Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii ya kuweza kuchangia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nimshukuru sana Rais wetu kwa jinsi anavyopambana katika sekta hii ya elimu. Mama anajitahidi ametupa fedha nyingi na amejenga madarasa mengi pia. Lakini vilevile nimshukuru Waziri wa elimu pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri ambazo anazifanya, kweli wanapambana na wanaleta maendeleo katika elimu. Nimshukuru pia Katibu wa Elimu pamoja na Manaibu wake kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nasema nishukuru kwa sasa, katika Mkoa wa Simiyu Wilaya ya Meatu tumepata fedha kwa ajili ya kujenga VETA, kwa hiyo nashukuru sana. Mwaka jana nilisimama hapa kuchangia nikaomba hivyo Waziri umetekeleza; wakazi wa Wilaya ya Meatu tunashukuru sana. Lakini vile vile tunashukuru kwa fedha mlizopeleka. Mmepelekea milioni 228, lakini kazi ile ni ya bilioni tatu. Jitahidi sana Waziri kupeleka pesa kule ili yale majengo yajengwe kwa wakati na si kwamba VETA ijengwe kwa muda wa miaka mitano, haipendezi. Jitahidi fedha zile ziende na shughuli ziende vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kazi nzuri ambazo mnaendelea kuzifanya, mnaelimisha jamii, mnatoa fedha nyingi, tunapata madarasa na madawati pia. Lakini tukumbuke Watanzanjia tuna watoto wengi sana katika shule zetu. Pamoja na kupambana kujenga madarasa miundombinu lakini bado tuna upungufu mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongea juu ya walimu. Walimu kwa kweli wako katika mazingira ambayo ni magumu sana, lazima niwasemee. Walimu wanahangaika wanafanya kazi katika mazingira magumu. Niliona shule moja hapa, niliwasiliana na Mkuu, shule moja ambayo iko katika Wilaya ya Itilima ina watoto1,200 lakini ina walimu 11, just imagine, wale waaalimu wanafanyaje kazi jamani? Mwalimu afundishe kuanzia chekechea, akitoka chekechea ana kipindi cha darasa la kwanza, akitoka kipindi cha darasa la kwanza, ana kipindi cha darasa la tatu yule mwalimu kweli unamuandalia mazingira mazuri hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajikuta mwalimu anachoka, anaongea na wale watoto yaani ukiingia darasani katika Mkoa wetu wa Simiyu nisemee, darasa moja lenye wanafunzi wachache labda ni wanafunzi 125 au 130, mwalimu huyu mmoja. Sasa jiulize, darasa la kwanza mwalimu anaandika kengine kanamfinya; yaani mwalimu unamuweka katika mazingira ambayo ni magumu hata kazi yake anaona kwamba jamani nifanyeje. Lakini bado mwalimu yule anatoka mbali, umbali wa kilometa tisa mpaka kumi, mwalimu anaendesha baiskeli ama kabebwa kwa boda boda na kwa hela hiyo hiyo tunayoijua. Afike kule mwalimu amechoka, kanyeshewa mvua, yaani ni vitu vya ajabu. Mwalimu tena aingie darasani lakini akifika darasani na penyewe mwalimu anapata shida watoto ni wengi wengine wamekaa chini mwalimu anaandika wanamvuta sketi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usiombe kufundisha darasa la kwanza, na ndiyo maana walimu wengi huwa wanakimbia sana kufundisha darasa la kwanza la pili na la tatu, ni watoto amabo ni wasumbufu mno. Una watoto 140 mwalimu mmoja unafundishaje? Haya wengine wamekaa kwenye madawati, wengine chini, ni vurugu; kanakolia, kanafanya nini, unajikuta mwalimu hafanyi kazi katika mazingira yaliyo mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamesema habari ya private; private wanajitahidi kweli inabidi Wizara ya Elimu kujiuliza kwamba inakuwaje shule zetu za Serikali zinakuwa na walimu wachache kiasi hicho? na wale wanajitahidi wanakuwa na walimu wengi ambao wanakuwa na mgawanyo mzuri wa masomo, basi mwalimu hata kama amezidiwa namna gani awe na watoto 50; watoto 50 anaweza akajitahidi mwalimu akawafundisha. Mwalimu huyu unampa watoto 130 au 140 lakini atoe maswali 50 kwa kila somo, hasa darasa la saba na la sita, hivi hebu fanya 50 mara 120., atakuwa amesahihisha maswali mangapi? Yule mwalimu akitoka pale atakuwa na hali gani? Waziri wa Elimu naomba ajitahidi sana kwa hilo, atuletee Walimu wa kutosha katika Mkoa wa Simiyu ili tupunguze idadi ya wanafunzi wengi ambao hawaelewi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine napenda niseme, Serikali imefanya vizuri sana katika kuwapatia Walimu vishkwambi kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia. Tunashukuru kwa hilo Walimu amewasaidia, lakini kuna sababu ya Serikali isaidie upatikanaji wa wireless internet ili kurahisisha watoto na walimu kusoma kwa kutumia teknolojia mpya hii ya kisasa, Mwalimu asaidiwe. Niliwaona Walimu siku ya Mei Mosi walikuwa wakimwambia mama, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wanasema mama tumepewa vishkwambi tunavyo, lakini tunataka tufundishwe jinsi ya kuvitumia. Kwa hiyo, Profesa atumie muda wako apate timu ambayo itawasaidia Walimu ili waweze kufanya kazi katika njia iliyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni upungufu wa miundombinu kwa Walimu. Walimu wengi hawaishi shuleni, wanaishi mbali sana. Angalia mazingira ya kule kwetu, Mwalimu anatoka pale Bukundi anaenda Lukale Shule ya Msingi, ni mbali sana ni kama kilometa kumi na tatu, kumi na nne, anaendesha baiskeli, akifika kule Mwalimu amechoka hawezi kufanya kazi na bado mazingira yetu sisi ni magumu sana kule. Walimu wangepata nyumba, wangefanya kazi vizuri, wakae katika maeneo ya shule ili Mwalimu aweze kutekeleza majukumu yake vizuri. Naomba Waziri alichukue hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona Rais wetu amejitahidi amejenga madarasa mengi sana, basi uwepo na utaratibu wa kujenga nyumba za Walimu ili wakae katika maeneo ya shule, maeneo ya shughuli zao. Walimu wanaishi mbali sana, unakuta anatoka pale Mwanuzi Shule ya Msingi anaenda mbali, umbali wa kilometa kumi na mbili, kumi na tatu, hivyo, Mwalimu anafika amechoka hata ule ufundishaji wake unakuwa uko chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nataka niseme ni changamoto ya madarasa. Madarasa kweli Serikali imejitahidi kujenga, lakini bado kuna upungufu mkubwa. Walimu wanahangaika katika madarasa na watoto wengine wanasoma nje kwa sababu vile vyumba vya madarasa havitoshi. Serikali ilijitahidi kumweka Mwalimu katika mazingira mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande mwingine nataka kuzungumzia habari ya hawa watoto wenye mahitaji maalum, watoto hawa wanahangaika sana. Unakuta Mwalimu anafundisha hana darasa la watoto hao, anavamia hapa, yuko hapa, mara yuko nje. Basi Serikali ijitahidi ijenge madarasa maalum kwa wale watoto wenye mahitaji maalum ili nao wasome katika hali nzuri na wajisikie vizuri, pia hata Walimu wawe na mazingira mazuri ya kuwafundisha watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine Mheshimiwa Waziri nataka nishauri juu ya hawa watoto wa MEMKWA. Watoto wa MEMKWA ingependeza nao waandaliwe miundombinu yao, wawe na madarasa yao special kwa ajili ya kufundishiwa. Kwamba, hii ni MEMKWA wafundishwe, sio mpaka wasubiri watoto wengine wamalize, wamechelewa, anaingia Mwalimu akiwa amechelewa na ufundishaji wake unakuwa haujakaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho napenda niseme, Walimu wetu wanalalamika sana juu ya mafao yao, hasa wanapostaafu. Wanapostaafu inaonekana kwamba, Walimu tunawasahau na tunawatelekeza, lakini wamefanya kazi nzuri sana na kazi ya hali ya juu ya kuinua elimu ya nchi yetu ya Tanzania. Mwalimu anapostaafu pension yake inakuwa ni matatizo, wengi wanalia, kila siku napigiwa simu, tusaidie huko. Jamani Mwalimu anapokaribia kustaafu kabla hata ya miezi mitatu mwandalie pension yake, apewe hela yake yote aifanyie kazi yeye mwenyewe, sio aanze tena mizunguko ya kuja Dodoma mara mbili, mara tatu, mara nne, hata hela hana, anakopa. Tunaomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hilo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuishukuru sana Serikali yangu kwa utendaji mzuri ambao unaendelea. Serikali imefanya vizuri sana kuwapatia Walimu hivyo vishkwambi, kama nilivyosema, lakini hapa kuna message nyingi, wanasema, mwambie Waziri ajitahidi tuelewe vizuri kuvitumia vile vishkwambi. Kwa hiyo, wengi hawaelewi. Waziri apate muda, atafute timu yake, iwafundishe Walimu ili waweze kuvitumia vizuri vile vishkwambi na viwe msaada kwao wao na kwa wanafunzi ambao wanawafundisha, litakuwa ni jambo jema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Napenda niunge mkono hoja. (Makofi)