Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana kwenye uchumi wa nchi yetu lakini kwenye maendeleo ya nchi yetu kwa sababu taasisi zote muhimu ambazo zinakwenda kuboresha uchumi wetu zipo chini ya Wizara hii. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, pamoja na wakuu wa taasisi zake zote wanafanya kazi nzuri sana na kazi ambazo tunaziona na ule usemi wa kwamba kazi iandelee, hapa kweli kazi inaendelea. Tunawapongeza sana ninaimani huu ni utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi chini ya Jemedari Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hakika kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina mambo kadhaa ya kuweza kuchangia kuhusu Wizara hii na nitapenda nianze na suala la barabara. Tumeona kwenye bajeti hii namna ambavyo barabara nyingi zimeoneshwa kwenda kutengenezwa na barabara nyingine ujenzi wake unaendelea na nyingine tayari zimekwisha zinduliwa. Tunaipongeza Serikali kwenye hili na nina imani zile barabara ambazo bado zimebakia zitakwenda kufanyiwa kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini moja kati ya barabara ambazo bado hazijaweza kujengwa barabara ya mkoa ni barabara ambayo inaunganisha kati ya Mkoa wa Mbeya pamoja na Mkoa wa Tabora na Singida. Barabra hii inapita ndani ya Wilaya ya Chunya ambako ndipo jimbo langu lilipo. Barabara hii ni muhimu sana kiuchumi kwa sababu barabara hii inakwenda inafungua Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Mikoa ya Kanda ya Kati na Kanda ya ziwa. Kwa hiyo, muiangalie barabara hii kwa jicho la kipekee. Maana yake ukiifungua barabara hii kwa kiwango cha lami maana yake sasa utakwenda kuifungua mikoa ya nyanda za juu kwa maana ina mipaka miwili kule, Mpaka wa Tunduma na mpaka wa Malawi unakwenda kutuunganisha sasa na Mkoa wa Tabora na Singida ambapo tunakwenda moja kwa moja mpaka mikoa ya kanda ya ziwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri barabara hii ina umuhimu mkubwa sana, naomba uweze kuiangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia hapa kwenye bajeti yako namna ambavyo miradi inaendelea. Mheshimiwa Waziri na hii barabara na yenyewe naomba uweze kuiweka kwenye mpango wa EPC + F ili na yenyewe iweze kujengwa. Tumeona mmeanza upande wa Mkiwa kilometa 56 lakini hizi ni kidogo sana. Kwa sababu barabara hii ina kilometa zaidi ya 350. Ukianza kilometa 56 upande wa Mkiwa mpaka uje ufike Makongolosi huku inaweza ikachukua miaka mingi sana. Niombe sasa, unapoanza upande wa Mkiwa kule ambako kazi inaendelea, sasa tuanze upande wa Makongolosi kwa maana ya Wilaya ya Chunya ili tuweze kwenda huko angalau tupate kilometa 100, tutaweza kwenda vizuri sana na barabara hii itaweza kukamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna barabara nyingine kuanzia Makongolosi ambayo inakwenda kutuunganisha na Mkoa wa Songwe na Wilaya ya Songwe. Barabara hii inaanzia Makongolosi inapita kwenye Mji wa Mkwajuni inakwenda kutuunganisha na Mbalizi. Barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa Mkoa wa Songwe lakini kwenda kutuunganisha na Mkoa wa Songwe pamoja na Mkoa wa Mbeya. niombe Mheshimiwa Waziri, anapokwenda kupanga mipango yake na hii barabara pia aweze kuiweka kwenye mipango pia iweze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo barabara za mwendokasi. Barabara hizi zimeanza kujengwa kwenye Mji wa Dar es salaam lakini baadae zitaenea katika maeneo mbalimbali kwenye nchi yetu hii ya Tanzania. Barabara hizi ni nzuri, sasa hivi Mji wa Dar es Salaam unapendeza. Lakini, zinapokuwa zinajengwa hizi barabara kunakuwa na changamoto kwenye ujenzi wake. Tumeona, wakati wa awamu ya kwanza ya barabara inajengwa tumeona kwa maana ya kuanzia Barabara ya Morogoro, lengo kubwa lilikuwa ni kwenda kuzitoa daladala ambazo tumekwishazoea kuzitumia siku zote. Hata hivyo, lengo hili lilishindwa kutimia kwa sababu wakati wanajenga havikujengwa vituo vya kusimamia dala dala za kawaida. Leo hii dala dala za kawaida zinasimama katikati ya Barabara, hali ambayo inapelekea foleni kubwa sana. Lengo la barabara ya mwendokasi ni kupunguza foleni lakini kwa sababu tulishindwa kuzitoa dala dala za kawaida na zenyewe zinasimama kwenye vituo zilivyozoea kusimama kule. Hii barabara inakuwa tena haitusaidii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilitegemea Mheshimiwa Waziri pamoja na wataalamu wake hasa wa TANROADS, kwamba baada ya kuona awamu ya kwanza tumeshindwa kuzitoa dala dala , awamu zinazofuata kwa maana ya kuanzia Barabara ya Kilwa Road kwenda Mbagala na hii ya Nyerere Road kwenda Gongo la Mboto tuweze kuweka provision ya vituo vya dala dala hata kama dala dala hizi tutakuja kuzitoa baadaye, hii provision ya vituo hivi vya dala dala itatumika pale mtu atakapokuwa amepata emergence gari itasukumwa itakwenda kusogezwa pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunavyosema na wewe gari inapopata tatizo lolote mtu anaweza kutembea kilometa mbili mpaka kikometa tatu ndipo aweze kupata mahali pa kuweza kujibanza. Hii tunaomba sana mlichukue na huko mbele mnapoendelea kujenga, na hata sasa hivi kwa kuwa bado ujenzi unaendelea, muone namna ambavyo mnaweza kulirekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia Uwanja wa Ndege wa Songwe. Tunaishukuru Serikali imefanya kazi nzuri sana uwanja wetu sasa hivi umekuwa ni mzuri, jengo letu la abiria sasa limefikia zaidi ya asilimia 98 na kwa kweli jengo linapendeza sana, lakini pia uzio kwenye uwanja wetu wa ndege umekamilika tunaipongeza Serikali kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hili, mimi niombe sasa, ule uwanja jengo la abiria pale imeshakamilika, sasa, hizi asilimia zilizobakia ziweze kukamilika na baadae sasa jengo hili lizinduliwe ili sisi wananchi wa Mbeya na wananchi wa Nyanda za Juu Kusini tuweze kufaidika na huduma bora ambazo zinapatikana ndani ya uwanja huu wa ndege, na hasa ukizingatia sasa hivi ndege zinaanza kutua usiku, kwa hiyo wananchi wengi sana hapa wanatumia ule uwanja. Nina imani jengo lile litakapokamilika huduma nyingine zitazidi kuboreka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bei yake, ule uwanja sasa hivi hauna cold room; niombe wakati ujenzi huu unaendelea iweze kujengwa cold room kwa ajili ya perishable goods. Tuna amani, kwamba sasa hivi kuna parachichi pale zinazalishwa kwa wingi sana zitahitaji kusafirishwa kwenda nje, tuna mazao ya horticulture na mazao ya maua yatasafirishwa kupelekwa nje. Haya yote yanahitaji sana ile cold room. Kama ulivyosema kwenye hotuba yako, sasa ndege ya mizigo iko njiani inakuja, sasa, ndege ya mizigo hii kama iko njiani inakuja itashindwa kufanya vizuri kwa ufanisi kwa sababu cold room sasa hivi hatuna pale. Niombe sana hivi vyote viwili viweze kwenda kwa pamoja, vitaweza kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo na upande wa ATCL, wanafanya kazi nzuri, lakini kumekuwa na changamoto kubwa sana ya cancellation ya safari. Sisi watu wa Mbeya mara nyingi sana tumekuwa tunasafiri kwa ndege hizi usiku. Tiketi inakuonyesha saa kumi na mbili jioni, mara saa mbili usiku unakuja kuondoka saa saba za usiku; na hii yote inakwenda hata taarifa haupewi, na baadaye unakuta tu hata kuombwa radhi inakuwa ni changamoto. Lakini sisi abiria ambao leo ukipata changamoto kama hiyo ukataka Kwenda kubadilisha tu tiketi yako, bei ya kubadilisha tiketi ni kubwa sana, ambapo ni bora ukate tiketi mpya kuliko kubadilisha tiketi ambayo inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili wananchi wengi wakaosa mahali pa kusemea. Sasa sisi tuwaombe kupitia Wizara lakini kupitia watu wa ATCL, ninaimani Engineer Matindi ni msikivu sana, waliangalie kwa jicho la peke yake. Wananchi wanapotaka kubadilisha tiketi basi bei iwe reasonable ambayo kila mwananchi anaweza akafanya hivyo, lakini bila hivyo wananchi wengi wanaumia kiasi kwamba inafikia hatua mtu anaona ni bora aiche tiketi iende apate tiketi upya kuliko kubadilisha tiketi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naunga mkono hoja.