shida sana katika watendaji hawa mafundi mchundo na hawa mafundi stadi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumegeuza ndiyo, tunazalisha shahada, siyo mbaya, lakini sasa tuone, kama nilivyosema, ukuaji wetu wa uchumi sasa hivi tujipange kuona kwamba hawa mafundi watendaji kazi wanakuwa wakubwa zaidi na namba yao inaongezeka zaidi. Sisemi kwamba shahada tuziondoe, Hapana, la hasha, lakini nasema tujipange kuona kwamba uwiano huu twende kidunia zaidi, ndiyo tunaweza kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali sasa kuongeza hiyo bajeti ya mikopo, wastani wa asilimia 70 mpaka 80 zinakwenda kwa wanafunzi wale wanaochukua masomo ya arts, hiyo ndiyo taarifa. Yaani wa masomo ya arts asilimia 70 mpaka 80 ndiyo zinakwenda kwao, ukiangalia hii bajeti ya mikopo. Sasa ukiangalia wanafunzi wanapomaliza masomo, wengi wao wanakaa muda mrefu sana bila kupata ajira, lakini ndio wamechukua hiyo asilimia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema sasa tuanze kujitafakari, yaani hiyo iwe katika mpango, akilini mwetu, tuanze kujipanga sasa. Je, watoto hawa wanaomaliza Kidato cha Nne na cha Sita, siyo vema wakaanza kupata mikopo ili waweze kujiunga na kusomea ujuzi uwasaidie kujiajiri? Hilo mliweke yaani kama mpango wa baadaye, muanze kulifikiria sasa hivi. Maana yake tunapompa mkopo huyu mtoto anayemaliza Chuo Kikuu halafu unakuta hata ajira hana, amesoma tu shahada, ajira hana. Inaleta shida na wakati mwingine kumwongezea mzigo wa umasikini. Kwa hiyo, tujipange kwenye eneo hilo tuione kama sasa tunaweza kufanya, akimaliza form four au form six, anapata mkopo, anakwenda kwenye fani za ujuzi na kuweza kujiajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye ujenzi wa vyuo vikuu. Hili nalisema kwa masikitiko makubwa sana. Mkoa wa Mtwara na Ruvuma, yaani hata ukiangali vile vyuo vikuu vya private vingi vimekufa. Nilikuwa nafikiria, hivi Serikali, haiwezi kusaidia? Kwa mfano, tulikuwa na chuo cha udaktari pale Peramiho, kikafungwa, wale wanafunzi wakapelekwa Mbeya. Yale majengo yako pale, wananchi wa kuzunguka yale maeneo ya Peramiho waliwekeza sana katika majumba na mashamba, lakini sasa hivi wamebaki pale hakuna kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukafikiria wakati mwingine tukasikia kuna chuo Tunduru, Branch ya SUA. Ghafla tukaona ile SUA imekwenda Katavi. Siwaonei wivu, wala sikatai, lakini pale ambapo wazo la Tunduru lilianza, kwa nini halikuendelezwa, badala yake sasa nguvu ziko Katavi? Sasa wanasema huenda kikaendelezwa. Naomba Mheshimiwa Waziri Chuo cha Tunduru pale branch ya SUA, nguvu mnazozipeleka kule Katavi zianze pale kwanza, kwa sababu Katavi ilikuwa ni ya pili. Kule hatuna mradi mkubwa, nikwambie ukweli. Hatuna mradi mkubwa wowote Ruvuma wala huko Mtwara. Miradi mikubwa na sisi tunaipenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mnafikiria kujenga Chuo Kikuu sijui cha IT Dodoma, niliwaza sana. Kwa nini hamkukipeleka Ruvuma? Dodoma kuna hii UDOM ambayo sasa hivi imekuwa kubwa na ina changamoto za kutosha. Kwa nini hiyo IT mnayosema chuo kikubwa kinajengwa hapa Dodoma kisijengwe hata kule kusini tukawa na sisi na mradi mkubwa? Miradi mikubwa nasema hata ya maji, hatuna, Ruvuma na Mtwara ni shida. Kwa hiyo hii ya vyuo, niwaombe sana msaidie kama ambavyo Mheshimiwa Mkapa alivyosaidia ile Muslim University ya pale Morogoro, walikuwa na changamoto ya majengo, akawasaidia akawapa majengo. Serikali ulizeni hivi vyuo, kwa nini hiki chuo cha udaktari pale Peramiho kimekufa? Kwa nini kile chuo kingine cha St. Joseph, Ruhuiko kinakufa na ninyi mpo? Hebu wasaidieni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hivyo vyuo vikuu, nirudi tena. Kila siku tunaongea hapa, Chuo cha UDOM ni Chuo Kikubwa Afrika Mashariki. Nenda pale, utashangaa. Yale majengo yanaporomoka, roof inaanza kudondoka, vigae chini vimepasuka, na mabomba ya maji yamepasuka. Nimekwenda pale nikaingia kwenye vyoo vya kule UDOM, yaani mpaka unaona aibu. Kuna mlipuko utatokea. Maji yanapotea pale kwa sababu mabomba yote yamepasuka. Wana upungufu wa maji karibu lita milioni 1.1, Serikali mpo. Sitaki Mheshimiwa Waziri tuongozane, nenda ukaone UDOM, hali ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu pale pale UDOM kuna jengo la Chimwaga. Ule ni ukumbusho mkubwa sana. Sasa tuangalie, Chimwaga tunaiacha hivi hivi? Tuliingia mle ndani wakati tunafanya lile kongamano, yaani unaingia mle ndani unafurahi. Ni ukumbi mkubwa mno, lakini angalia nje. Ynatakiwa ukarabati ufanyike, tena kwa kumuenzi Mwalimu Nyerere na kwa kuenzi Makao Makuu ya hapa Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuzungumzia shule kongwe. Kuna shule kongwe zimesahaulika kabisa. Kuna shule kongwe ambayo Mheshimiwa Mkapa amesoma huko, Marehemu Mheshimiwa Profesa Mbilinyi alisoma huko, inaitwa Shule ya Kigonsera, hakuna maktaba, you can’t imagine. Kuna form five, pale wapewe maktaba, na watoto wajifunze kujisomea, ahsante sana. (Makofi)