Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya kuweza kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwanza kabisa, naomba nichukue nafasi hii kuendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuwa wazima. Kipekee sana, naomba niendelee kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa na namna alivyojipambanua katika Wizara ya Elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema vijana wa Tanzania tunamwelewa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunamaanisha, na tunaposema zaidi tunamwelewa katika Wizara ya Elimu, tunamwelewa sana; na tunaposema Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amejipambanua kwenye elimu, tunamaanisha kwamba ameyatafsiri maono yake kwa vitendo, huku akiamini kwamba, ili kuwawezesha vijana wa Tanzania, lazima tuwe tuna human capital na physical capital. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote ni mashahidi, Wabunge wa Majimbo hapa wamejinasibu sana, wamesema, katika maeneo mbalimbali ya majimbo shule nyingi zimejengwa, lakini siyo shule tu, hivi karibuni tumeiona Wizara ya Elimu imeendelea kufanya maboresho mapya ya mtaala wa elimu. Hiyo inaonesha jinsi gani Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sasa anataka Wizara ya Elimu iendelee kuonesha umahiri na ubora wa human capital. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema human capital, majengo yanajengwa, miradi ya elimu inatekelezwa, lakini hatuwezi kuiboresha elimu kama hatuna uwezo wa kuendeleza skills and knowledge kwa wanafunzi wetu wa kitanzania. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunawashukuru wenzetu wa Wizara ya Elimu, kwa sababu kwanza wameendelea kuwa wasikivu na pia tunawapongeza sana, wameendelea kutoa ushirikiano mzuri kwetu sisi Wabunge huku wakiamini kwamba sisi kwa pamoja lengo letu ni kuwasaidia vijana wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, pia nataka niseme kwa dhati ya moyo wangu, vijana wa Tanzania wamenituma niseme kwamba wanampongeza na kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Bodi ya Mikopo kwa kutuongezea kiasi kikubwa cha kujikimu kwa Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Rais amejipambanua na kuona kwamba sasa elimu yetu sasa ni sayansi na teknolojia. Hivi karibuni tumewaona wenzetu wa Wizara ya Elimu wameenda kutoa vishikwambi nchi nzima, na vishikwambi hivyo vimetolewa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Tunamshukuru sana na tunampongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja zangu leo zitajikita katika maeneo matatu. Jambo la kwanza nalotaka kulizungumza, Mheshimiwa Waziri sasa hivi tupo katika formulation ya mitaala. Katika mitaala hii, yako mambo mengi yamezungumzwa, lakini nilitamani sana, na ninajua kwamba katika mitaala hiyo kuna vitu vingi ambavyo vinaenda kuonekana kwamba ni maboresho na vitakuwa vipya. Naomba niwazungumzie walimu. Walimu wanatakiwa nao wapate skills na knowledge mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa Wizara ya Elimu hapa walituambia, na katika majibu ya msingi walikuwa wanajibu wakisema kwamba, wamepata kibali cha kuajiri walimu wapya. Nilikuwa naomba sana tuwazingatie na hata wale walimu walio katika site, tuwatengee fedha na bajeti ya kutosha ili nao wakapate mafunzo ya ziada waweze kuendana na mahitaji ya walimu ambao tunawataka katika maboresho ya mitaala yetu ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, pia kuna jambo, hili sikuliona sana kwenye Wizara ya Elimu tu, hata katika Wizara nyingine na sekta nyingine. Tunaposema promotion, tunamaanisha kwamba, kuwa- motivate wale ambao wanatoka stage moja kwenda stage nyingine. Kumekuwa na changamoto moja, wenzetu walimu wanapoomba vibali kutoka kwenye Wizara ya Elimu na Wizara nyingine tofauti, pengine mwalimu amemaliza shahada ya kwanza, ameomba kibali anakwenda kufanya shahada yake ya pili, lakini anaporudi kwenye kituo chake cha kazi kumekuwa kuna changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto inayojitokeza, hakuna aina yoyote ya promotion ambayo anaipata. Jambo hili limekuwa ni changamoto na linaweza kuwafanya wanafunzi wetu wengine wasizidi kwenda kujiongeza kwa sababu wanajua, anaporudi kwenye kituo chake cha kazi hakuna chochote kinachoenda kumwongezea yeye, na hakuna tofauti baina yake na yule aliyemwacha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Waziri wa Elimu na Wizara yetu ya Elimu tulichukue hili tulibebe na liwe kama ni promotion kwa wanafunzi wetu au wafanyakazi wetu ambao wanatoka katika maeneo ya kazi wanapoenda kusoma na wakirudi ili waweze kuwa kama wana motivation fulani kwa sababu wanajua, mimi nimemaliza Degree, nikienda kusoma Masters nikirudi, kuna kitu kidogo kinaweza kikawa kimeongezeka na hiyo inaweza ikawasaidia wengine ili kuweza kupata promotions. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza vizuri sana hapa bajeti ambayo ilikuwa inasomwa. Nilitarajia sana, kwa sababu mmoja wa Mbunge ambaye alikuwa anauliza maswali mengi kuhusiana na vyuo vya kati, nilikuwa ni mimi. Nilitarajia sana leo au jana ikisomwa bajeti hapa, tuone walau kuna kiasi cha fedha ambacho kimetengwa kwa ajili ya vijana wa vyuo vya kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza vyuo vya kati, hivi ndiyo vyuo ambavyo vinarejesha kwa haraka mikopo. Simaanishi kwamba vyuo vya juu wakipewa mikopo hawarejeshi kwa haraka, Hapana, lakini kwenye vyuo vya kati return yake inakuwa ni ya haraka, kwa sababu mwanafunzi anachoenda kukisoma ndicho kile anachoenda kukifanyia kazi katika eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye vyuo vya kati, huku ndiko tunapowapata vijana wanaojifundisha driving, ndiyo tunawapata vijana ambao wanajifundisha masuala mbalimbali, umeme na vitu vingine. Akitoka pale, mwanafunzi yule tunamtarajia aidha kwa kujiajiri mwenyewe au hata kwa kwenda kuajiriwa. Hata kama hakuweza kuajiriwa, atakuwa ana uwezo wa kujiajiri mwenyewe. Akiwa na uwezo wa kujiajiri mwenyewe, maana yake returns ya ule mkopo itakuwa ni ya haraka zaidi kuliko na wale wengine ambao wanasoma kwa ajili ya kuja kurudisha ile return baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, kama Wizara, hili tulichukue kwa uzito wake, na Wabunge bahati nzuri wamelipigia kelele sana humu ndani wakiomba kwamba hili jambo tulibebe na tuweze kuwasaidia wenzetu ili waweze kupata mikopo katika hivi vyuo vya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nataka nimalizie katika maslahi ya walimu. Maslahi ya Walimu bado hayaridhishi. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri hili mlichukue, na muwe na wivu na watendaji wenu wa Wizara ya Elimu. Hivi leo ikitangazwa kazi ya TRA na kazi ya Ualimu vijana wengi watafukuzia kazi ya TRA. Kwa nini wafukuzie kazi ya TRA wasifukuzie katika Wizara ya Elimu? Maana yake inaonesha bado masilahi ya walimu yapo duni, na yapo chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi walimu tunasema, kazi hii ya ualimu, malipo yake yapo kwa Mungu. Basi tunaomba walau kidogo wale walimu nao wapate moyo wa kuendelea kufundisha vizuri. Muda mwingine hapa unaweza ukasema mwalimu anafundisha shule mbili; leo yupo private, kesho yupo katika shule ya Serikali, ni kwa sababu bado masilahi yao ni madogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nawashukuru sana. (Makofi)