Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kipekee namshukuru Mungu na nakiri kwamba Mungu ni mwema kila wakati ndiyo maana tuko hapa wote kama ilivyompendeza yeye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme wazi kwamba nitazungumzia maeneo matatu tu na nitajikita katika hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Nashukuru kwamba kitabu hiki ni kizuri, kimeeleweka na sasa basi nataka kuzungumzia machache ili niendelee kuboresha maeneo aliyotuletea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na ule ukurasa wa 38 pale alipozungumzia Mfuko wa Afya ya Jamii (Community Health Fund). Mfuko huu ulianzishwa siku nyingi na ulianza pia wakati inaanza NHIF lakini hauko katika mfumo rasmi kama NHIF ambao uko kwa watu ambao wana ajira na wanapata mishahara yao kila leo. Kwa hiyo, NHIF utakatwa kwenye mshahara lakini hii CHF ni ya hiari. Inapokuwa hiari leo ukiwa nacho utatoa kesho huna hutoi. Bahati nzuri sana Serikali inajazilia mkitoa kumi Serikali inajazia kumi, mijini au manispaa inaitwa tele kwa tele huku kwingine inaitwa kujazilia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na nia nzuri ya Serikali mfuko huu umedumaa. Pamoja na takwimu tulizopewa hapa kwamba wanachama wameongezeka lakini kwa Tanzania nzima figure ni kidogo. Sasa nini kifanyike? Serikali ina nia nzuri kuwa na wananchi wenye afya nzuri kwa sababu Taifa lenye wananchi wenye afya nzuri ni Taifa zuri. Watu wanafanya kazi, watu hawaumwiumwi, hakuna wengi waliolazwa hospitalini na pale anapopata rufaa anakwenda kutibiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, shida ya CHF unakatwa au unakuwa na hiyo kadi unatibiwa katika eneo linalokuzunguka, pale pale katika kata labda sanasana wilaya, huwezi kwenda mbali. Inapokuja rufaa ile kadi haitumiki wakati NHIF unaweza ukatibiwa Tanzania nzima. Ombi langu la msisitizo Serikali ione sasa kuna kila sababu kuuongezea mfuko huo ili mtu akishakuwa na ile kadi ya CHF atibiwe kutoka wilayani mpaka mkoani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wetu hawajiwezi sana, mara nyingine kama mtu hana watoto basi inakuwa uwezo wake ni mdogo. Naomba hili lifikiriwe kwa mapana, Serikali haiwezi kupungukiwa kwa kiasi hicho. Siku za nyuma watu hawa walikuwa wanatibiwa bure leo imekuja lazima tuchangie na sasa tuko kwenye wakati wa mpito Serikali inataka iwe na ule mfuko wa jinsi ya kutibu kwa ujumla, naomba sana hili jambo lisimamiwe na liwezekane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema kilio changu cha CHF, kwa sababu naumia sana kwani wanawake wa Kilimanjaro wengi wangependa kujiunga lakini wamejiunga wachache kutokana labda na hali duni, wakati mwingine mazao hayatoshi au kipato ni kidogo na ninaamini hata huko kwa Wabunge wengine hali ni hiyo. Niseme wazi Wabunge tulio hapa ni wadau wakubwa wa mfuko huo kwa ajili ya watu wetu na hasa wale Wabunge wa Viti Maalum tunaweza kutumiwa kutoa hiyo elimu na siku zote tuungane kwa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hilo, naomba sasa nizungumzie jambo lingine ambalo ni ajira kwa vijana. Jambo hili limezungumzwa kwa muda mrefu, ajira kwa vijana, mimi najiuliza vijana wa wapi? Najiuliza mwenyewe vijana wa Tanzania walio wapi? Ni kina nani hao?
Wana ujuzi gani? Je, hii ajira mnayomfikiria anaitaka? Sasa leo ilivyokuja TAMISEMI nikajua hapa hapa jungu kuu, kwa sababu hakuna zaidi ya TAMISEMI. Halmashauri zetu ndizo zenye watu wote na vijana wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ufanyike utaratibu rasmi wa kutambua vijana ambao hawana ajira. Vijana hawa wakishatambuliwa tuwajue wako eneo fulani kama ni kata, kama ni wilaya wako vijana wangapi na wanataka ajira za aina gani? Suala hili linaweza likaonekana gumu lakini tuna vijana wetu wengi wanafanya research zao lakini hazifanyiwi kazi. Kuna vijana wengi ambao wako kwenye shule au kwenye vyuo lakini nao pia hawatumiki. Naomba sasa halmashauri ziwajue vijana ambao hawana kazi na watambulike rasmi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano kidogo tu. Hivi tulivyo hapa kuna vijana wanaandikishwa kwenda JKT unakuta wilaya nyingine wamepeleka maombi vijana 5,000 na wanatakiwa vijana 200 tu. Je, wale 4,800 wanakwenda wapi? Tuwatumie sasa wale vijana tuwajue hawa ndiyo kundi linalohitaji ajira na tuwaelekeze namna ambavyo watasaidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo ambayo hayatumiki mfululizo, mojawapo ni eneo la Nane Nane unakuta nyumba zipo, watu ambao wanakuweko pale au mashirika wakishatumia ile wiki ya Nane Nane nyumba zile zinafungwa sana sana zinakuwa ni maeneo matupu. Kwa nini sasa vijana kama wale tukishirikiana na hawa wadau ambao wana majengo huko Nane Nane, tusiwatumie kama majeshi yetu, kama ni wale wakulima, vijana wale wakafundishwa pale kwa muda hata wa mwaka mzima mpaka tena itakapofika Nane Nane na baadaye Serikali ikasaidia kuwapa kianzio? Mtu kusimama na kuweza kujitegemea au kusimama mwenyewe ni kitu kigumu. Ndiyo maana unakuta hata mstaafu anapofika wakati wa kustaafu anaomba kuongezewa muda kwa sababu hajasimama sembuse vijana wetu hawa wadogo? Naomba Serikali na sisi wenyewe tuwasaidie vijana hao wasimame wapate ajira na waweze kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ambalo nataka kulizungumzia ni hili eneo la biashara ndogo ndogo. Ni kweli tamko limetolewa kila mahali watambue maeneo ya kufanyia biashara na yapimwe. Hili ni jambo zuri na ningeomba kabisa hata hizo Halmashauri hivi sasa zilinganishwe au zipimwe kwa kigezo hicho kwamba ni Halmashauri gani zimeweza kutambua maeneo hayo au Halmashauri ngapi zimeweza kuweka hayo maeneo katika hali nzuri?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niseme jambo moja. Kuna zile biashara ndogo ndogo zaidi, biashara za babalishe, mamalishe, nataka niufahamishe umma huu kwamba sasa hivi watu wengi wanapenda kula kwa mama lishe kwa sababu chakula ni kitamu, kinapikwa kidogo na kilichoungwa vizuri na nazi na kila kitu. Mtu anapiga kona tu anachota anakula kwa mama lishe. Shida ya maeneo haya yamekaa hovyo hovyo, takataka zinatupwa hovyo, mitaro inaziba, huwezi kumchukulia mtu hatua matokeo yake ni kipindupindu na magonjwa ambayo hatukuwa tumetarajia. Hii yote ni kwa sababu wale ni watu ambao wanatembea na jiko na vitu vyake vya kulia, dakika yuko hapa, dakika yuko pale, wanahamahama. Athari nyingine Serikali inaingia gharama kubwa sana kusafisha miji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona katika ule ukurasa wa 37, Mheshimiwa Waziri ameongelea shughuli za usimamizi wa usafi kwamba sasa baada ya tamko la Rais tufanye miji yetu safi kila mwisho wa mwezi kila mtu akafanye usafi, itadumu kwa muda gani? Is this sustainable? Inatakiwa sasa tujue kwamba watu wote wanatakiwa waweke maeneo yao safi hususani hao akina mamalishe na babalishe. Mwarubaini wake ni nini? Ni Halmashauri zetu kutenga maeneo sasa ya kina mamalishe wawaambie hapa ndiyo mtakapokuwa mnafanyia biashara zenu na msionekane kwingine. Siyo tu kwa akina mamalishe ni pamoja pia na wale vijana wetu ambao wanaitwa matching guys.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.