Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. JACQULINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ili niweze kuchangia bajeti hii ya miundombinu ya mwaka 2023/2024. Naomba nianze kwa kumshukuru sana Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo anaifanya na pia kwa miundombinu mizuri sana ya barabara ambazo zimeweza kujengwa katika Mkoa wetu wa Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea nataka tu nikueleze kwamba sisi wana Ruvuma tumebaini kwamba Mheshimiwa Mbalawa kumbe si Mbalawa ni Mbawala wa kwetu Ruvuma. Kwa hiyo amefanya ujanja ujanja tu wa kubadilisha jina ajiite Mbalawa ili akwepe majukumu ya kupeleka miundombinu kule Ruvuma. Kwa hiyo wana Mbawala wenzako wamenituma niseme haya yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya bypass ya kilometa 16 ya Songea Mjini ambayo ni barabara yenye urefu wa kilometa 16, inatoka Mletele kwenda Msamala mpaka Namanditi. Miaka mitano iliopita nikiwa hapa katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimeshaizungumza zaidi ya mara nne, na barabara hii ilikuwa wakati naizungumzia ilikuwa na urefu wa kilometa 11, sasa hivi zimezaliwa kilometa nyingine, sasa ina urefu wa kilometa 16.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Mheshimiwa Waziri alete pesa ili tujenge ile barabara. Kuna msongamano mkubwa sana katika Manispaa ya Songea, malori ni mengi mno yanayobeba makaa ya mawe. Jamani makaa ya mawe yanayopita katikati ya mji kwa kubebwa na malori ni zaidi ya malori 1,000 kwa siku. Ndugu zangu naomba mtusaidie. Kumekuwa na ajali nyingi sana kumekuwa na mitobozano mingi sana kati kati ya mji. Kwa hiyo tunaomba, ili kuwanusuru wananchi wa Manispaa ya Songea tujengee ile barabara ya bypass ya kilometa 16 ili sasa mji wetu uweze kuendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Namtumbo – Tunduru, kwa maana ya Mtwara Pachani kwenda mpaka kule Lingusenguse na hatimaye kufika Mbesa, Mbesa - Tunduru, barabara hii ina urefu wa kilometa 303. Feasibility study tayari imekwisha fanyika, tatizo ni nini barabara hii haitangazwi ili kuleta fedha na iweze kuanza kujengwa? Mheshimiwa Mbawala mwenzetu, tunakuomba sana utusaidie ili barabra hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa barabara ya Likuyufusi - Mkenda yenye urefu wa kilometa 24, niishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na jitihada zinazofanywa na dada yangu Jenista Mhagama na mimi pia nasema tena, maana ninasema kila siku humu ndani. Kilometa 60 za Barabara hii tayari Serikali imeonesha commitment ya kuanza kuijenga. Sasa kuonesaha commitment ni jambo zuri lakini tunataka mafungu yaende ili sasa ianze kujengwa mwaka huu wa fedha. Barabara hii itajengwa kilometa 60 kutoka Likuyufusi mapaka pale Mkayukayu. Sasa tunataka Serikali iweke pia commitment kutoka Mkayukayu mpaka pale Mkenda, kilometa 64, ili ianze kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka hapo Mkayukayu hakuna commitment yoyote ya Serikali. Barabara hii ina urefu huo, kwa hiyo mkijenga kipande nusu halafu baadaye inasubiri tena miaka mitano hainogi kwa hiyo malizieni kilometa 124 zote ziwe na commitment ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya urefu wa kilometa 35 Kitai – Ruanda mkandarasi yuko kazini lakini barabara hii ni barabara ambayo itagharimu pesa za Kitanzania bilioni 60. Lakini mapaka sasa hivi mkandarasi amepata advance ya asilimia 10 tu ambayo ni sawa na bilioni 5.9. Mkandarasi anashindwa kuendelea na kazi, karibu anasimama kabisa na wakati huo huo tunaelekea kwenye masika, tunaomba sasa…

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jacqueline, kuna taarifa.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Taarifa iwe ya maana na mnanijua. Taarifa iwe ya maana.

MWENYEKITI: Karibu Mheshimiwa Benaya.

TAARIFA

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kumpa taarifa mchangiaji kuhusu barabara hii ya Kitai Kwenda hadi Ruanda na inaelekea hadi Lituhi. Mkandarasi amesimama tangu mwezi wa pili kwa sababu ya kukosa malipo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jacqueline taarifa unaipokea?

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Makofi mengi sana kwa Benaya. Nimeupokea mchango huo. Ahsante sana, nataka taarifa zenye afya kama hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyofafanua na inapita kwenye jimbo lake, ni sahihi kabisa kilometa 35 ambazo sasa ndio magari yale yanayobeba makaa ya mawe yanapita kwenye barabara hiyo. Kwa hiyo tunaomba pesa iharakishwe kupelekwa pale ili barabara hii iweze kujengwa. Kutokufanya hivyo maana yake ni kudumaza hali ya uchumi katika Mkoa wa Ruvuma na katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hadhalika Ruanda – Lituhi ameshanisaidia hapo Benaya kilometa 50 mkamalizie pale. Imetangazwa lakini pesa hazijapelekwa. Kutangazwa ni jambo moja, kupeleka pesa ni jambo jingine. Sasa Mheshimiwa Mbalawa mwenzetu tunaomba upeleke pesa kule ili barabara hizi zianze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nizungumzie suala la reli, kwa maana SGR. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri sana anayoifanya. Majuzi amesema kwamba miradi yote iliyoachwa na Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli anahakikisha anaimaliza kwa asilimia 100. Ninampongeza kwa sababu kazi ya SGR inaendelea. Hali kadhalika nimpongeze sana CEO wa SGR ambaye ni kaka yangu Kadogosa ambaye anafanya kazi nzuri sana. Kaka yangu Kadogosa wewe fanya kazi kelele za chura hazimzuii tembo kunywa maji, hizo ndizo changamoto za kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama wajumbe wa kamati ya PAC tumekwenda tumekagua namna mradi unavyoenedelea. Mradi ni mzuri mabehewa ni mazuri, hayo mengine yote ni majungu, endelea kufanya kazi na Mungu akutie nguvu, endelea kupambana, sisi tuko nyuma ayako tutaendelea kukutia moyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie sasa reli ya Mtwara – Mbamba Bay. Mimi naomba sana, ninaamini kabisa Mheshimiwa Mbawala hajaona yale malori ambayo yanabeba makaa ya mawe kule. Angeyaona huyu Mheshimiwa Mbawala mwenzetu kwa kweli angeweza kuchukua jukumu la kuharakisha ujenzi wa reli kutoka Mtwara Kwenda mpaka Mbamba Bay kwa sababu hali ya barabara sasa hivi ni mbaya. Malori yale yanachimba barabara haiwezekani. Ukiangalia barabara ambayo imetengenezwa hivi karibuni inayotoka Songea kwenda mpaka Tunduru pale katikati pale Namingwea mashimo yanafikia hapa kiunioni. Ndugu zangu hali ni mbaya sana. Kwa hiyo tunaomba sasa reli hiyo ikijengwa kwa haraka itarahisisha sana ubebaji wa mizigo, badala ya kubeba kidogokidogo basi itapakia mabehewa mengi na yatasafirishwa kwenda katika Bandari ya Mtwara na kupeleka maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie makaa ya mawe yaliyoko katika Mkoa wa Ruvuma ni makaa super ni grade number one, na ndiyo maana yamekuwa na wateja wengi sana. Daraja ya Mitomoni mwaka jana namalizia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia dakika mbili.

MWENYEKITI: Malizia sekunde 30.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja Mitomoni mwaka jana nilipiga magoti hapa Mheshimiwa Mbawala wewe utapata laana na wana Ruvuma. Daraja lile halijajengwa watu wanaendelea kufa pale.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jacqueline…

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jacqueline, Mheshimiwa Mbunge…

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Litengwe kilometa 22 tunaomba kujengwa Kigonsela kilometa 35. Baada ya maneno hayo machache…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Jacqueline anaitwa Profesa Mbarawa naomba uendelee kumuita Mbarawa na siyo Mbawala.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye anaelewa na ndiyo maana anacheka.

MWENYEKITI: Nashukuru sana, muda wako umeisha nashukuru sana Mheshimiwa.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Ahsante sana, naunga mkono hoja.