Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Rehema Juma Migilla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia kwenye Wizara yetu ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Utukufu wake. Pia ninapenda kumshukuru Rais wetu kipenzi, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa dhamira yake ya dhati kabisa kuhakikisha elimu ya Tanzania inakuwa bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kumshukuru pia Kaka yangu, Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda, Kaka yangu, Mheshimiwa Omari Kipanga na dada yangu makini sana, Profesa Carolyne Nombo, kwa kazi nzuri sana ambayo mnaifanya katika Wizara ya Elimu. Tunaona Wizara ya Elimu sasa hivi ina mafanikio makubwa sana ambayo yanakwenda kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta yetu ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kuna kuongezeka kwa bajeti ya Wizara ya elimu, tunaona walimu wetu wamepewa vishkwambi, tumeona wanafunzi zaidi ya 1,967 walikuwa wamekwama wameweza kurudishwa shuleni, tumeona pia kuna wanafunzi 593 wote hawa wameweza kupata Samia Scholarship. Mwenyezi Mungu awabariki sana muendelee kuwatumikia Watanzania kwenye suala la elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya mafanikio makubwa tuliyoyapata kwenye sekta yetu ya elimu, ninaona bado kuna changamoto mahali fulani. Suala la kwanza ni uboreshwaji wa maslahi ya walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mwalimu kabisa. Tunapokwenda kwenye suala la uboreshaji wa mitaala na sera, suala hili haliwezi kukamilika vizuri bila kuhakikisha maslahi ya walimu yanakamilishwa na kutekelzwa. Sasa hivi walimu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, hawana nyumba za kukaa, mishahara midogo, madeni mengi, huku wanafundisha wamerundikana darasani watoto kibao, kiasi kwamba ukiwapima sasa hivi afya za akili walimu wetu haziko sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaitaka Serikali kuhakikisha kwamba tunapokwenda kutimiza hii sera na mitaala ya elimu tuhakikishe walimu wanaboreshewa maslahi yao, bila hivi tutakuwa tunapiga mark time. Suala lingine ni kuhakikisha kabisa hao walimu wanapewa mafunzo. Sasa hivi walimu wanapewa mafunzo pale tu Serikali inapotaka, tena kuna wengine yaani kuisikia semina mpaka afanye lobbying, wakati ni hitaji. Kuna walimu ambao wanataka kujiendeleza wenyewe, lakini hao walimu wanaojiendeleza wenyewe Serikali mnakwepa majukumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Halmashauri zetu mwalimu akitaka kwenda kujiendeleza inamwambia kabisa mpaka uingie kwenye mpango. Anasubiri kuingia kwenye mpango lakini huo mpango anakuja kupewa barua kwenda mafunzoni anaambiwa atajigharamia gharama za masomo tena iko bolded kabisa. Bado huyu mwalimu anapotoka kwenye masomo hathaminiwi, habadilishiwi muundo wake wa mshahara kwa wakati, na bado hata unapofika wakati wa kupanda daraja wakati yuko masomoni wenzake wakipanda daraja yeye hapandi daraja, eti kisa yuko masomoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamkatisha tamaa huyu mwalimu kujiendeleza, lakini bado ataona amepoteza muda wake bure, na ametumia gharama zake. Niombe Serikali tusikwepe hizi gharama. Naomba sana hizi Halmashauri zinaposema uko kwenye mpango, mpango huo ni pamoja na kumpa rushusa na kumsomesha kwa sababu ndiyo jukumu la mwajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu wadau wa elimu kuwekewa vikwazo vingi sana. Mheshimiwa Waziri Serikali ndiyo ina jukumu la kusimamia shughuli za elimu a hundred percent, lakini Serikali peke yake haitoshi, inabidi hao wadau wa elimu, hasa private sectors waweze kushirikishwa na wamekubali kujitoa lakini wanawekewa vikwazo vingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunaona shule za private zinafutiwa matokeo eti kisa tu wamefanya udanganyifu kwenye mitihani, labda niulize swali moja, anayetunga mtihani huu wa Taifa si ni NECTA? Ni Serikali huyo huyo, Msimamizi wa hii mitihani ni NECTA, anapeleka walimu wakasimamie mitihani. Siyo walimu peke yao, kuna TAKUKURU, mgambo, polisi, Usalama wa Taifa, wote hao wanasimamia huu mtihani. Bado anayekwenda kusahihisha ni huyuhyu NECTA. Halafu leo matokeo yanapotoka mnatangaza shule mmezifungia. Kabla ya kuzifungia jitafakarini huko ndani, nani anasababisha haya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wazazi tunachangia pesa nyingi sana, tunawekeza hela nyingi sana kwa watoto wetu mnatuumiza wazazi, lakini pia mnawaumiza watoto. Mbaya zaidi baadaye mnawapa mtihani wale watoto kwenye mazingira mengine wamekuja ku-perform tofauti na ile mwanzo, this is shame jamani. Tunawakatisha tamaa hawa wawekezaji, hebu tuache hii tabia, tuweke mazingira ambayo private sector watafanya kazi yao ya kuisaidia Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nimeoa eti tumeacha kutangaza matokeo, kuya-rank kwa sababu mazingira yako tofauti. Hivi wewe ukipeleka kwenye shule zako walimu wa kutosha, miundombinu ya kutosha na madarasa ya kutosha, wanafunzi watashindwa ku-perform? Wanafunzi wata-perform vizuri tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ninaomba hili suala la kutozi-rank hizi shule kwa kigezo hicho hapo hatufanyi sawa. Kwa sababu hii pamoja na kwamba ni huduma lakini kwenye sekta binafsi ni biashara. Tunaposema tunazi-promote hizi shule, kwani hakuna shule za Serikali ambazo zinachukua wanafunzi cream? hazipo? Zipo, zinachukua wanafunzi cream kabisa, mnaziita shule maalum, zinachukua wanafunzi cream.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado sasa hivi, kama alivyochangia Mheshimiwa Taska pale, kuna shule sasa hivi Halmashauri na zenyewe zinafanya biashara. Maana yake walimu wa Halmashauri wanalipwa mshahara na Serikali, wengine wanafundisha private schools, Serikali haifanyi biashara. Kama inafanya biashara basi hawa wanafunzi wetu na wenyewe tuwafanyie ranking.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niulize swali, hivi ingetokea shule kumi bora zikawa za Serikali, msingetangaza? Tuwe wakweli. Tunawakatisha moyo hawa wawekezaji wetu, wanaisaidia sana Serikali, lakini tunakuja na sababu ambazo wakati mwingine tusikwepe majukumu yetu, tutangaze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ni ushindani, shindaneni ili ajulikane bora ni yupi. Hauwezi kufanya biashara bila promotion, huu ndiyo ukweli. Wekezeni huko miundombinu iwe mizuri, walimu wawe wa kutosha, mtaona matokeo, hata hizi shule za private zitaji-phase out zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni vyuo vya VETA. Mheshimiwa Waziri nikupongeze sana, tumeona kuna ujenzi wa vyuo vipya vya VETA 29 na vyuo vingine 63 vinakwenda kujengwa, hongereni sana kwa huu ubunifu. Ndiyo tunataka sasa haya mageuzi tunayosema tunakwenda kuyafanya yafanyike huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ila tunachoomba sasa, VETA zilizopo, mfano VETA yangu mimi ya Ulyankulu ambayo inawakilisha Halmashauri ya Kaliua, kiukweli imechoka mno, imechakaa mno, haifai. Bado hata karakana hazitoshi. Kozi zinazotolewa kule zilishapitwa na wakati. Hebu tunaomba sasa kwenye hili, haya mageuzi ambayo tunakwenda kuyafanya tuweke kozi ambazo zinakwenda na soko la ajira. Leo kuna kozi ya udereva vijana wengi sana watashawishika kwenda huko, kuna kozi ya saluni, kozi ziko nyingi sana. Tumekazania kozi nyingine ambazo hazitoi ajira kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana walimu wapelekwe huko, kama chuo changu kikarabatiwe, na kilishawahi kutengewa pesa, milioni 638, zirudishwe huko vifanyiwe ukarabati, walimu mahiri waweze kupatikana ili waweze kuendana na soko la ajira. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni mikopo ya vyuo vya kati.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Migilla, kengele ya pili imegonga.

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)