Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii. Kwanza nianze kumshukuru Mungu sana kwa kunipatia uhai na kunijalia kuwa hapa. Nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini kunileta hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, ambaye hakika ametufanyia maajabu mengi sana kwa kutuletea miradi ya maendeleo kwenye maeneo yetu. Vilevile leo pia kwa mara ya kwanza nishumkuru sana Mheshimiwa Waziri Mbarawa na Naibu wake Kasekenya na Naibu mwingine Mwakibete na nishukuru sana Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimekuja kwa namna nyingine kabisa ya shukurani, kwa sisi Wakristo kuna maneno kwenye Biblia yanasema hivi “Moyo usiyo shukuru hukausha mema yote.” Sasa mimi sitaki kuwa kama hivyo, ni siku mbili zimepita Mheshimiwa Waziri amekuja kwenye Jimbo langu na tumesaini mkataba wa kujengewewa kilomita 25 kwa lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini ambao hawakuona barabara hiyo tangu wamezaliwa, tumesaini mkataba. Sasa ninaposaini mkataba ni wazi kwamba ni ishara tosha kwa sisi Wakristo huwa tuna ndoa tunazifunga na mkataba ule tunauchukulia kama ndiyo ndoa mie na Serikali ya kujengewa barabara hiyo. Kwa maana hiyo basi naamini kabisa kutokana na kilichofanyika jimboni, ni wazi kwamba barabara itajengwa na wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini wataona barabara ya lami mwaka huu. Naamini kwa mkataba tuliyo saini, hakika sina namna ya kushukuru na neno la shukrani siyo kubwa sana. Kwa lugha yetu ya Kiswahili unasema ahsante, ukiongeza sana unasema ahsante sana imeishia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kwa kingereza pia na unajua siyo neno refu ni thank you unamalizia thank you very much, hata ukiongea kwa lugha yangu nyingine ya mtani wangu Mwigulu unasema nini songela ukiongeza unasema songela zigizigi, hata kwa rafiki yangu Musukuma unasema wabheja halafu unaelekea kwenye wabheja sana. Sasa hizi ni shukurani na kwa sisi Wakristo huwa tukishukuru tuna namna yetu kwenye sala ya baba yetu unaposema “Baba yetu uliye mbinguni jina lako litukuzwe” una mshukuru huyu Mungu, halafu unaendelea tena unasema “utupe riziki za kila siku” maana yake unaomba tena. Sasa ndugu yangu Mheshimiwa Mbarawa kilomita 25 si ndogo, sasa si ndiyo naomba tena. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeiona barabara ile iko hapa na imetengewa fedha, imetengewa bilioni tano. Siyo ndogo kwa sababu si nilikuwa sina, ilikuwa zero. Sasa kwa sababu barabara ile ni kilomita 389, nimwombe Waziri huo mwanzo siyo mbaya, leo nimekuja kwa namna nzuri kabisa ya upole, ile sarakasi ya mwaka jana Waziri hataiona leo. Hataiona kwa sababu tumekubaliana tunajenga barabara na kwa ajili hiyo basi naomba ndugu yangu ameonyesha kabisa hapa anajenga kilomita zote hizi 389 kuanzia Karatu, maana ataunganisha Mkoa wa Manyara na Arusha, atakuja Mbulu Mjini, atakuja Dongobesh, atakwenda Haydom, lakini pia atakwenda Sibiti utakwenda na Lalago River mpaka Meatu na Simiyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa tu taarifa ndugu yangu hapa kilomita 25 ni nzuri kwa hiyo tumeishai – design tayari, lakini naomba basi sasa barabara ile ijengwe kama nilivyosema na hawa Washirika wa Maendeleo ambao Waziri amewasema hapa EPC + Finance, lakini asisahau ile Barabara ya Dareda unakuja Dongobesh ambayo ameiwekea kilomita nane, lakini pia barabara ile pia ambayo inatoka Mugitu kuja Haydom kwa sababu Mheshimiwa Waziri ameahidi katika mkutano ule wa hadhara, naomba asiisahau hiyo barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba barabara hizo zitakavyojengwa, Waziri atakuwa amefungua maeneo ya uchumi katika eneo letu kubwa kabisa ambalo unakwenda moja kwa moja kutokea Meatu, hata watu wa Mara watapitia barabara ile hawana haja ya kuja Singida, hawana haja ya kwenda Babati wanapoenda Arusha hata wanapoenda Ngorongoro hawana haja ya kupitia kwenye Msitu ule wa Serengeti. Kwa hiyo barabara ile hakika ni ya kimaendeleo. Kwa bahati nzuri kule tunalima vitunguu, vitunguu saumu, mahindi, mbaazi, alizeti, kwa hiyo ni barabara ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, ombi langu kubwa sana hasa kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha tumeisha saini mkataba, isitokee ile tabia tunayoiona ya kusubirisha wakandarasi wasipate fedha. Naomba Mheshimiwa Mwigulu, yeye ni mtaalam wa mambo ya uchumi, awalipe hawa wakandarasi ambao sasa tumeshasaini, fedha ziende mara moja ili barabara ijengwe kabisa moja kwa moja. Sasa hivi kesi mimi na Waziri Mheshimiwa Mbarawa imeishia hapa kwa sababu najua tumeshasaini, kesi yangu inahamia kwa Mheshimiwa Mwigulu ili atoe hela na hela hizi anapozitoa maana yake ni barabara inajengwa. Nina hakika wananchi wa Mbulu ambao Mbulu imeanza mwaka 1905, ilikuwa haina barabara kwa kusaini huko basi, maana yake tutakwenda kujengewa barabara ambayo itaondoa kabisa ile hali ambayo ameisema Mheshimiwa Mbunge mmoja wa Singida hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ya Haydom ni hospitali kubwa sana, inategemewa sana na Mikoa mitano Simiyu, Singida, Manyara…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana na kwa kweli leo niunge hoja mkono na nimalizie hapa. (Makofi)