Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nimshukuru Mwanyezi Mungu kwa kunijalia siku ya leo kuwa na hali ya uzima wa afya na kushuhudia bajeti ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum ambayo leo inasomwa tarehe 18 Mei, 2023.
Mheshimiwa Spika, naungana na Mheshimiwa Waziri kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hasan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kunipendelea na kuniamini kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum. Lakini pia niwashukuru viongozi wote wa Wizara na watendaji kwa kutekeleza majukumu ya Wizara.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya pekee naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum kwa maelekezo na ushirikiano wa hali ya juu anaonipa katika kutekeleza majukumu yangu katika Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuwashukuru viongozi wangu wakuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Isdor Philip Mpango kwa kuendeleza vyema na kutusimamia katika Wizara yetu hii na kuhakikisha tunakwenda vyema na tunatekeleza majukumu yote ambayo tunahitaji. Lakini pia sina budi kuwashukuru familia yangu kwa kunipa wepesi na kufanya kazi zangu kwa urahisi ili kuhakikisha kazi zangu zote zinakwenda kwa salama na amani.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya naomba nitamke rasmi kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia 100, lakini pia niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia hoja hizi. Niishukuru Kamati ambayo imeungana na sisi katika kutuelekeza hoja zetu na kutupa maelekezo ambayo tutayafanyia kazi kadri wanavyotuelekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwashukuru waunga hoja wote ambao wamechangia katika Wizara yetu hii ya Maendeleo ya Jamii, wengi wamezungumzia masuala ya ukatili wa kijinsia kwa watoto wetu. Ni kweli Serikali yetu sasa hivi tuna kazi kubwa ya kuelimisha na kutoa elimu kwa wananchi kwa ajili ya watoto wetu kutokana na mmonyoko wa maadili ambao unaendelea katika nchi yetu. Suala hili limechangiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi, na sisi kama Wizara tutaendelea kutoa elimu kuhakikisha kwamba watoto wetu wanakuwa salama. Nitoe msisitizo kwa wazazi, wazazi, ukatili wa kijinsia unaanzia katika nyumba zetu, kwa hivyo wazazi tuhakikishe tunapata muda wa kushirikiana na watoto wetu na kukaa na watoto kuwapa elimu ili wao waweze kuelewa mila na desturi za utamaduni wetu katika nchi yetu hii ambazo zinaendelea ambapo nchi nyingi wanapenda mila zetu na desturi zetu katika nchi hii na wanapenda kuziiga; lakini wanakuja kwa mlango wa nyuma kuhakikisha kubomoa utamaduni wa nchi hii.
Mheshimiwa Spika, nitoe rai tu kwa wazazi walezi jamii kujumuika katika malezi makuzi na matunzo ya ukuzi wa mtoto ili kuwawezesha famila kuwa sehemu salama kwa watoto, kuishi na kufurahia haki zao katika hatua mbalimbali. Hatua kali tutazichukua kwa wale wazazi ambao wanajua kama mtoto wao huyu ana matatizo lakini akamwachia kwa makusudi tunaomba wazazi kwamba mtoto ukimuona ana matatizo basi Wizara ipo, mfikishe pahali salama, sisi Wizara tutaweza kumhudumia.
Mheshimiwa Spika, mtoto ambaye unamuona nyumbani humuwezi sisi Wizara tuna vituo vyetu vya kulelea Watoto, tunalea watoto kwa kutumia haki zote zile ambazo wanazozihitaji. Mtoto anahitajika kupewa haki zote za msingi kuanzia elimu mavazi na kila kitu ili aweze kukua vizuri na kukua katika saikolojia nzuri, kwa sababu tunawahitaji sana. Watoto tunawahitaji kwamba, ni viongozi wetu wa kesho, tusipowapa malezi bora hivi sasa basi tutakuwa na taifa ambalo halina viongozi bora. Hivyo tujitahidini wazazi.
Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako Tukufu niwaombe Waheshimiwa Wabunge wanapokuwa katika majukwaa basi watoe elimu hii kwa wazazi na walezi ambao wanalea watoto hawa ili kuhakikisha malezi na makuzi yanaenda salama.
Mheshimiwa Spika, aidha, natoa wito kwa jamii na watu wenye moyo wa kutoa huduma kwa malezi na makuzi kwa watoto wa kambo kuhakikisha kwamba wanawalea watoto hawa kwa kuzingatia ubora na haki zote ambazo zinahitajika. Lakini pia kuna Waheshimiwa wengine hapa wamezungumzia kuhusu mmonyoko wa ndoa na mirathi.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna mmonyoko wa ndoa unaotokana na ukatili wa jinsia kwa wanawake. Kuna waume wengine wanakuwa hawana imani kwa wake zao. Jambo linaweza kuwa dogo lakini wao wanalichukulia kubwa na kuwapiga wengine hadi kufikia kuua. Niwaombe wazazi wenzangu wanapofikia hadi hali hiyo watoe taarifa katika vyombo husika, wasikae kimya, sheria zipo zinaowalinda.
Mheshimiwa Spika, ili uweze kuwa na haki kamilifu basi unatakiwa utoe uwazi wote mahakama itakusikiliza na ikupa haki yako. Na ndoa ambazo tunazihitaji zote zitasikilizwa. Ili mtu aweze kupata urithi basi ndoa hizo tujitahidini tunapokutana na wapendanao basi tukazisajiri ndoa zetu, ili kuhakikisha kwamba mirathi ile inakwenda kutokana na taratibu; na kila mtu anadini yake ambayo anapokea mirathi kutokana na mtiririko wa usawa na ugawaji wa mirathi hiyo.
Pia nizungumzie kuhusu watoto wa mitaani. Ni kweli kuna tatizo la watoto wa mitaani, lakini watoto hawa wanatokana na mmonyoko wa maadili kwa wazazi. Wazazi wanapokuwa hawafahamiani, wanapogombana basi hawashughulikii watoto na watoto wale wanaanza kuingia mitaani. Hili linaipa mzigo mkubwa Serikali. Serikali sasa hivi tumeamua, tumeunda Kamati ambayo itawasimamia watoto hawa ili kuhakikisha kwamba watoto ambao wapo mitaani tunawarejesha kwa wazazi wao, na mpango huo, tunamhitaji mzazi huyo tutapomkabidhi basi tutampa masharti ambayo mtoto atakaporudi tena mtaani basi tutamkamata yeye kwa sababu vipo vituo ambavyo vya kupeleka malalamiko na vipo vituo ambavyo mtoto anaweza akasaidiwa kuhakikisha anapata haki zake zote.
Mheshimiwa Spika, pia kuna vituo vyetu vya malezi ya Watoto, ambapo tuna Kikombo – Dodoma na Dar es salaam – Kurasini. Watoto hawa tunawalea na tunawapa haki zao zote za msingi na malezi bora, kwa hivyo watoto wetu hawa tuwatunze.
Mheshimiwa Spika, mmomonyoko wa maadili upo lakini tuhakikishe tunafanikisha sisi wazazi. Mtoto halelewi na mzazi mmoja au mzazi peke yake. Utamaduni wetu huko nyuma wazazi tunalelewa mpaka na majirani. Mama Salma hapa ana msemo, anasema mtoto wa mwenzio ni wako. Wahakikishe kwamba tunashirikiana, na wazazi tuwape watoto malezi bora.
Mheshimiwa Spika, pia kuna jambo jingine ambalo limesemwa hapa na Waheshimiwa kuhusu wafanyabiashara wadogowadogo. Ni kweli wafanyabiashara wadogowadogo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaamini na amewajali na kuwaleta katika Wizara yetu hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ili kuhakikisha na wao wanapata fursa mbalimbali za kufanya biashara ili waweze kukua kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, Wizara hii Mheshimiwa Rais ameiunda kuhakikisha kwamba amaeona kwamba wanawake wengi walikuwa wanapata tabu na biashara zao, hawana sehemu za kuzipeleka hawana sehemu za uhakikika kuhakikisha biashara zao zinafanya kazi.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ametoa fedha takriban mikoa yote 26 na kuhakikisha kwamba kunawekwa Wizara ambazo zitawasaidia hawa wajasiliamali wadogowadogo, hasa wamachinga, nao watajisaidia katika Wizara zile na malalamiko yao yote basi katika ofisi hizo ambazo ametoa pesa Mheshimiwa Rais basi zitasaidia katika kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Spika, tumpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kuwaona na kuwajali wananchi hawa na kuhakikisha na wao wanakua kiuchumi ili nchi yetu iwe na usawa. Kama yeye mwenyewe alivyoamua kuwa kinara wa usawa wa kijinsia basi tumshike mkono ili kuhakikisha Taifa letu linakua na linaendelea vizuri.
Mheshimiwa Spika, kuna mambo mbalimbali ambayo yamefanyika katika Wizara hii. Tunazidi kutoa elimiu Wizara yetu kuwaelimisha wananchi kuhakikisha wanapata elimu ya ukuaji wa maendeleo yao. Kwa hivyo tunawakaribisha sana katika Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii ili kupata elimu na kuhakikisha mambo yao yote yanakwenda sawa.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingi zimesemwa hapa na wajumbe, lakini Mheshimiwa Waziri wangu ataendelea kuzijibu na hoja nyingine zitajibiwa kwa maandishi. Nikushukuru sana na niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao kwa hapa mmetoa hoja zenu na kwa ushirikiano mliotupa. Nawatakieni kila la kheri katika mafanikio ya bajeti hii ili ipite na tuendelee kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii, ahsante sana. (Makofi)