Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, ambae anataka Bunge lako liweze kumpitishia bajeti ya bilioni 74.2 ili aweze kutekeleza majukumu yake. Pia, mimi nitangulie kuunga hoja mkono kwamba Waziri tutakupitishia bajeti hiyo ili uweze kwenda kushughulikia ustawi wa jamii yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitangulie kumpongeza waziri pamoja na naibu wake na watendaji wake kwamba, wizara yao ndani ya muda mfupi tangu imeundwa wameweza kutengeneza miongozo na kuanzisha madawati ambayo watatathimini utendaji kazi wao ili mwishowe tuweze kuona kwamba wanafikia ule ufanisi ambao unatarajiwa baada ya kuandaa hiyo miongozo pamoja na madawati waliyoanzisha mahali pote yalipo aanzishwa. Lengo ni jamii yetu iendelee kupata ustawi na maadili yaweze kupatikana lakini pia kushughulikia changamoto ambazo zinaikabili jamii yetu.

Mheshimiwa Spika, asubuhi ya leo ningependa kutoa mchango wangu kuhusu sehemu moja ya kwanza inayohusiana na elimu ya makuzi pamoja na malezi ya mtoto.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa tabia ya mtu inafanyika katika miaka saba ya awali. Katika miaka saba hii ya awali ndipo mtoto katika akili yake changa anaweza kuelekezwa mambo yaliyo mema na akili yake changa iko tayari kupokea kutoka kwa wazazi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunaambiwa kwamba katika miaka hiyo saba ile mitatu ya awali ndiyo ya msingi kabisa maana ndipo tunapojenga msingi wa kupokea maadili, msingi wa kuchambua yaliyo mema na ndio maana napenda nitumie mitahli moja inayotoka katika kitabu cha Mithali 22:6 inasema “Umlee mtoto katika njia impasayo naye hataiacha hata atakapokuwa mzee”.

MBUNGE FULANI: Haleluya.

MHE. PROF. SHUKRAN E. MANYA: Mheshimiwa Spika, sasa, kama hilo ndilo hoja ya kwamba malezi ya mtoto angali mtoto mdogo akilelewa vizuri hataweza kuiacha njia hii hata uzee wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana yangu ni nini? Katika kipindi hiki cha miaka ya awali na ndio mana tunapendekeza miaka hii ya awali, mtoto aweze kukaa na wazazi wake. Wazazi wake wapate namna ya kumuingizia maadili wanayoyataka wao. Kwa hiyo, ndio muda wa kumlinda mtoto yaani first line of defense (hatua ya kwanza ya ulinzi wa maadili ya mtoto ni akiwa nyumbani kwao) ndipo ambapo anawekewa misingi ambayo ataweza kuiishi hata huko baadae. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, anapokuwa amelindwa ndio muda wa kumweleza mtoto kwamba wewe ni wa jinsia ya kike, wewe ni wa jinsia ya kiume na wala hakuna trans gender wakati huo akiwa mdogo. Yaani asifike mahali eti akishakuwa mtu mzima anakutana na mafundisho ya kwamba eti kuna jinsia ya katikati hapa, hapana. Akiwa mtoto mdogo ndio wakati wa kumweleza, ndio wakati wa kumweleza mtoto, wewe unapaswa kujitambua kwamba ukiwa wa jinsia ya kiume au ya kike hakuna kuguswa na mtu yeyote yule sehemu zako za siri. Huu ndio wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ndio wakati wa kumuonesha mtoto upendo, ndio wakati wa kumuonesha mtoto imani, kujenga naye imani na ujasiri wa kwamba iwapo mtu awae yote si mjomba, si baba mdogo, si shangazi, mtu awae yote atakapo kutendea jambo lolote ambalo si jema baada ya kumfundisha jema, apate imani na ujasiri wa kuja kumwambia baba yake au mama yake kwamba fulani amaenitendea hivi, huu ndio wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, kwa jinsi hiyo kama hivyo ndivyo, huu wajibu unawaangukia wazazi na hasa akinamama. Na ni wajibu ambao haupaswi kuahirishwa wala haupaswi kupokezana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa jinsi hiyo niombe sana, yawezekana kweli jamii yetu inahangaika kutafuta mali, yawezekana kweli tunajaribu kutengeneza namna ya kujenga chumi zetu za familia, ni kweli.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni wajibu ambao hauhamishiki, kwa sababu ni wajibu ambao hauwezi kuahirishwa, wazazi tusiseme huu usemi ambao tunapenda kusema kila wakati “sina muda” hapana. Wazazi tutenge muda hata kama majukumu yetu ni makubwa kiasi gani yanatutaka, ni lazima kila siku inayopita tutenge muda wa kukaa na watoto wetu na usemi wetu wa kusema sina muda hiyo sio usemi unaopaswa kusemwa na mtu aliye na mtoto mdogo ambae ni mzazi anaetambua kwamba huu ndio wakati wa kujenga maadili ya mtoto wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbona hata kama tunakuwa busy mbona tunakuwa na muda wa whatsApp, twitter na facebook katika simu? Si ni bora tuache hiyo Facebook, tuache hiyo twitter lakini tupate muda wa kujenga maadili ya Taifa lijalo. Tukifanya hivyo, mafundisho yote yanayokuja yale ambayo ni potofu hata haya ya kumwandaa mtu katika kumuingiza mtindo wa ushoga, kama ameandaliwa vizuri mtoto atakuwa anajitambua na mtoto atakataa kushawishiwa katika maadili potofu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wazazi lazima turudi tuchukue sehemu yetu, tukae kama wazazi, tufanye wajibu unaotuangukia na wala tusisingizie shughuli za kuingiza mali au shughuli za uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa namchukua huyu mtoto kwamba pale nyumbani ameandaliwa vizuri, baadae anatamani kwenda kwenye jamii, yawezekana ni shule au yawezekana kupata masomo ya dini huko. Lazima tuweke mifumo thabiti na salama inayomhakikishia huyu mtoto ulinzi wake.

Mheshimiwa Spika, ninaposema hivi ni kweli kwamba Mheshimiwa Waziri, atasema ameanzisha madawati lakini ni lazima tuweke mifumo rahisi na myepesi ya kushughulikia iwapo hawa ambao wamepewa dhamana ya kumlinda na kumtunza wanakwenda njia ambayo sio. Maana kama walivyosema wenzangu, watu wengine ambao wameaminiwa ni shule, viongozi wa shule, wameficha maovu haya wakitamani kuyamaliza kwa njia nyepesi, hapana. Kwa hiyo, Serikali iweze kuweka mfumo ambao ni rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naona kama muda wangu umekwisha.

SPIKA: Dakika moja.

MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Spika, niongelee hoja ya mtoto yatima. Mtoto yatima akiwa private school (shule ya binafsi) inakuwa vigumu kurudishwa katika mfumo wa shule za Serikali. Kwa hiyo, katika dawati lake inapotokea mtoto yatima wazazi wake wamefariki, Serikali iweze kurahisisha namna ambayo huyu mtoto anaweza akasaidiwa kutoka shule ya binafsi kurudishwa katika shule ya Serikali ili wazazi wasiweze kupata shida sana katika kumhudumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)