Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli kwenye sekta ya elimu kule kwetu Hai amefanya mambo makubwa sana. Pamoja na kwamba ni TAMISEMI, lakini kwa kweli tunashukuru shule zetu zile kongwe, kwa maana ya Machame Girls na Lyamungo, sasa hivi zinang’aa, zimefanyiwa marekebisho; pale Hai Day na kila mahali kwa kweli kwenye sekta ya elimu ametufanyia mambo makubwa sana. Nampongeza na apokee salamu nyingi za shukurani kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Hai.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayofanya kwenye sekta hii. Hongera sana. Naibu Waziri pamoja na wasaidizi wako wote tunatambua mchango mkubwa sana. Pia nawashukuru sana walimu wetu na watendaji wote kwenye sekta ya elimu kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa Taifa letu. Ikumbukwe haya yote tunayojadili kwenye bajeti hapa, mtekelezaji wake kwenye ubora na kwenye kila kitu ni wale watumishi. Kwa hiyo, naomba nitambue mchango wao mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kwenye sekta ya elimu na afya kuna wadau wetu wa maendeleo, na hawa sio wengine ni taasisi za dini. Naomba kwa nafasi hii nimshukuru sana Shehe Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, kuna taasisi nyingi zinatoa elimu kule kwetu Hai kama Mudio na nyingine. Pia namshukuru Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo, ametuletea pale kwetu chuo kikuu, kinaendelea pale. Vile vile pale KCMC kuna chuo kizuri ambacho kinatoa elimu kwa wauguzi wetu na madaktari wetu, nawapongeza sana. Kipekee, nampongeza sana Dkt. Masenga kwa kazi nzuri anayoifanya pale KCMC na kule Mkwarungo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kuchangia hoja hii kwa kuzungumza eneo moja linalohusu stahiki za Wahadhiri wa Chuo Kikuu. Tumekuwa tukizungumza hapa habari ya walimu, tumetoka kwenye walimu, na leo naomba nizungumzie Wahadhiri wa Vyuo Vikuu. Bahati nzuri na Waziri naye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu, anaelewa adha ambayo wanapata Wahadhiri wenzake. Tusipotazama eneo hili tukawapa heshima stahiki, hata hii mitaala tunayoenda kuiandaa bado haitatusaidia, kwa sababu watekelezaji na wasimamizi ni hawa watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta mwalimu anayesimamia research ana wanafunzi zaidi ya 20. Hebu niambie, tunaenda kutengeneza watu wa Ph.D wa aina gani? Nami kwa ku- declare tu, ni mwanafunzi wa Ph.D pale UDOM. Kwa hiyo, naona ugumu ulivyo. Unamtafuta mwalimu wiki tatu, na siyo kwa makusudi anafanya hivyo, lakini ana wanafunzi wengi. Akitoka hapo, unakuta anamiliki saluni Dodoma. Hata walioko kule SUA ambao tulitegemea wamiliki mashamba, wamiliki mifugo, tunakutana nao wanamiliki bar huku. Kwa nini wanafanya hivi? Stahiki zao hazitoshelezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, leo nitasimama hapa kuomba sana Mheshimiwa Waziri, ninafahamu linahusisha Wizara nyingi, lakini kwenye eneo hili kaa na Wizara wenzako wanaohusika kwenye jambo hili, tuwape heshima hawa wahadhiri, ndiyo kiwanda kinachofyatua watu wa kuja kutusaidia kwenye sekta zote. Tukiendelea kuwaacha, waache ku-concentrate kwenye eneo la elimu, wakawa na shughuli nyingi wanazofanya za kujitafutia kipato, hatutawatendea haki. Nami nashauri, hawa watu, wakifika level fulani ya uprofesa, ili aweze kutulia kule alipo afanye kazi yake kwa umakini, ni lazima tuangalie stahiki zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nimeanza viashiria vya utafiti wangu, kuona ni kwa namna gani watu wanaotoka kwenye taasisi za elimu kukimbilia maeneo mengine, hata humu ndani, gap linalobaki kule, nani anayelitunza? Naomba sana, majibu ya haraka ni kwamba hawa watu wapate stahiki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nizungumze kuhusiana na nidhamu ya wanafunzi walioko chuo kikuu. Mheshimiwa Waziri tusipotazama jambo hili litatuletea shida. Hao walioko chuo kikuu wengi wanasoma degree. Kwa hiyo, tunawaandaa kuwa viongozi. Sijui ukipita hapo Dodoma unajifunza jambo gani, au pale UDOM? Ukimwona kijana aliyeko sasa hivi mwaka wa tatu, anafanana kuandaliwa kuja kuwa kiongozi na msimamizi wa taasisi wa Serikali? Wakati mwingine wahadhiri kule wanalalamika kwamba eti sisi wanasiasa, wakiguswa kidogo, sisi ndio tunawatetea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisimame hapa niseme kwamba hawa ndio viongozi tunaowaandaa. Ukimwona mtoto mwenye degree leo, unapishana naye Mheshimiwa Waziri, kwa kweli inasikitisha. Huwezi kumtofautisha na aliyeko Form Two na anayesomea degree.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakutana na mtoto kala ndala anapita kwenye mitaa ile physical appearance ya kuandaliwa kama kiongozi haifanani. Niombe mambo haya, wenzetu wa SAUT wamejitahidi sana kufanya hivyo. Mambo ya nidhamu yanaenda sambamba na utoaji wa taaluma, hatuwezi kuviacha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwenye eneo hilo pia…

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naungana kabisa na anachokizungumza Mheshimiwa Saashisha. Wanafunzi wengi wanakulia boarding schools, wanapofika kwenye level ya chuo kikuu wanakuwa wamepata uhuru mkubwa sana. Mwanafunzi mazingira haya anakuwa hana control yoyote na hawa ndio wanategemewa kuja kuwa watumishi wetu. Mheshimiwa Waziri pia wanafunzi wanao disco idadi imekuwa ni kubwa sana kwenye vyuo kutokana na jambo hilo ni vema Serikali ikaangalia jinsi gani ya kuli–control.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Saashisha, taarifa hiyo.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea kwa mikono miwili na niendelee kusisitiza kwa kweli Mheshimiwa Waziri tazama eneo hili ili tuweze kupima elimu yetu kabla hatujaenda kwenye utekelezaji wa mtaala mpya.

Mheshimiwa Naibu Spika, niingie kwenye kuchangia mtaala mpya ambao tunaendelea na majadiliano nao. Nilikuwa natamani Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa utuambie hivi mmefanya tathimini ya utekelezaji wa mtaala wetu tangu tumepata uhuru mpaka hapa tulipo umetupa matokeo gani? Nitaomba kupata hilo na kama hatujafanya wakati tunaendelea basi tuweke fikra zetu kutazama huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikisema hapa Mheshimiwa Waziri na mwaka jana nilichangia, kwamba mawazo yangu ninafikiri ili tuwe na mtaala mzuri tutanguliwe na malengo ya Serikali na sijui kwa nini linakuwa gumu hili? Nichukue wito huu kukuomba wewe una wataalam wengi Maprofesa wako huko hebu wafanye utafiti ni namna gani nchi yetu inaweza ikawa na malengo na maono ya muda mrefu. Tuwe na Tanzanian interests za kwetu ambazo tulitekeleza kwa kipindi cha miaka 100.

Mheshimiwa Naibu Spika, tungekuwa na malengo hayo na maono hayo ya miaka 100 tunapokuja kutengeneza mtaala huu unatakiwa u–reflect National objectives. Yale malengo ya Serikali ya miaka mitano, malengo ya Serikali ya miaka 100 basi mtaala huu unamwandaa Mtanzania aweze ku-fit kwenye malengo tunayotaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama tumeshaanza mchakato kwa kutazama malengo ya miaka mitano fine. Lakini tunajua mtaala huu muda wake wa utekelezaji unaendelea hauna kikomo. Utaendelea kufanyiwa marekebisho kama huko nyuma ambavyo imekuwa ikifanyiwa marekebisho. Sasa kama ni jambo kubwa namna hii ni lazima tutengeneze dira na tusiwe waoga wa kufikiri mambo makubwa. Hata wenzetu ambao wanakwenda kwenye sayari za mars walianza kama sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuweke malengo makubwa, maono makubwa ya kufanya mtaala huu huko unakoenda uweze kujibu matarajio ya mahitaji ya wananchi. Niseme tu mtaala huu u–focus mara nyingi tumekuwa na shida ya career choice ya watoto wetu. Mwanafunzi anakwenda chuo kikuu hana maono hajui anafika kwenye jambo gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tutumie mfumo wa co- curriculum kutazama elimu au mtaala huu tunaotengeneza ukaongezee talanta aliyonayo mtoto. Kuliko kulazimisha mtu hana sifa ya kusoma sheria mradi tu baba yake alisoma sheria tumlazimishe aende huko. Niombe namna ya kutama career choice liwe kama somo ambalo linalofundishwa kuanzia kidato cha tano na sita ili watoto waweze kujiandaa wanakwenda kuwa wakina nani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefurahishwa sana na mwonekano na mawazo yaliyoko kwenye mtaala huu mpya unaokwenda sasa kugusa ujuzi. Mheshimiwa Waziri, niombe na nilisema hapa mwaka 2022 eneo hili libaki la kwetu ndani, na hata kama kuna utekelezaji unaohusika tusihangaike sana na hela za watu. Password ya maendeleo yetu, password ya uwezo wetu wa kufikiri uko kwenye knowledge na skills za watu wetu. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri tafadhari tazama eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningetamani kugusa, wapo walimu wastaafu, kwa kuwa wewe ndio Baba yao na wewe ndio mlezi wao wengi wamestaafu miaka mingi. Ninafahamu utaratibu wa vikokotoo ulivyo, wao wametumikia Taifa wengine mara baada ya uhuru, wengine wale ambao wachache wamebaki, na wengine miaka ya 50, miaka ya 40 wamestaafu, unakuta wanacholipwa ni kidogo mno. Hapa nina messages nyingi wanaomba jamani wakumbukeni, nikuombe sana kaa na Wizara ya TAMISEMI, kaa na Waziri wa Fedha, muone namna ya kuwakumbuka hawa wastaafu ambao wameitumikia nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa formula ile iliyokuwa inatumika wakati ule sambamba na kwa wahadhiri wa vyuo vikuu, formula iliyotumika wakati wanastaafu haikuwa rafiki kwao. Pamoja na uchumi wetu bado haujakuwa katika kiwango hicho naomba muwatazame. Unakuta mtu analipwa shilingi 20,000, shilingi 50,000, hebu tutazame viwango hivi pamoja na kwamba ninafahamu kulikuwa na formula ya wakati huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho niombe sana, Wizara ya Afya wametengeneza guideline ya wale wauguzi na watoa huduma wa afya wanaojitolea. Hebu na hapa Mheshimiwa Waziri, tafuta utaratibu wa kutengeneza na wewe guideline ya walimu wanaojitolea kwenye shule zetu ili inapofika wakati wa ajira kuwe na guideline inayowaongoza.

Mheshimiwa Spika, pia hata kama sio kuajiriwa, kwa maeneo yale ambayo Serikali hatujaweza kufika kwa maana ya kuajiri kuwe na mwongozo proper unaowaongoza kuelekea kupata ajira lakini hata kuajiriwa na kulipwa na wazazi kuwe na mwongozo fulani unaowaongoza ili kuepuka mkanganyiko ambao unajitokeza sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho Mheshimiwa Waziri, ninakuomba, zamani tulikuwa na mitaala inayotoa elimu ya ufundi kwa shule za misingi. Kwa mfano; pale kwangu Hai tulikuwa na shule kama nne zinatoa elimu ya ufundi. Zilikuwa zinaitwa shule ya msingi ufundi, shule kadhaa mtaala ule au utaratibu ule umesitishwa na mitihani imesitishwa. Lakini kuna majengo, kuna walimu na kuna rasilimali. Niliwahi kuuliza swali hapa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, akatuambia kwamba hizi shule zimefutwa na sasa tunaelekea VETA. Lakini hizi rasilimali zilizoko katika hizi shule nani anazitunza?

Mheshimiwa Naibu Spika, nategemea pale kwangu tumekwishajenga Chuo cha Ufundi cha Rundugai na sasa hivi tunahangaika na Losaa, zile mali na vifaa vile ambavyo vilikuwa kwenye shule hizi za msingi namna ya kuvihamishia viende kwenye vyuo vyetu kuliko kuviacha vitu vinaozea pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna walimu wana taaluma hizi, niombe wawe allocated kwenye maeneo ambayo wanaweza kwenda kuisaidia nchi yetu. Ikishindikana, kama maeneo hayana shule basi waingizwe kwenye vyuo vya VETA ili wasikae kwenye maeneo ya utoaji wa elimu ambayo wao hawawezi kusaidia nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema hivyo naona umewasha nakushukuru sana na naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)