Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Jang'ombe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALLY HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kutujaalia siku ya leo uzima kuja kujadili mambo yanayohusiana na bajeti ya Wizara hii ambayo inahusika zaidi na watu.
Mheshimiwa Spika, kwanza mimi nilikuwa niwaambie Waheshimiwa Wabunge wenzangu ambao waliotangulia hapa kuzungumza, naona hii group hii ya wanaume imeandamwa sana. Maana katika group hii members wengi kwanza walishame–left, sasa bado inakamatwa kwamba wapewe pombe wazidi kuleftishwa (to left) wengine watabakia wangapi? Members wengi walisha-left katika hili group jamani. Msiwe na wasiwasi sana kuna visukari huko mtaani.
Mheshimiwa Spika, mimi kwanza niipongeze sana Serikali na nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais katika makundi maalumu, hasa kwa kuwajali kundi hili ambalo linaloitwa wamachinga. Tumeanzisha sub vote ya wamachinga kwa ajili ya maendeleo ya wafanya biashara ndogondogo ambao tunaamini kwamba kwenye sub vote hii itakwenda kuwasaidia. Lakini pamoja na pongezi hizi za kuanzisha sub vote hii, mwaka uliopita tumepeleka bilioni 22 kwenye msimu huu ambao tunaumaliza, na safari hii tunapeleka bilioni 20 nyingine kwa ajili ya wamachinga. Kwa hiyo hii mimi ninawapongeza sana Serikali kwa kuliona kundi hili, hapo pokeeni pongezi Serikali.
Mheshimiwa Spika, katika wamachinga Mheshimiwa Waziri alieleza katika hotuba yake, anasema kwamba Wizara inakamilisha utaratibu wa kuzipokea bilioni 22. Sasa mimi najiuliza, kwa nini hapakuwa na uwazi katika fedha hizi za wamachinga, hizi bilioni 22? Mheshimiwa Waziri anajiandaa kuzipokea, fedha ambazo zilivyokuja zilikuja kama mkopo wa ECF. Mheshimiwa Mwigulu alituambia katika hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2022/2023, alisema hivi, kwenye paragraph ya 81, kwamba Serikali inatarajia kupokea fedha trilioni 2.5 ambayo kwa miezi 40. Lakini kwa bahati katika paragraph ya 85 ya Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti kuu 2022/2023 alisema kwamba bilioni 45 zitakwenda kuratibu mambo ya machinga pamoja na kupatiwa mikopo wamachinga waliojipanga vizuri.
Mheshimiwa Spika, sasa hotuba hii moja kwa moja ilipofika tarehe 18 Julai 2022, IMF wame-release hizo fedha kuja hapa Tanzania Julai 2022. Bunge lako kupitia Kamati zake likakaa, na lilivyokaa likapokea fedha hizi Kwenda kwenye sekta tofauti tofauti. Zimekwenda kwenye umeme, kilimo, mifugo, TASAF na nyingine hizi bilioni 22 ndizo zilikuwa zinakuja kwa wamachinga.
Mheshimiwa Spika, jambo la kushangaza ni kwamba hizo zote zimeonekana katika kitabu kikubwa hiki cha bajeti katika approved estimate, lakini hizi za wamachinga hazijaonekana. Sasa mimi najiuliza, kwa nini fedha hizi za wamachinga peke yake zisionekane? Fedha hizi bilioni 22 ukiziwekeza katika Benki ya Azania kwenye fixed deposit kwa miezi 11 unapata faida ya bilioni 2.3. Fedha hizi endapo mzingelikopeshwa kwa wakati kwa wamachinga, kwa sababu zinaitwa revolving, kwa hiyo zingelikuwa zinarudishwa anaanza kukopeshwa wengine.
Mheshimiwa Spika, lakini fedha hizi za wamachinga zingekuwa zimetolewa hiyo athari tunayoisikia huko Kariakoo kwamba kuna wamachinga wanachajiwa (be charged) ushuru wa store lengo lake ilikuwa wale wanaopewa bidhaa mkononi ili waweze na wao kwamba ziwe zimeshalipiwa kodi. Hii ni kwa sababu wanafanyabiashara wakubwa wanatumia ujanja kuwapa wale wadogo wadogo ambao wametandika vi-busati pale mbele na wanaokamata mkononi. Kwa hiyo athari hii nayo pia ingepungua.
Mheshimiwa Spika, cha kushangaza fedha hizi ziliingia mapema sio bajeti inayosubiriwa kukusanywa. Na malengo yake yalikuwa ndiyo hayo. Sasa najiuliza kwa nini kwamba sasa hivi ndio unafanyaika utaratibu. Mwezi wa 11 huu ndio unafanyika utaratibu wa kupokea hizo fedha. Utaratibu huo unafanyika sasa hivi, Serikali ilikuwa wapi muda wote huo? Maana ingelikuwa mimi ningeenda kuweka kwenye fixed deposit nikapata faida. Tunaambiwa sasa hivi, lakini fedha hizi zilikuja tokea mwezi wa saba, na kamati zako hizi ndizo zilizohusika kuzipokea fedha hizi za wamachinga.
Mheshimiwa Spika, sasa mimi nilikuwa naiuliza Serikali, kwa nini fedha hizi hapakuwa na uwazi? Kwa nini kwenye REA zimekwenda bilioni 100? Kwa nini TANESCO zimekwenda bilioni 100? Kwa nini kwenye kilimo zimekwenda? Kwa nini kwenye mifugo zimekwenda? Hizi zilikosa nini? Na fedha hizi zilipokelewa milioni 151.7 Dola za Kimarekani, na zilikuja mwezi wa Saba na zilifanyiwa utaratibu zikaenda kwenye vote hizo. Sasa mimi najiuliza hapa Serikali kwa nini wametufanyia kitu cha aina hii?
Mheshimiwa Spika, wanasema kwamba account haijafunguliwa kwa ajili ya kuwakopesha wamachinga, si kweli. Bilioni 6.8 zilikuwa zinahusika na other charges ambazo ni kuratibu, lakini milioni 680 zilikuwa zinahusika na ujenzi wa ofisi za wamachinga kwa kila mkoa ambazo zimo mule; na hizi Mheshimiwa Rais amepita akizisema anapokutana na wananchi, kwamba atajenga ofisi za wamachinga kila mkoa. Sasa huku uratibu gani unaotakiwa? Bilioni 15.5 ndizo zilikuwa ziwe revolving fund, na tarehe 7 Oktoba. Serikali ilileta kwenye Bunge lako hili kwamba tarahe 7 Oktoba, 2022 kwamba imeleta mchanganuo wa fedha hizi jinsi zitakavyotumika, na hiyo barua imekwenda Wizara ya Fedha na Wizara ya Fedha imekuja nayo Pamoja na Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalum. Sasa nashangaa fedha hizo zinatafutiwa utaratibu sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, hapa tunachezewa. Bunge hili tulipokea ceiling, Bunge hili tumepitisha bajeti. Ilitakiwa kuwe kuna media report. Media report ilisemaje? Kwa nini fedha hizi zisiingizwe? Media review kwa nini Bunge lako lisielezwe? Yaani tusijue, tunakuja kuja sasa hivi. Hata hiyo randama ambayo iko hapa sasa hivi ni kwa sababu ya mabadiliko, kwamba Serikali inataka kuji-defend. Sasa hizi fedha zimetumika lazima itakuwa ziko pahala ambako zimekaa.
Mheshimiwa Spika, mimi lengo langu, endapo Serikali haitakuwa na maelezo mazuri juu ya uwazi wa fedha hizi kama Bunge linavuyotaka na sheria ya bajeti inavyosema mimi naweza nikaja nikazuia shilingi ili Serikali itueleze tu; kwa sababu Hapana uwazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo jingine ambalo nilizungumze, katika makundi maalumu kuna kundi la wazee pale Zanzibar. Wazee ambao hawakuwa katika mfumo rasmi wa ajira wanapata pension, inayoitwa pension kwa wote. Kwa nini kwenye uchumi mkubwa kama huu wa Tanzania hatuwezi kuratibu hicho kitu cha pension kwa wote? Tuweke pension kwa wote. Hawa wazee ndio walioshughulika kututafutia sisi uhuru, lakini wengine kazi yao walikuwa wakulima, wengine wafugaji, lakini walizalisha. Tukumbuke kwenye vita vya Uganda vita vya mpakani vile watu walitoa mali zao ambao walikuwa si waajiriwa hawa na hii nchi imekuwa salama. Sasa niiombe Serikali au niishauri Serikali, tutengeneze huu mfumo wa pension kwa wote tuwasitiri wazee wetu. Hawa wazee wametulea tusiache wakaanza kupita wakaombaomba huko. Wakianza kuomba omba ni aibu na fedheha kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, nitaunga mkono hii hoja Serikali itakapotupa uwazi pamoja na sheria, kwa sababu kifungu namba 65 cha sheria ya bajeti utakapofanya uzembe kama huu kuna vitu pale vimetajwa.
Mheshimiwa Spika, nashukuru.