Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hii Wizara ya Elimu. Kwanza kabisa nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa namna ambavyo amenipa afya njema nimeweza kupata nguvu ya kusimama, kuchangia wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa namna ambavyo inafanya kazi vizuri ya kuboresha mambo ya elimu kwenye nchi yetu hii ya Tanzania. Mheshimiwa Rais, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, anafanya kazi nzuri amekuwa akitenga fedha nyingi sana kwa ajili ya elimu na mambo mengine mbali mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ninaomba kabla sijaanza kuchangia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Mkenda pamoja na Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watumishi wote, wanafanya vizuri sana kusimamia elimu kuhakikisha inakwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kubwa sana kwenye shule za msingi. Shule za msingi zipo lakini ni kama tumezisahau kidogo, shule za msingi madarasa yamekuwa ni machakavu kwelikweli. Madarasa ni machakavu halafu wakati huo huo wanaweza yakawa hayatoshelezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano pale Wilaya ya Rungwe, Kiwila kuna shule ya Mpandapanda ile shule ina wanafunzi jumla ya 1,380 ina vyumba vya madarasa saba kiasi kwamba darasa moja wanakaa wanafunzi 197 hiyo inapelekea shida kweli kweli namna gani ya kukaa wakiwa madarasani ili watoto waweze kuelewa wanavyofundishwa na walimu. Msongamano huo ni mkubwa sana, wakati huo huo kuna shule ambazo zina hali mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Wilaya ya Kyela kuna shule moja ya msingi inaitwa Makwale ina hali mbaya sana. Lakini wakati fulani hata ofisi zinakosena, wanachukua darasa wanaweka kama ndiyo ofisi, ambapo inaendelea kupungu zaidi idadi ya madarasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiomba Serikali, naomba itizame kwa upya, maana elimu ya msingi ina matter sana kwa sababu bila msingi hawajafika watoto sekondari, hawajafika chuo, hawajafika maprofesa wanakuwa hawapo wala madaktari bila shule ya msingi. Kwa hiyo, nilikuwa napenda kushauri Serikali shule za msingi hizi tuzitazame ziboreshwe, ziwe mkazo wa kuboreshwa kwa sababu elimu yote inaanzia huku chini ndipo madarasa na vidatu vingine vinaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba nishauri Serikali pia, nishauri Serikali kwa upande wa wahasibu. Ninaipongeza Serikali imeweka wahasibu lakini kwenye shule zile kongwe Sekondari ya Rungwe, Iyunga Sekondari, Loleza kuna wahasibu kule na zingine nyingi tu ambazo zina wahasibu. Hizi shule zetu za kata za sekondari zilizo nyingi hazina wahasibu, anateuliwa mmoja wa walimu kwa ajili ya kwenda kufuatilia fedha kwenye halmashauri na mifumo inakuwa inasumbua, anaweza akaenda kwa siku nne mfululizo na mwalimu yule ana vipindi darasani anatakiwa afundishe kwa hiyo, watoto wanakosa vipindi. Kwa sababu mwalimu anaenda kufatilizia mambo ya kiuhasibu kwenye halmashauri na si kwamba halmashauri wanafanya makusudi, hapana ni kwa sababu mifumo inakuwa inasumbua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi nilikuwa natamani serikali kama itaona inafaa basi watafutwe ama waajiriwe wahasibu siyo kwa kila shule, anaweza akawa muhasibu mmoja, ambaye anaweza akawa ana shughulikia shule tano mambo ya kifedha nadhani hilo litatusaidia kuiweka elimu yetu katika utaratibu mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifano ipo hai kabisa, mtu anatoka Kata ya Nzovwe kule Mbeya Jiji au Iziwa nauli ni zaidi ya shilingi 5,000 anakwenda mjini Mbeya Jiji pale kwa ajili ya huduma. Mfumo umegoma basi anarudi kama alivyo kesho hivyo hivyo lakini bado mambo yanakwama kwa sababu vipindi ambavyo alitakiwa afundishe watoto wale wanakwama kupata masomo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuchangia kwenye upande wa vyuo. Serikali inafanya vizuri sana kule Mbeya, Wilaya Rugwe tumebarikiwa, tuna vyuo viwili vya walimu, kuna chuo cha Mpuguso. Chuo cha Mpuguso Serikali imekitizama kwa jicho zuri, imefanya vizuri kwa maana imeboresha majengo lakini pia imeongeza mabweni lakini iliweka lami pia japo kwa sehemu lakini kuna changamoto. Chuo cha Mpuguso cha Ualimu kina wanachuo 670, wapishi wapo wawili, kiuhalisia walitakiwa wapishi wawe watano mpaka sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hicho ni chuo cha Mpuguso nakisema kwa mfano halisia si mfano ni halisia ya hao watumishi hawapo ila na vyuo vingine yamkini vina mapungufu kama haya. Kwa hiyo, nilitamani sana kuhusu upande wa vyuo Serikali itizame watumishi namna ambavyo wapo na wanatakiwa kufanyaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia chuo hicho kina wakufunzi wa sayansi wawili tu. Kiuhalisia walitakiwa wakufunzi wawe wanne kwa hivyo chuo kina upungufu wa wawakufunzi hao ninaomba sana Serikali itizame upungufu huo wa wawakufunzi kwenye vyuo, ili iweke uhalisia na mambo mengine yaweze kwenda sawa sawa na vile mpango unavyoenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mazuri Serikali inavyofanya uchakavu wa nyumba za watumishi. Kuna nyumba za watumishi lakini ni chakavu sana. Hivyo basi, nilikuwa naomba sana Serikali itazame hili namna ya kuboresha, kufanyia ukarabati nyumba za watumishi. Lakini pia bado azitoshelezi kuna uhaba, kuna uhaba wa nyumba za watumishi pale Chuo cha Walimu Mpuguso. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali namna ambavyo imeweka vyuo vya VETA. Haijatusahau hata pale Iyunga kuna chuo cha VETA lakini pia kuna Sekondari ya Iyunga, Sekondari ya Iyunga ni sekondari ya muda mrefu sana ni ya tangu mwaka 1925 lakini miundombinu yake si rafiki sana kwa sababu haijafanyiwa ukarabati. Najua hili ninaweza kwenda moja kwa moja TAMISEMI lakini kwa sababu tunaongelea mambo ya elimu na pale ni elimu inapatikana ya sekondari. Ninaomba sana, sana muiangalie shule ya sekondari ya Iyunga ambayo ni shule bora sana kati ya shule nyingi ambazo ziko vizuri. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Suma, kengele imeisha lia.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja hii ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante kwa kunipa nafasi ya kuongea. (Makofi)