Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi. La kwanza, nianze kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakifanya katika kuwekeza katika miundombinu na maeneo mbalimbali. Tumeshuhudia namna uwekezaji ulivyo mkubwa kwenye kampuni yetu ya ndege, ndege mbalimbali zimenunuliwa na zingine ziko njiani zinakuja. Kwa kweli wamefanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia uwekezaji kwenye SGR ambayo ni matrilioni ya fedha. Tumeshuhudia uwekezaji kwenye bandari, kwenye upanuzi wa bandari na wametumia zaidi ya milioni 421 dola za Marekani kwenye upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na maeneo mengine. Kazi kubwa wameifanya tunawapongeza sana. Kwa hiyo tunaipongeza Wizara, tunawapongeza watendaji wote, watendaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara hii wanafanya kazi nzuri sana. Hongera sana sana kwa kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwanza kwa kutusaidia kuhakikisha kwamba Barabara ya Ruanda – Idiwili mapaka Nyimbili ikiwa inaelekea mpaka Itumba kwa kuiweka kwenye bajeti imepangiwa bilioni moja japo ni ndogo, lakini tumeona wameweka kilomita 21, tunawashukuru sana kwa kazi hiyo nzuri. Pia kuna Barabara ya Vwawa – Hasamba kwenda kwenye Kimondo, Kimondo cha aina yake ambayo wamekuwa wakiijenga, wanaendelea kuijenga. Tunaamini wataendelea kutenga fedha ili kuhakikisha kwamba ile barabara inakamilika, kusudi watalii wanapoenda kwenye kimondo waweze kufika kiurahisi. Tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna Barabara ya kutoka Ihanda kwenda Chindi kupitia Ipunga hii barabara wanaifanyia kazi, wanaihudumia, tunashukuru sana kwa wakiendelea kuihudumia. Kuna Barabara ya Hezya mpaka Itumba bado ilikuwa kwenye upembuzi yakinifu, sasa tunataka waikamilishe ili ile barabara sasa watu wa kutoka Malawi wanaweza wakapitia ile barabara mpaka kuja katika maeneo mengine, kwa hiyo tunaamini wataendelea kuifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Meneja wa Mkoa wa TANROADS, anafanya kazi nzuri sana. Huwezi kuamini wakati mwingine saa sita za usiku anakwambia naenda kuangalia sehemu fulani mkandarasi amekwama, naenda kufuatilia hiki, anafanya kazi nzuri sana na anatupa ushirikiano mzuri sana, nampa hongera kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi pale Mpemba tunaomba Bandari Kavu. Tunataka mizigo ikisafirishwa na TAZARA kutoka Dar es Salaam iende mpaka pale Mpemba ili Nchi za SADC, ziende kuchukulia mizigo pale itarahisisha sana na itakuwa imetoa mchango mkubwa sana tunaomba sana hilo liweze kufanyika na tunaamini litatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sanjari na hilo Reli ya TAZARA ni muhimu ikaimarishwa, ikaboreshwa, mabehewa yakatafutwa, uwekezaji ukafanyika, ile sheria tukaipitia upya ili kuhakikisha kwamba iendelee kutoa mchango mkubwa katika eneo la kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nchi yetu imebahatika kwa sababu ni nchi ambayo tuna bahari kubwa, tunayo Bahari ya Hindi, tunayo Maziwa na maeneo mengine. Nchi yoyote wenye bandari, yenye bahari haitakiwi kuwa maskini. Sisi tumebahatika kuwa na nchi ambayo tuna–access na bandari, sasa uwekezaji lazima ufanyike, natamani kuona Bandari ya Dar es Salaam ifanane na Bandari ya Rotterdam, Bandari ya Singapore na bandari zingine kubwa duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote yanawezekana kwa kuwekeza na uwekezaji wa kwenye bandari unaweza ukawekeza kwa hela ya kukopa, unaweza ukawekeza kwa kukopa kutoka kwa wananchi kama walivyofanya Wamisri, Wamisri wakati wanajenga ule mfereji wa Suez Canal wa pili wao walikopa kwa wananchi, wakaamua kujenga mfereji wa pili ili meli ziwe zinapishana, waliamua na sisi tunaweza tukawekeza pale kwenye bandari kwa hela ya kutoka kwa wananchi au tukakopa nje au tukafanya lolote lile maadam bandari yetu tuongeze uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha bandari hii inapanuliwa, bandari hii ifanye kazi, tunataka kuona pale Bandari ya Rotterdam upana wa kule ni kilomita 42, sisi pale bado ni padogo. Kwa hiyo tunahitaji eneo hata lile lote la Kigamboni, watengeneze maeneo ya kuweka mizigo, waboreshe ili kusudi mizigo yote ya huku iweze kupitia pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo iwe tuna fedha iwe hatuna ambapo tumefanya maamuzi makubwa ya kukopa, ya kutafuta kila mahali tulivyowekeza na Bandari ya Bagamoyo atafutwe mwekezaji, ajenge na yenyewe ikiwezekana ile bandari nyingine kama itapatikana kokote tujenge ili tuweze kujenga uchumi imara wa nchi yetu. Tunaamini kwa kufanya hivyo, mizigo ya nchi jirani inaweza ikahudumiwa na nchi yetu ikapata fedha nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nakushukuru kwa kunipatia nafasi.