Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Hotuba ya Wizara ya Elimu. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwani wizara hii tayari imeishapokea asilimia 70.2 ya bajeti kufanya kubakia asilimia 29.8 ambapo kimsingi tunaamini mpaka mwisho wa bajeti hii tunayoenda nayo mtakuwa mmeishakamilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pia niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwani bajeti ya sekta ya elimu imeongezeka kwa asilimia 18 sisi wote tumekuwa mashuhuda fedha takribani bilioni 300 ambazo zimeenda kwenye miundombinu ya ujenzi wa madarasa ya UVIKO hivyo kufanya kupata madarasa 12,000 tunawapongeza sana kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia ubora wa elimu na tunapozungumzia ubora wa elimu Mheshimiwa Waziri penda usipende, taka usitake lazima tutalizungumzia ama utalisikia suala zima la upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari ambayo takribani ni 160,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Husna, amesema hapa kwamba suala zima la walimu wa kujitolea kwamba majibu ambayo umetujibu ndani ya Bunge ni kwamba hakuna miongozo. Swali lingine ambalo Mheshimiwa Waziri, nikuulize inatohali nini? Au inatutaka nini kuweza kupata hii miongozo kama suala la miongozo tunaamini kwamba walimu wa kujitolea ni kweli linasaidia watoto wetu, linasaidia wanafunzi wetu sasa kwa nini msilete hiyo miongozo? Ama kwanini msitoe hiyo miongozo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Waziri hapa ulipokaa unafahamu kwamba kwenye shule zetu walimu wa kujitolea wapo, wanapeleka maombi, walimu wakuu wanawapokea na wanalipwa posho na inategemea Serikali za vijiji. Serikali za vijiji ambazo zina mapato mazuri ndiyo hawa wanatoa fedha kulipa posho walimu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakati tunasubiri mpango wa muda mrefu kuhakikisha walimu laki tatu wote tuweze kuajiri siyo jambo la miaka miwili, miaka mitatu inatuchukua hata miaka mitano hata miaka sita. Kwa hiyo, wakati tunasubiri kwenda kwenye jambo la muda mrefu, embu tuje namkakati wa muda mfupi, tuje na jambo la muda mfupi kama tutafanya ile ya kuingia mikataba sawa, kama tutaendelea hili la kusema kwamba Serikali za vijiji lakini mwisho wa siku ni vijiji vingapi vyenye uwezo? Hili kama tunalibariki bado linatakiwa kuja huko wizarani. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, kama sote tunakubali walimu wanaojitolea ni msaada kwa wanafunzi wetu. Kwa hiyo, hatuwezi kuzungumzia ubora wa elimu kama hatuna walimu, hatuna madarasa, hatuna matundu ya vyoo, hatuna madawati, hatuna nyumba za walimu. Kwa hiyo, suala zima la ubora wa elimu ni lazima tuangalie miundombinu lakini pamoja na walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo mbali na hilo suala zima la elimu msingi ni lazima Sera itamke wazi wazi kwamba elimu ya msingi ianzie elimu ya awali. Suala hilo Mheshimiwa Waziri, nakusikiliza na nakufatilia sana huwa unalitamka kwamba elimu ya awali na yenyewe ni elimu msingi. Lakini tukija kwenye Sera aijitabanaishi, haijasemwa popote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, elimu ya awali ni iwe elimu ya lazima. Kwa sababu hali ilivyo sasa ni kwamba wengine wanaona ni lazima lakini wengine wanafanya hiyari, na ndiyo hii sasa unakuta katika shule zetu masomo ya kujifunza wakati kwenye shule ya awali a for apple b for ball and c for chair. Watoto wa private wanajifunza kwenye shule za awali lakini watoto wetu sisi wa Serikali wanaenda kujifunza kwenye shule za msingi na ndiyo matokeo yake wakimaliza darasa la saba kwenye mitihani wanaandika mazombi hawajui kuandika majina yao, wakimaliza hawajui kusoma na kuandika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati umefika wa elimu ya awali kuwa elimu ya lazima ili tuweze kuwa na msawazo mzuri kati ya vijijini pamoja na mijini na isiwe kwamba kwa ambae anaejisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka kulizungumzia kwamba tunapo zungumzia ubora wa elimu na tuna zungumza suala zima la udhibiti wa ubora wa shule. Sasa tunao mradi mzuri, niwapongezeni kwa huu mradi wa strengthen school quality assurance. Mheshimiwa Waziri umeutengea takribani bilioni moja lakini mpaka tunavyo zungumza mwezi Februari hakuna hata senti kipande ambayo imeenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi una nia njema, una nia nzuri ya kuweza kusaidia suala zima tunaloliita ubora wa elimu. Tunakuomba kwenye kipindi kilichobaki hebu wapeni fedha ili waanze na mchakato wa huu mradi wa strengthen school quality assurance. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamesema watu hapa wadhibiti ubora kwamba wadhibiti ubora tunataka kuwalinganisha na CAG katika masuala mazima ya elimu. Sote tunafahamu kazi nzuri inayofanywa na CAG katika masuala ya fedha lakini kama tunasema wadhibiti ubora ndiyo CAG kwa upande wa walimu. Mheshimiwa Waziri muda umefika sasa wadhibiti ubora kuwaanzishia ama kuanzisha taasisi ya udhibiti ubora, wasiishie kuwa kwenye kurugenzi ama kwenye idara kwa sababu kazi wanayoifanya ndio tunataka kusaidia watoto wetu..

Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia inaenda kasi sana, mambo yanaenda kasi sana. Kwa hiyo kama hatutakuwa na elimu iliyokuwa bora kwa watoto wetu, tutashindwa Kwenda kushindana huko duniani. Kwa hiyo muda umefika wa kuanzisha taasisi ya udhibiti ubora, muwapatie bajeti yao, muwapatie vote ya kwao ili waweze kufanya kazi bora na nzuri ya elimu hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nakushukuru sana, kubwa la kwangu nililokuwa nataka kulizungumzia ni hilo. Ifike mahala tuwe na elimu iliyokuwa bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)