Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba na mimi nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri, na niseme tu tangu mwanzo kwamba mimi naunga mkono hoja. Lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ameendelea kuifanya elimu kuwa kipaumbele kikubwa kwenye nchi, na hili tunaliona kwenye bajeti. Kwa mujibu wa bajeti ambayo tunayo takribani asilimia 17 imewekwa kwenye elimu, na haya ni maamuzi sahihi, na hakuna sehemu ambapo watu waliwahi kula hasara kwa kugharamikia elimu, kwa hiyo napongeza sana Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza kwanza kwa kumkumbusha Mheshimiwa Waziri kwamba pale Geita Mjini tuna Chuo cha VETA na kile Chuo cha VETA pamoja na kusua sua kwake kimefikia level ambayo naamini sasa tunaweza kuwa tayari kukifungua angalau tukaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tu kumtaarifu mapema Mheshimiwa Waziri kwamba nimeunga mkono bajeti yake, lakini natamani kuona kwenye bajeti hii sasa ameweka mahitaji yote ya lazima ili kile chuo kiweze kuanza.
Tunahitaji walimu , vifaa na miundombinu mingine. Namna yalivyo sasa majengo yale yataanza kuharibika kabla hayajaanza kufanya kazi. Kwa hiyo nimesema naunga mkono hoja lakini namtahadharisha Mheshimiwa Waziri kwamba natamani kuona kwenye bajeti hii sasa chuo changu kinaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili Kamati imesema vizuri kwamba tuna upungufu mkubwa sana wa walimu ; na jambo hili liko kwenye Halmashauri yangu. Mimi nina upungufu mkubwa wa walimu takribani walimu 500. Naipongeza sana Serikali imekuwa ikitupa walimu wachache; na hivi karibuni Mheshimiwa Waziri ametuma vishikwambi tunakushukuru sana kwa vishikwambi, amepelekea walimu .
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka anieleweshe vizuri; vishikwambi kama vilivyo havitawasaidia kama kwenye bajeti yake hatutaona ametenga fedha kwa ajili ya bundle kwa sababu watabaki na madude ambayo hayana kazi. Lakini nataka kujua sasa vitasaidiaje kupunguza upungufu wa vitabu? kwa mfano hata kishikwambi kimoja kikiwa kwenye shule kama kuna mfumo wa kuhamisha kufanya kishikwambi kuwa resource center na kuhamisha materials sasa kuyafanya yaweze kupatikana kwenye shule nzima ni jambo jepesi. Lakini shule zetu nyingi hazina printer, copier na umeme. Nataka kuona huo makakti vishikwambi hivi viweze kutumiaka vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu tuzungumzie habari ya mikopo. Naiomba Serikali, katika maeneo ambapo tumeendelea kufanya vizuri; tumeongeza fedha mwaka jana na nimeona mwaka huu pia wameongeza fedha kidogo kwenye mikopo lakini bado hatujatosheleza. Naiomba Serikali kapo kakundi kadogo sana ka walemavu, ambako kanahitaji tu kawekewe fungu maalumu, hata 1% au 2% ambao wanateseka sana. Ni moja ya kundi ambalo haliwezi kuhangaikia mikopo kama wanavyohangaikia watu wengine. Kwa hiyo kakundi hhiki kiwekewe kiwango maalumu kwamba aina yoyote ya mlemavu anapofanikiwa kwenda university habari ya mkopo kwake iwe granted, na jambo hili ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza NMB kwa kuja na package ya mikopo kwa ajili ya kukopesha wanafunzi. Shida yangu pale ni moja tu collateral ni nini? Huyu mwanafunzi collateral yake ni registration anaipata chuo kikuu? Nimeona, marejesho yake ni kama commercial, ni kama ya kibishara. Asilimia tisa ni hela nyingi sana kwa mtu ambaye hana uwezo wa kujisomesha.
Mheshimwia Mwenyekiti. kwanza registration iwe ni collateral number one, lakini cheti chake kiwe ndicho guarantee ya kumfanya huyu mtu aweze kuaminika. Familia nyingi hazina uwezo wa ku-service huu mkopo na riba ya asilimia tisa kwa mwanafunzi ambaye ameshindwa kujisomesha. Tunawapongeza sana kwa kuja na hiyo package, lakini bado naamini kwamba kuna haja ya kuapanua na kuona huyu anapopata udhamini peke yake iweze kumsaidia kwenda chuo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakwenda kwenye mambo yangu mawili ambayo nilitaka kusema. La kwanza, pamekuwa na double standard ya maelekezo kwenye ofisi ya Mheshimiwa Waziri. Unakuja waraka wa elimu. Kwa mfano kuna waraka wa elimu ambao umetoa maelekezo ya kuondoa darasa la kwanza mpaka darasa la nne kwenye bweni, na watoto wa bweni waanzie darasa la tano mpaka la saba. Mimi nataka Serikali inaisaidie; tunazo shule tayari ambazo zimefanya investment hii zaidi ya miaka 20 huko nyuma, na tuliwapa wenyewe leseni tukazisajili. Sasa tunapoleta waraka unaoanza sasa kuzuia tunafanya mambo gani? Maana yake tunazuia wale wasiandikishe watoto au tunawaambia wawekezaji wapya kwamba tunasheria double standard kwenye nchi moja kwamba ukienda shule B utakuta watoto wapo, ukienda shule C utakuta watoto hawapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa mimi kwa maoni yangu Wizara itafute namna ambavyo itatoa waraka ambao utafanana kwenye usimamizi maeneo yote. Hata hawa wasimamizi wadhibiti ubora tutawapa kazi kubwa. Akienda kwenye shule A anakuta criteria tofauti, akienda kwenye shule B anakuta criteria ni tofauti, na wazazi pia tunawachanganya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme jambo moja hapa; hakuna mtu aliyechagua, anayechagua kwenda kwenye shule ya gharama kubwa wala anayechagua kupeleka watoto bweni. Wako watoto wako kwenye bweni si kwa sababu wazazi wanapenda. Kuna mtumishi anaajiriwa leo, mke wake anaajiriwa Dodoma, baba anaajiriwa Lindi. Anakopelekwa baba hakuna shule, anakobaki mama nafanya kazi asubuhi mpaka saa kumi, solution ni kumpeleka mtoto bweni, kwa hiyo hawa wanapeleka mtoto bweni si kwa kupenda. Ninaiomba sana Wizara iliangalie jambo hili kwa mapana yake, isilichukulie jambo hili kama jambo ambalo watu wanaopeleka watoto kwenye shule za bweni wanapeleka kwa kupenda. Wengi wanapeleka kwa sababu mazingira ya malezi yanawalazimisha kutokuacha watoto na house boy ama na house girl, na matokeo yake Watoto hawa ni bora uwapeleke shule ambako unaweza kuwa na uhakika angalau na asilimia chache ya malezi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuwepo na utaratibu ambao ni uniform; tusije na utaratibu ambao unaanza kubagua sasa, watu waliowekeza mpaka miaka fulani wana masharti tofauti na wengine wanaokuja wana masharti tofauti. Hii itatuharibia sana kwa sababu inatuletea double standard kwenye eneo moja ambalo mimi naamini linahitaji kusimamiwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na jambo ambalo ni la msingi kabisa katika maeneo haya, tunaamini kwamba, watu wote, hata kwenye shule za Serikali ambazo tunazo, kipimo kikubwa ni kuona kwamba wanafunzi na watoto tunaowapeleka wanapata elimu kwa mujibu wa mwongozo, sera na sheria za Serikali. Kinachoendelea sasa hivi ni kama vile kuna ushindani, sasa kunakuja ushindani, kwamba wanaotoa elimu binafsi ni washindani wa Serikali, lakini mimi Mheshimiwa Waziri nataka kusema hawa sio competitor wako shule binafsi ni partiners kwenye hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuikumbusha Serikali kwamba siku ikitokea shule zote za msingi za watu binafsi zikafungwa au ikatokea shule zote za Serikali zikafungwa mzigo huu mkubwa ambao umebebwa na wawekezaji binafsi utachukua miaka mingine 10 au 15 kufikia kwenye level ambayo tunayo sasa ya utoaji wa elimu Serikalini. Tuwachukulie hawa kama wenzetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alizungumza hapa mzungumzaji mmoja jana kwamba, kwenye elimu ya sekondari na shule za msingi kuna kodi nyingi sana kiasi kwamba zingine zinakatisha tamaa wawekezaji wakifikiri kwamba tunawakomoa; lakini kimsingi jambo hili lilipaswa kubebwa na Serikali kwa sababu huu ni mzigo wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananfunzi zaidi ya 200,000 ambao wako kwenye shule binafsi wakirudi ghafla Serikalini, iko miji ambayo haina maeneo ya kujenga shule. Nataka tu nitoe mfano, mimi nina shule yangu moja ya msingi inaitwa Mbugani ina watoto 4,500. Katika eneo lile tukisema tunafunga shule binafsi, tukaongeza watafika watoto 6,000; hakuna sehemu ambapo tutawapeleka hawa watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ninaiomba Serikali, kutokana na upungufu wa walimu kuna michango mingi sana kwenye shule zetu huko chini. Kuna maeneo ambapo shule zinaamua kupeleka watoto kwenye kambi gharama zinakuwa kubwa. Kwa hiyo michango ile tuliyoifuta mwanzo imerudi kwa style kwa sababu ya ku-cover upungufu wa walimu. Sasa niombe itoe mwongozo ambao kama tumeruhusu kuajiriwa kwa mikataba, utolewe mwongozo na namna gani ya kufanya ili wazazi waweze kupunguziwa mzigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)