Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nianze kwa kupongeza Wizara na hasa Waziri Gwajima na Naibu wake angalau tunaanza kusikia wizara wanasema inawaka waka, kuna amsha amsha ndani ya wizara, hata hivyo ni bado muendelee.

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia hili suala sasa hivi limeota mizizi na hasa kwa wazazi ambao ni baba na walimu. Hawa walimu tuna wakabidhi watoto lakini sasa hivi limeibuka kweli hili wimbi walimu wakabidhiwa watoto ili wakawafundishe lakini imetokea walimu hao ndiyo wanawabaka watoto, walimu wana wabaka wanafunzi.

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi wa tatu mpaka wa nne kuna kesi sita za walimu wanawabaka wanafunzi, sasa wazazi wanajiwaza hivi hao watoto tunawapeleka wapi? Ukienda makanisani shida, misikitini shida hata shuleni. Kwa hiyo, suala la wazazi na hasa baba, baba mzazi wa mtoto kujiusisha kumbaka mtoto mpaka anampa mimba hili suala limekuwa ni zito sasa nini nataka kusema hapo?

Mheshimiwa Spika, ifikie wakati sasa na ndiyo maana Waziri wa Katiba alijibu hapa ilifikie wakati kama alivyosema Mheshimiwa Mwantumu, suala hili la ubakaji na ulawiti hawa watu wasipewe kabisa dhamana, hawa watu wasipewe dhamana waendelee kukaa ndani hata kama hizo kesi zinakaa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Hakimu wa Kilolo aliyemfunga yule mwanamme aliye mbaka mtoto wa dada yake kifungo cha Maisha. Lakini kifungo cha maisha hakitoshi yule alitakiwa anapoingia gerezani atandikwe viboko kumi na mbili halafu ndiyo aingie huko lakini kule bado mwili wake haujajeruhiwa ndiyo maana tunasema hawa watu wapewe adhabu kali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliwauliza baadhi ya Wabunge mistari kama mitatu hivi hapa nyuma nikasema hebu chagueni adhabu kati ya kunyongwa au kuasiwa? Wakasema afadhali kunyongwa sasa inamaana hao wanapenda sana waendelee kubaka au kulawiti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, chakufanya hapa bora hawa wahasiwe ile wanayoikataa ndiyo tuiweke huko, wakihasiwa hili janga litapungua na wale wa sheria hao mnapoenda kujadili mmeniahidi kwamba mtaleta mswada. Tunaomba mlete muswada wa sheria kali, sisi tunaogopa nini? Mbona wenzetu wanawanyonga kabisa ni aibu, ni aibu sana maana yake tunalisema, tunalisema lakini watu wanaendelea tu, kila siku unapata hizi kesi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hilo nimelisema kwa uchungu na tuanze na hawa walimu wanao lawiti watoto. Hawa ndiyo wawe mfano kwenye hizi adhabu kali, ni mwalimu lakini kwa hilo nasema tuanze na walimu na baba wazazi wanaofanya hicho kitendo leteni huo mswada haraka sana ili turekebishe hayo mambo, dhamana isiwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya sana wakitoka nje kama wamepewa dhamana wanaenda kushirikiana na ndugu hata wazazi wanakaa pamoja, kesi ile inafutika, tume ziwe zinaundwa kuchekiā€¦

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara, kuna taarifa, sijajua ni wapi?

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, inatoka hapa kwa Mheshimiwa Ramadhan.

SPIKA: Ahaa jirani yako. Mheshimiwa, haya kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ramadhan Ramadhan.

TAARIFA

MHE. RAMADHAN SULEIMAN. RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa kwa ruska yako mzungumzaji kabla ya mwaka 2018 Zanzibar kwenye Sheria yake ya Penal Code (Kanuni za Adhabu) makosa ambayo yalikuwa na dhamana yalikuwa matano tu.

Mheshimiwa Spika, baada ya 2018 tukafanya marekebisho ya sheria yakaongezwa kutoka matano mpaka kumi na moja kwenye Sheria za Mwenendo wa Adhabu (Criminal Procedure) za Zanzibar. Miongoni mwa makosa ambayo yaliwekwa yasiwe na dhamani ni makosa ambayo mchangiaji anayasema. Kwa kiasi kikubwa hii taarifa imsadie kwa kiasi kikubwa tumepunguza wimbi la makosa haya kwa sababu ya ukali wa washeria zetu zilizoko Zanzibar. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara, unapokea taarifa hiyo?

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, naipokea ahsante sana, ahsante sana Mheshimiwa Ramadhan. Sasa nilikuwa nasema kuna ndugu akienda kuambiwa huyo mtoto wako, tukae chini tulimalize hili wanakubali. Ndugu na wale watumishi na polisi wanaohusika katika kuhakikisha kwamba kesi hizi zinaishia huko mitaani nao waingizwe kwenye hiyo adhabu wafungwe maisha na wao wahasiwe pia tukifanya hivyo watajua hee sasa hivi hali mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije kwenye hili suala la elimu ya jamii, kwa kingereza wanaita sociology of education. Mambo yanayofundishwa au niseme haya mambo yanayaofundishwa kwenye sociology of education vyanzo vyake ili mtoto aelewe, apate hiyo elimu ya jamii, anaipata kwenye familia, anapata shuleni, anapata kwenye rika, anapata kwenye media, anapata kwenye NGO, anapata kwenye vyombo vya dini.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi, vyombo hivi, hivi vyanzo hivi vikitoa elimu potofu au vikitoa elimu mbaya inamuathiri mtoto kwenye jamii wakitoa elimu nzuri inamsadia mtoto kwenye jamii.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sasa hivi, katika hivi nilivyovitaja hivi vyanzo, media ikitoa kitu kibaya mnasikia hata Bunge tunakemea. Lakini leo hii naomba niliseme kwa faida ya watoto wetu. Kuna wakati mwingine elimu inayotolewa kwenye hizi dini zetu ni elimu ya uongo tunasika, vyombo vya dola wapo, Wizara ya elimu ipo, maendeleo ya jamii wapo. Watu wanafundishwa kwamba mtu unaenda mbinguni unaoana na Mungu. Watu wanafundishwa kwenye madhehebu kwamba humu ndani kuna mtu alikufa sasa hivi amefufuka yuko kwenye hiki chumba, kwa nini polisi wasiende kumtoa huyo mtu aliyekufa kwenye hicho chumba? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tunafundishwa vitu vya uongo watu wanavichukua na wakati mwingine mimi naona kama ni ujambazi na kupora fedha za watu. Suala hili tuliangalie; kutangaza elimu za uongo kwa kutumia madhehebu ya dini lazima Serikali tukae macho.

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu gani? haya yanayotokea nchi za jirani tukae chonjo, yanayotokea nchi za jirani yanaweza yakatokea hata Tanzania. Nasema tujipange, Wizara zinazohusika zihakikishe elimu zinazotolewa kwenye hivi vyanzo ziwe elimu za ukweli.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, naomba nimalize dakika mbili tu, please!

SPIKA: Dakika moja malizia.

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, dakika moja. Niwaombe Wizara hebu angalieni sheria ya jamii inasemaje kuhusu watoto wadogo wanaoajiriwa majumbani. Inasemaje sheria? Wanapataje haki zao au wanastahili kweli kuajiriwa wakiwa watoto wadogo? Na sheria za wafanyakazi wa majumbani bado. Ongea na Wizara ya Kazi na Ajira, mjipange muone kwamba hakuna unyanyasaji kwa watoto wanaoajiriwa wakiwa wadogo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.