Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Momba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakuskuru kwa kunipatia nafsi. Kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Profesa Mkenda pamoja na timu yake, lakini pili ninaipongeza Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia kwa namna ambavyo ameendelea kuboresha miundombinu kwenye elimu yetu hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, naomba niwapongeze walimu wote nchini kwa ngazi mbalimbali, kuanzia kindergarten, shule za msingi, sekondari mpaka vyuo vikuu. Hatuwezi kusema wala kujivuna wasomi tulioko Tanzania hii bila kuwashukuru na kuwaheshimu walimu wetu, hata wale ambao wamestaafu kwa namna ambavyo walijitolea kuhakikisha tunaelimishwa.
Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa naomba nitumie nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru walimu ambao wako ndani ya Jimbo la Momba. Kwa nini ninawapongeza walimu waliopo ndani ya Jimbo la Momba? Jimbo la Momba tuna vijiji 72 na vitongoji 302; yako baadhi ya maeneo hatuna zahanati kwenye baadhi ya vijiji lakini walimu hawa wameendelea kufanya kazi kwa kujituma na kujitoa pamoja hata kama hakuna huduma za afya.
Mheshimiwa Spika, yapo maeneo ambayo kuna changamoto ya miundombinu ya barabara na kuna wakati mvua zikianza kunyesha njia haziwezi kupitika walimu wanaweza wakakaa zaidi ya miezi mitatu hawajaenda mjini, lakini walimu hawa wameendelea kufanya kazi kwa kujituma na kwa kujitoa.
Mheshimiwa Spika, ndani ya Jimbo la Momba vijiji 50 havina maji safi na salama lakini walimu hawa wameendelea kushirikiana kunywa maji na mifugo lakini wakiendelea kufundisha watoto wetu ndani ya jimbo la momba, wakiendelea kujitoa na kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, ndani ya Jimbo la Momba kuna maeneo hakuna umeme lakini walimu hawa wameendelea kujituma, yamkini wanaendelea kutumia vibatari mafuta ya taa na sola; kwa namna yoyote ile lakini wameendelea kuwa wazlendo kujitoa ndani ya jimbo la momba.
Mheshimiwa Spika, ombi langu nikuombe Profesa Mkenda, tutakapomaliza Bunge la Bajeti twende tukawatembelee walimu wa Jimbo la Momba, wanashida nyingi ambazo wanatamani mwalimu mwenzao uweze kujua. Kwa walimu wote wa Jimbo la Momba na wengine wote walioko vijijini ambao wanapitia changamoto lakini wanafundisha watoto kwa kujituma ninawapongeza wakiongozwa na DC wa wilaya yangu ambaye pia ni mwalimu.
Mheshimiwa Spika, ombi jingine, kwa kuwa sisi watu wa Momba tunalima kufuga na kuvuna, tunaomba tupate chuo ambacho kitafanana na shughuli zetu ambazo tunazifanya ili watoto wa Jimbo la Momba watakapotaka kusoma whether wajifunze kulima katika ubora unaotakiwa kuvua katika ubora unaotakiwa na kufuga katika ubora unaotakiwa.
Mheshimiwa Spika, ombi lingine; Mkoa wa Songwe hatuna Chuo Kikuu chochote ambacho kinatoa digrii. Tunayo kampasi ya Dar es salaam Institute of Technology, ina mazingira mazuri na maeneo makubwa. Tunaomba kuanzia pale muwape hadhi waanze kutoa degree tupate chuo kikuu ndani ya Mkoa wa Songwe tukitumia Dar es salaam Institute of Technology.
Mheshimiwa Spika, ombi lingine, tunayo shule ya sekondari Songwe Girls ambayo tunasema ni shule ya mkoa; shule hii haina tofauti na shule ya kata, na mwanzilishi wa shule hii alikuwa ni Mheshimiwa Dkt. Samia Hassan Suluhu. Tunaomba tumpe heshima Mheshimiwa wetu kwa kuiwekea miundombinu bora shule ile ili watoto waendelee kupata elimu ndani ya Mkoa wa Songwe.
Mheshimiwa Spika, sina mashaka na ufanisi wa Wizara ya Mheshimiwa Mkenda, anafanya vizuri sana, anasimamia vizuri sana sera ambazo zimewekwa kwa utaratibu kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, mimi nataka kushauri mambo kadhaa. Inawezekana hata sasa hivi tunavyotaka kubadirisha elimu ni kweli tuko sahihi lakini kwa nini tunaona kumekuwa na uhitaji mkubwa sana wa kubadilisha mitaala yetu?
Mheshimiwa Spika, niseme kwamba teknolojia tuliyonayo ndiyo inatusukuma kutuvuta kutupeleka hapo. Serikali haina makosa yoyote kuona kwamba kuna baadhi ya ajira zinaondoka kwa vijana kwa sababu ya kuongezeka kwa teknolojia, lakini Serikali itakuja kufanya makosa kama haitataka ku-adopt hizi teknolojia kuziwekea mpangilio mzuri kwenye nchi yetu ili wananchi na Watanzania wasione kwamba artificial intelligent imechukua ajira zao bali tuione kwamba artificial intelligent tuitumie kama fursa ya kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanapata ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nikawa na wazo, nikaona Wizara ya Profesa Mkenda inaitwa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Mheshimiwa Nape inaitwa Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Mheshimiwa Spika, Profesa Mkenda huyu kwenye Wizara yake a-deal na mitihani ya darasa la nne, darasa la saba, form two, form four wapi, bado wanafunzi hawajagoma, bado hatujaomba tubadilishiwe elimu, bado Walimu hawajataka kuboreshewa mazingira yao; mambo kede kede kwenye Wizara hii. Ni wakati gani Profesa Mkenda atakuwa anahangaika na timu yake kujua kuna emerging technologies ambazo ziko duniani zinaweza zikawasaidia watanzania kujiajiri?
Mheshimiwa Spika, lakini ukiangalia Wizara ya Mheshimiwa Nape, Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari a-deal na wandishi wa Habari mikonge ya Habari, kule Momba kuna watu hawapati mawasiliano yote haya ni ya kwake saa ngapi tena atakumbuka na teknolojia ya Habari? teknolojia zinakuja kila wakati. Ushauri wangu kwa Serikali nilikuwa naomba yafuatayo;
Mheshimiwa Spika, kama itawapendeza, kama mtaona inafaa tupate Wizara mpya ya Teknolojia peke yake. Kipengele cha Mheshimiwa Profesa Mkenda kibaki Wizara ya Elimu na Sayansi, Teknolojia iondoke, kwenye Wizara ya Mheshimiwa Nape ibaki Wizara ya Habari na Mawasiliano, Teknolojia iondoke tupate Wizara ya Teknolojia. Ndani ya hiyo Wizara ya Teknolojia kuwe kuna taasisi zake. Kuwepo na taasisi ambayo itasimamia old technology kwa sababu bado ziko taasisi hapa nchini kwetu tunatumia teknolojia za kizamani. Pia iwepo taasisi ambayo itasimamia current technology ambayo tunatumia sasa hivi muda huu lakini kuwepo na taasisi ambayo itasimamia emerging technology na future technology ili Wizara hii ndio iweze kusambaza ujuzi mbalimbali kwenye Wizara ya Elimu, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Uvuvi na vitu mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa najiuliza, mfano leo mimi nimwalike Elon Musk aje hapa Tanzania nitampeleka kwenye Wizara ipi akapeleke ujuzi wake kwa ajili ya kujadiliana na Serikali yangu? Tunashindwa kujua, atakwenda kwa Mheshimiwa Mkenda kwa sababu ana teknolojia au ataenda kwa Mheshimiwa Nape kwa sababu ana teknolojia ya Habari?
Mheshimiwa Spika, tunaomba Serikali ichukulie teknolojia kama ni jambo la muhimu. Matajiri wote ambao tunawaongelea sasa hivi, mfano sasa hivi tunapomuongelea huyo Elon Musk ambaye anayo kampuni ya Spacex ambayo imefanya mambo makubwa kwa ajili ya kwenda huko angani, ni mwanateknolojia, ni mtu ambaye alizaliwa tu hapo Pretoria, South Africa, sasa hivi anaonekana ni mtu mashuhuri sana duniani. Aliununua mtandano wa twitter kwa zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 44 kwa ajili ya teknolojia tu. Tukimwangalia mtu kama Mark Zuckerberg, wote hao waliwekeza kwenye teknolojia, tukimwangalia mtu kama Bill Gates, wote hawa ni matajiri ambao walitokana na teknolojia.
Mheshimiwa Spika, tunabadilisha mtaala hii, ni kweli, lakini ninaona baada ya miaka kumi bado tutarudi hapa kuona kwamba bado mitaala yetu tuliyobadilisha haifanani. Ninasema hivyo kwa sababu gani, hatuwezi kushindana na teknolojia, tutakuwa tunajidanganya kushindana na teknolojia ni kama kushindana na muda.
Mheshimiwa Spika, ni kwa sababu naongea katika hali ya Kibunge, lakini nilitamani ningewaonyesha pia watu kwamba teknolojia hii namna ambavyo inashabihiana zaidi hata na mambo ya kiroho. Wanaosoma vizuri Biblia wataelewa vizuri sana vita ya Urusi na Ukraine nini kinaendelea. Sasa hivi benki zinavyofungwa ni mambo ambayo kwenye Biblia yameandikwa. Sasa sisi kwa nini tusiendane na huo wakati?
Mheshimiwa Spika, vijana wa Kitanzania wanaona hakuna ajira kabisa lakini kama tukiamua kutumia artificial intelligent in a positive way tunaweza tukapata ajira nyingi zadi ya ajira ambazo zilikuwa zimeandikwa kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Tunaweza tukapitiliza.
Mheshimiwa Spika, vijana wa Kitanzania wamekosa platform, wamekosa sera namna ya kuja kuonesha ujuzi wao. Wako vijana huko nje ni mahiri, ni wataalamu, wapeni nafasi, wapeni room, wajue wakija wata-fit kwenye taasisi ipi, wata- fit kwenye taasisi ya teknolojia ya zamani teknolojia ya sasa au teknolojia inayokuja? Vijana wa Kitanzania muwape nafasi waweze kutengeneza hata stimulation za teknolojia ambazo tunazitarajia. Zipo teknolojia za blockchain hatujazikumbatia, zinatoa ajira nyingi sana huko duniani. Sasa hivi kuna wakati unaweza ukaona benki zinabisha, hawataki kupokea digital currency. Mimi nataka uwaambia hivi wanajidanganya, watashindana na ukuta. Huko tunakoenda na majira yaliyopo na benki ambazo zinafungwa huko duniani, na kwa namna hali ilivyo tupende tusipende tunakuja na currency moja duniani; na tumeshaanza kuona wachumi wa dunia ambavyo Dola ya Marekani imeshaanza kuteteleka. Kwa hiyo niiombe Serikali…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Dakika moja, malizia Mheshimiwa.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, hatua ya kumalizia ni kumuomba Profesa Mkenda atakapokuwa pia anahitimisha kwenye hitimisho lake aseme kidogo ni namna gani ambavyo ametumia artificial intelligent kutengeneza ajira nyingi ambazo ziko kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ukiacha hizi ajira ambazo vijana wa kitanzania tunagawana…
SPIKA: Ahsante sana.