Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Jeremiah Mrimi Amsabi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wataalam mbalimbali wa elimu na masuala ya maendeleo duniani wamebainisha uhusiano mkubwa wa matatizo mbalimbali katika Taifa yakiwemo ajira na ukosefu wa maendeleo endelevu kuwa na uhusiano mkubwa na elimu duni na pia kuwepo uhusiano mkubwa wa elimu na duni na mitaala duni na uwekezaji mdogo katika elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa, nampongeza Rais wetu, amezingatia ushauri huu wa wataalamu na sasa tumeona uwekezaji mkubwa kabisa katika elimu. Tunaona mapinduzi na mageuzi makubwa katika mitaala yetu. Kazi hii kubwa ambayo inafanyika, tumeiona na tunaipongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kipekee kabisa amesikiliza maoni ya Watanzania. Ni muda mrefu Watanzania walikuja na hoja hii ya uwepo wa mitaala mipya. Kwa mfano, katika aspect hii ya 7:4:2:3 na kuendelea, walikuja na maoni. Jambo hili ilianza muda mrefu, toka miaka ya 1985. Wenzetu Kenya walikuwa na mfumo kama huu, toka mwaka 1964 mpaka 1985. Walipofanya mabadiliko haya, kwao katika aspect hii wakaenda miaka minane, miaka minne, minne; kwetu Tanzania pia hitaji hili lilianza. Sasa kwa muda wote huo, hakukuwahi kuwepo mabadiliko mpaka wakati huu ambapo Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia amekubalia kufanya mabadiliko haya na tunampongeza sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Serengeti tunamshukuru kwa pesa nyingi ambazo tumepata kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA ambacho tayari sasa kinaendelea. Nawapongeza watumishi wote katika Wizara ya Elimu kuanzia ngazi ya Wizara mpaka kule Wilayani. Kipekee kabisa nampongeza Prof. Adolf Mkenda pamoja na msaidizi wake, Naibu Waziri Mheshimiwa Kipanga. Nimeangalia mitaala ile, uwezo wa kutafsiri vision kwenda na kuiweka katika grounds vizuri kiasi kile, sisi tunawapongeza sana, tunawaombeeni kazi iendelee vizuri na muimalize vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri mambo machache, kama manne, katika kuchangia bajeti ya Wizara hii. Moja, fedha ile ya SEQUIP, fedha ya uboreshaji wa elimu ya sekondari, naomba fedha hii ipelekwe kwa kiasi kikubwa kwenye ujenzi wa shule za ufundi. Nasema hivi kwa sababu, shule hizi za elimu ya jumla, tayari tumekuwa nazo nyingi sana, na tayari sote tunaona shule hizi hazijaweza kutusaidia vizuri. Sasa Serikali inaendelea kujenga shule zile zile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Serengeti pia tumepata shule ya Nagusi inajengwa. Shule kama ile tungependekeza ijengwe kuwa shule ya ufundi. Zipo shule nyingine zinazoendelea kujengwa, tungefika mahali ambapo tungehakikisha walau kila wilaya pamoja na uwepo wa chuo cha VETA iwe pia na Shule ya Sekondari ya Ufundi pamoja na Shule za Msingi za Ufundi za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kuwa uwepo wa shule hizi za ufundi, zitasaidia sana kwenda kulisaidia Taifa letu kukabiliana na changamoto kubwa hii ya ajira ambayo tunaendelea kukabiliana nayo kwa wakati huu. Kwa hiyo, Wizara ya Elimu ikishirikiana na Wizara ya TAMISEMI, waone sasa ulazima wa kwenda kupeleka fedha zile katika ujenzi wa shule za ufundi. Kwa kufanya hivi, tutaisaidia Wizara ya Elimu kwenda kufanikisha mtaala huu mpya ambao wanakuja nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaala huu kwa ujumla wake umejielekeza sana kuhakikisha tunahamia kwenye elimu ya ufundi na elimu ya vitendo kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo naomba sana hilo la kwanza. La pili, iko fedha ambayo tayari Serikali yetu imeomba World Bank na wamefanikiwa na pesa hii ndiyo hii tunaona sasa imeanza kutoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikiliza hotuba za Mawaziri wengi inaonesha kwamba fedha hii itaenda kutumika na itaendelea kutolewa kwa muda wa miaka mitano. Ushauri wangu, fedha hii tungeiomba Serikali ifanye kila linalowezekana itoke haraka na itumike yote mapema, ikiwezekana tuitumie ndani ya miaka miwili ili tuweze kufanya mageuzi makubwa haya ya elimu ambayo sasa yanaendelea kuinjiniwa katika mtaala huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kuwa tayari tumechelewa, tayari tuko nyuma, sasa ni vyema tufanye uwekezaji huu mkubwa kwa haraka. Katika uchumi, mradi wowote ukiutekeleza kwa muda mrefu, utaingia gharama kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukumbuke tayari Wizara hii ya Elimu inahitaji uwekezaji mkubwa katika vifaa hizi shule mpya. Shule hizi za mtaala huu mpya ambao una–focus zaidi katika ufundi unahitaji vifaa. Tumemsikia Waziri akizungumza habari ya ku–train walimu, tumesikia uhitaji wa kuajiri walimu wengine wapya hii yote itawezekana kama tutaruhusu kwenda kutumia fedha hizi nyingi kwa haraka. Tukienda taratibu, tunaenda taratibu mwaka baada ya mwaka kwa miaka mitano, kuna uwezokano tusifikie tija nzuri ambayo tunaikusudia na hasa ambayo wenzetu katika Wizara ya Elimu wanaendelea kuifanya katika mitaala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivi tutaenda kukabiliana pia na ule upungufu mkubwa wa walimu ambao tunauona upo katika shule zetu. Tayari inaoneka shule nyingi wanafunzi ni wengi sana madarasani, wanafunzi wengi wanakaa katika madarasa yetu wakiwa hata hawawezi kufundishwa na walimu wa kutosha. Wakati mwingine ile ratio ya one to fifty, kwenye shule za misingi na ile ratio ya one to forty-five imefika mahali inashindikana. Kwa hiyo, ndiyo maana tunaomba mitaala hii sasa twende kuitekeleza kwa uwepo wa fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo hili kama unavyoliona limejengwa mara mbili, kuna ile plan ya Artech’s pamoja physical concession. Sasa wenzetu katika Wizara ya Elimu wanakuja na plan, wamekuja na plan nzuri ya namna watakavyo engineer mabadiliko makubwa ya elimu kwenye nchi yetu. Lakini ile utekelezaji wake, implementation ya mitaala hii bila fedha ya kutosha ya haraka, naona mabadiliko haya yanaenda kushindwa. Kwa hiyo, niombe Serikali, Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na TAMISEMI na Wizara ya Elimu waone ulazima wa kupeleka fedha hii haraka na tusisubiri miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niombe sana mitaala ile nimeiona Mheshimiwa Waziri, mnafanya vizuri. Ushauri wangu muangalie, Marx pamoja na Friedrich Engels, katika kitabu chao maarufu kabisa duniani cha Das Kapital wanasema mode of production ita–determine jamii itakuwaje, elimu itakuwaje na mahusiano hata pia yatakuwaje, dini itakuwaje na jamii itakuwaje sasa katika utengenezaji wa mitaala hii ni lazima watengenezaji wa mitaala hii waangalie sana je tunazingatia context ipi katika utengenezaji wa mitaala hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho la ushauri wangu, niombe sana Wizara ya Elimu iangalie sasa ufundishaji bora wa kingereza. Iko shida katika namna ambavyo kingereza kinafundishwa wote ni mashahidi hapa hakuna mtu amewekwa darasani akafundishwa kiswahili lakini kwanini kingereza kinakuwa kigumu cha kueleweka? Ni namna ambavyo kinafundishwa approach imekuwa siyo sahihi. Nimeona mara nyingi mchina, muhindi akijifunza kingereza ambayo siyo lugha yake ya kwanza anaweza kuongea vizuri, lakini sisi waswahili tukijifunza kingereza iko shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana Wizara ya Elimu waangalie approach mpya ya kufundisha lugha ya kingereza na mwisho na kabisa niombe Wizara ya Elimu maombi matatu. Moja chuo kikuu cha Mwalimu Nyerere pale Serengeti eneo lipo, naomba mtukumbuke katika ujenzi wa benchi pia shule ya msingi na ufundi Mgumu tunaomba mtukumbuke, iweze kuboreshwa katika mpango wenu na mwisho tunaomba sekondari mpya ufundi pale Serengeti na ikikupendeza tuijenge katika kijiji cha Mesaga kule Ngolemi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)