Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi angalau kwa dakika chache niweze kusema mambo yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mungu kwa kunipa nafasi lakini la pili na mimi nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ya kipekee ambavyo amekuwa mtu mwema sana katika kuhakikisha kwamba fedha nyingi zinazokwenda kwenye miradi zinasimamiwa na zinatekeleza miradi ambayo imekusudiwa. Na hakika, kama mwenyewe anavyosema, hakuna mradi uliosimama kila mradi uliokusudiwa unaendelea na tumekuwa na miradi bora sana. Nimshukuru kwa kuhakikisha ya kwamba tunavyozungumza kama wenzangu waliokwisha kupita wamesema; ukitazama Daraja la Busisi ambalo linaunganisha Mkoa wa Mwanza na mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pale kwenye bandari utakuta kuna meli kubwa ambayo itakuwa ni meli ya kipekee katika ukanda wa maziwa makuu; MV. Mwanza, ambayo kwa hakika iko hatua za mwisho kabisa kukamilika. Ukitazama standard gauge ambayo inaanzia Mwanza kwenda isaka nataka nikuhakikishie kwamba miradi hii yote inatekelezeka na iko, wakandarasi wako kazini, na hakika wanafanya kazi nzuri sana. Ba hii peke yake imefanya Mji wa Mwanza kuwa busy, Mji wa Mwanza kuwa mji ambao unampishano wa watu kila mara na kwa wingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni nini? tafsiri yake ni kwamba uchumi unaojitokeza kwenye uendelezaji wa miradi unaotoa ajira nyingi kwa vijana tafsiri yake ni kwamba kukamilika kwa miradi hii kunaifungua mkoa wa Mwanza kunaifungua Kanda ya Ziwa na kufanya sasa mji huu uendelee kuwa mji wa pili mashuhuri na kwa ukubwa katika nchi hii katika kuhakikisha kwamba miradi hii inakuja kuleta tija kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusudi hilo nataka nimuombe Mheshimiwa Waziri mambo mawili peke yake. Kama tunazungumzia miradi yote hii na haina muda mrefu inakwenda kukamilika tunao Uwanja wa Ndege wa Mwanza. Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, unapozungumza ujenzi wa Daraja la Busisi, unapozungumza ujenzi wa SGR kutoka Mwanza kwenda Isaka unapozungumza uboreshaji wa bandari na ujenzi wa meli kubwa tafsiri yake ni kwamba Mji wa Mwanza unakwenda kuwa mji wa kitalii lakini unakwenda kuwa mji wa biashara asilimia 100. Hivyo nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, ninafahamu, ujenzi wa uwanja wa ndege, njia ya kukimbila ndege imeshakamilika lakini hivi tunavyozungumza ni aibu sana kuendelea kusema tuna jiji la pili kwa ukubwa lakini bado tuna uwanja wa ndege unaoweza kupokea ndege za kwetu za ndani peke yake na si ndege za mashirika mengine makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu Halmashauri za Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela zilianza mchakato wa ujenzi wa jengo la abiria lakini ukweli, ni kwamba Mheshimiwa Waziri na wewe utakubaliana na mimi haiwezekani imefika sehemu zimegota na sio jukumu lake kimsingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukuombe Mheshimiwa Waziri kama ambavyo tumekwisha kuzungumza uwanja huu wa ndege urudi TAA usimamiwe na wataalamu wenyewe na hazi halmashauri mbili kwa sababu mpaka sasa zimeshagharamia takribani shilingi bilioni nne fedha hii baada ya kuwa uwanja huu umerudi na jengo hili limechukuliwa zitatazamwa kwenye namna nyingine ili ziweze kupata share na zenyewe ziweze kufaidika na mapato haya ya ndani kwa sababu ni kodi za wananchi zimepelekwa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunasema uwanja wa ndege wa Mwanza? Leo ukitazama unapokea abiria zaidi ya milioni moja kwa mwaka lakini majengo yanayosubiri abiria, maeneo ya kupumzika, maeneo ya kusubiri kuondoka na kuingia hakika hayafanani kabisa na ule uwanja ulivyo hivyo nikuombe sana Mheshimiwa Waziri halmashauri hizi zimesharidhia ziko tayari ni kazi kwako kuhakikisha ya kwamba uwanja huu unauchukua na unauboresha kwenye mazingira ambayo yatafanya uwe uwanja wa kimataifa ndege kubwa zije ili na sisi tuweze kuona faida ya kuruka kutoka Mwanza moja kwa moja kwenda Dubai na maeneo mengine duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu barabara, Mheshimiwa Waziri unafahamu tunayo barabara moja kubwa ya Kenyatta na ya Nyerere. Barabara ya Nyerere na ya Kenyatta ni barabara ambazo zinapitisha abiria wengi sana ukiitaja kwa mfano barabara ya kenyatta peke yake abiria wote wanaoingia Mwanza kutokea Mikoa ya Dar es salaam na mikoa mingine yote ikiwemo mikoa inayounganishwa na Daraja la Busisi wanatumia barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni nini? Barabara hii imekuwa finyu na haina tena uwezo wa kuwahudumia wakazi wanaokuja Mwanza. Kwa hiyo ninachokuomba Mheshimiwa Mbarawa barabara hii ilishafanyiwa upembuzi yakinifu kwa njia nne na ulishakamilika siku nyingi, basi tuitazame kwa jicho la pekee na tuanze kuijenga angalau hata kwa kilometa kumi kwa mwaka wa fedha ujao, itakuwa imesaidia sana kuondoa changamoto hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakazi peke yake wa Mwanza wanaokadiriwa laki sita na sehemu nusu ya wakazi wa Mwanza wanatumia barabara hii, hapo hujawataja wageni. Barabara ina uwezo wa kuchukua magari zaidi ya 3,000 mpaka 6,000 kwa siku hii siyo jambo dogo, ni jambo kubwa, hivyo ni lazima tulitazame kimahesabu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hiyo tu, Mheshimiwa Waziri tumezungumzia namna ya kuipandisha hadhi barabara inayotoka Mkuyuni inapita Kanyenyere inakwenda Tambuka Reli inakwenda mpaka Nyanguruguru inakwenda kutokea Mandu na Mahina. Barabara hii ni muhimu sana kwa wakazi wa Jiji la Mwanza na ni muhimu sana kwa Mkoa wa Mwanza kwa sababu itasaidia kwenye maeneo mengi ambayo tunayategemea mno kwa ajili ya kuwavusha wananchi kwenda kwenye shughuli zao za kiuchumi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja, na ninaipongeza Wizara ya Ujenzi na taasisi zake zote kwa kazi nzuri wanayoifanya, na Mungu aendelee kuwasaidia kulitumikia Taifa. Ahsante sana. (Makofi)