Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Aloyce John Kamamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Bila kusahau kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutuletea fedha kwenye miradi mingi, ametufikia Kakonko, ametufikia Buyungu, tunamshukuu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, Katibu Mkuu, Manaibu Katibu Wakuu lakini bila kusahau watendaji kwa kazi nzuri, hongereni tunawapongeza sana. Lakini nipongeze Wizara kwa hatua nzuri ambayo mmefikia katika kuratibu mpango wa kurekebisha Sera ya elimu na mtaala, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, niipongeze Serikali kwa kupanua wigo wa kutoa huduma ya fedha kwa watoto wa kidato cha tano na sita ambapo takribani bilioni 10.3 zimetengwa kwa ajili ya watoto hawa tunaipongeza sana Serikali. Hii inakwenda sambamba na fedha za wanafunzi kwa ajili ya chakula, tumetoka shilingi 8,500 kwenda shilingi 10,000 si haba ni hatua nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze Serikali imeweza kupeleka miundombinu na imeweza kufanikisjha kwenye uandikishaji awali, Msingi na Sekondari. Lakini hali hii imepelekea upungufu mkubwa sana wa walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukipitia kwenye takwimu yetu ambayo imetolewa na BEST (Basic Education Statistics in Tanzania) ya mwaka 2021, kwa upande wa elimu ya awali, walimu waliokuwa wanahitajika ni mwalimu mmoja kwa 40 lakini hali ilivyokuwa ni mwalimu mmoja kwa 75. Kwa upande wa elimu ya Msingi waliohitajika ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45 lakini hali ilivyo ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 74. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na juhudi ambazo Serikali imeziweka kuajiri walimu 13,130, bado nisisitize Serikali kuhakikisha kwamba inaajiri walimu kwa ajili ya kukidhi mahitaji hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wilaya yangu ya Kakonko, kwa elimu ya awali walimu wnaohitajika ni 224 lakini wako walimu 14 tu upungufu ni walimu 210 upungufu ni sawa na asilimia 93.75 lakini kwa elimu ya Msingi mahitaji ya walimu ni 1189 wako 509 na upungufu ni walimu 680 upungufu sawa na asilimia 57. Nini unategemea katika maeneo kama hayo?

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe ufahamu tu kwamba, athari ya mapungufu ya walimu ni tofauti na mapungufu ya Daktari. Daktari asipopatikna leo Vifo vitatokea leo hii lakini athari ya kutokuwepo kwa walimu athari yake ni ya muda mrefu. Niombe sana Serikali ihakikishe kwamba ina ajiri walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nishukuru tumeweza kupangiwa majengo katika maeneo tofauti. Tumetengewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule mpya za Kazilamihunda na Nyamtukuza, lakini tumeletewa madarasa katika shule za Msingi, Bukiriilo, Gwarama, Kavungwe, Kigarama na Nyamwilonge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa elimu ya awali, tumeletewa fedha kwa ajili ya Shule ya Msingi Gwarama. Pia tumeletewa fedha kwa ajili ya Shule ya Msingi Bukirilo, Gwarama, Kavungwe, Kigarama na Nyamwilonge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeletewa fedha kwa ajili ya nyumba Shule ya Msingi Nyakaviro, hii ni pamoja na VETA. Sisi tunaendelea kushukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo nichangie kwa upande wa wanafunzi wanaopata elimu hasa watoto wa kike baada ya kupata ujauzito.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tungehitaji kujua baada ya kuweka utaratibu huu, ni wanafunzi wangapi sasa wa kike wameweza kupata elimu baada ya Mheshimiwa Rais kutoa nafasi katika eneo hili? Baada ya hapo ni vema tukafahamu je, changamoto zilizosababisha hawa watoto kuweza kupata elimu mpaka wameweza kupata ujauzito na baadae wameweza sasa kurudishwa je, changamoto hizo tumezifanyia kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huyu Dada alikuwa yuko peke yake, sasa ana mtoto na anahitaji chakula kwa ajili ya mtoto huyu na anahitaji chakula kwa ajili ya mtoto huyu tunamsaidiaje sasa ili aweze kukidhi masomo yake? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye Sera ya elimu, mwanafunzi akiwa nje ya shule awe wa kike au wa kiume kwa siku 90 mfululizo anaondolewa shule. Tunaangalia sasa mwanafunzi huyu wa kike amepata ujauzito ni zaidi ya siku
270 anarudi shule, hapa panahitaji mjadala wa kutosha. Tunamsaidiaje sasa huyu mtoto wa kiume kijana, kwa mujibu wa Sheria hayuko shuleni kwa siku 90 ameondolewa. Kwa Sheria ile maana yake akiondoka ni moja kwa moja, tunamsaidiaje huyu mtoto wa kiume?

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria hiyo haitoi haki sawa, niombe Wizara ya Elimu iliangalie upya suala hili ili liweze kutoa nafasi sawa kwa watoto wa kike lakini vilevile kwa watoto wa kiume. Hawa Watoto wa kike tumeona changamoto ambayo inawapelekea mpaka wanapata ujauzito lakini mtoto wa kiume nae anakuwa na changamoto mbalimbali katika Maisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wanaotoka wanakwenda kwenye boda boda, wapo wengine wankwenda kufanya biashara hali inayopelekea sasa aondolewe nje ya mfumo. Tungetamani nae kwa kuwa mtoto wa kike ameweza kupewa nafasi baada ya kupata ujauzito na huyu mtoto wa kiume pamoja na kwamba kwa mujibu wa Sheria siku 90 zimekwisha na yeye atafutiwe utaratibu ambao utamsaidia kupata elimu baada ya kuwa nje ya mfumo rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango mwingine wa kwangu niupeleke kwa wadhibiti ubora. Mdhibiti ubora ndiye jicho la Serikali kwenye upande wa elimu lakini hawajaangaliwa ipaswavyo. Hawajaweza kupewa vitendea kazi vya kutosha ikiwa ni pamoja na fedha za kuweza kufanyia kazi na kuweza kufanya ufuatiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo takwimu ambazo zinaonesha kwamba ukaguzi wa shule haufanyiki kwa zaidi ya asilimia 30. Kwa hiyo, asilimia 70 ukaguzi wa shule zetu haufanyiki. Niombe sana Serikali ipeleke fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba ukaguzi wa shule unafanyika ipasavyo na hasa ikizingatiwa kwamba ndilo jicho linaloisaidia Serikali kujua changamoto mbalimbali katika shule zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ulitolewa waraka ambapo wadhibiti ubora wakuu wa shule wa wilaya walistahili kupewa fedha za madaraka sawa na wakuu wengine katika halmashauri. Nikwambie kwamba waraka huo haujatekelezwa. Kwa nini hawajapea stahili zao hizo? Niombe sana Serikali iangalie uwezekano wa wadhibiti ubora wa shule kuweza kupewa stahili zao sawa na wakuu wengine wa idara katika halimashauri. Nina uhakika wakiwezeshwa wataweza kufanya zaidi.

NAIBU SPIKA: Ahsante kengele ya pili.

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa niombe UNESCO kama ambavyo tumeshauri kwenye Kamati liweze kuzingatiwa. Ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)