Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia Wizara hii ya Ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambazo anaendelea kuzifanya kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kwa kweli ataacha alama kubwa kwenye nchi yetu kwa kipindi chake cha miaka kumi. Kama tu sasa anamiaka miwili amefanya mambo makubwa sana kama vile amekaa miaka mitano au sita na- imagine akikaa miaka kumi atafanya mambo mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameweza kupigana na miradi mikubwa ya mikakati, ameweza kwenda nayo sambamba kiasi kwamba tumeona juzi amekamilisha Ikulu lakini anaendelea na Bwawa la Mwalimu Nyerere anaendelea na SGR anaendelea na meli ameenda kwenye ununuzi wa ndege, ananunua ndege nne, lakini analipa madeni ya ndege zilizokamatwa na Daraja la Busisi, Daraja la Tanzanite (Salender Bridge) yote hayo ni mambo makubwa na mengine mengi aliyoyafanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona madarasa lukuki yamejengwa bila mchango wowote kwa Watanzania kaya kwa kaya wala nini kwa nini, amefanya yeye kama Rais amesimama wima. Amepeleka pesa nyingi za kutosha kwenye halmashauri zetu. Wakati huu mgumu wa Corona, wa vita ya Urusi na Ukraine majirani zetu wanashindwa kulipa mishahara, Mheshimiwa Samia analipa malimbikizo ya watumishi, Mheshimiwa Samia ameahidi kuongeza mishahara ya watumishi; hakika ana haki ya kupongezwa. Na ndio maana kuna siku nilichangia hapa nikasema Mheshimiwa Rais Samia wale wenzetu wa upande wa pili wana haki sasa ya kumpa heshima ya kumwachia apite bila kupingwa kwa kazi kubwa ambayo anaifanya Mheshimiwa Rais anastahili kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pongezi zangu za dhati kwa Wizara ya Ujenzi kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na Wakurugenzi wake wote wa taasisi akiwepo Katibu Mkuu na Menejimenti nzima. Tunawapongeza sana kwa kazi zote zinazoendelea nchi nzima kila mtu ukizunguruka kazi zinaendelea kufanyika tunaziona na tunawapongezeni sana sana. Kaka yangu Mbarawa hana maneno mengi lakini vitendo vyake ni vikubwa tunakupongeza sana kwa kazi nzuri unazozifanya

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri, akiomba ridhaa ya kuingia ubia kwenye bandari yetu. Nikwambie Mheshimiwa Mbarawa kanyaga twende tumechelewa sana, huu ni usemi alikuwa anapenda kuutumia marehemu kaka yangu Le Mutuz anakwambia kanyaga twende tumechelewa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbarawa tumechelewa. Kwa nini nasema tumechelewa? Wenzangu waliotangulia kusema wamesema kontena lina toka China mpaka Dubai kwa dola 500 lakini Kontena hilo linatoka Dubai mpaka Tanzania kwa dola 4500. Hiyo ni gharama ambazo wafanyabiashara wataendelea kuilaumu Serikali kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie, Serikali haiwezi kufanya biashara. Hivi, crane moja tu likiaharibika linatengenezwa kwa dola elfu 18 utaambiwa kaa pale dokezo linaandikwa kwa Waziri dokezo linapelekwa kwa Katibu Mkuu, dokezo linaenda kwa Mhasibu, mtandao leo umekwama haufanyi kazi, yaani ni mambo ambayo hatutaweza kama Serikali, tutaendelea kulaumiwa; lakini tutaendelea kupata kodi ndogo ambayo itakuja kuwaumiza wafanyabiashara ili Serikali itimize malengo yake. Lazima kama Serikali ibuni vitu vya kuweza kupata kodi nyingi ili kupunguza kodi kwa wafanyabiashara wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni wajibu wa Serikali na siyo mtu mwingine yoyote kuhakikisha kodi inapatikana lakini walipakodi hawaumii. Leo walipakodi wanaumia tumeona mkutano wa Kariakoo wamelalamika mambo mengi na yote hii ni kwa sababu hatuna vyanzo vingi vya kukusanya kodi leo hii Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais ame-organize tukaenda kwenye Expo Dubai, wameenda kusaini mikataba chungu mzima ili tupate wawekezaji watusaidie. Leo Mheshimiwa Mbarawa amethubutu kupata mtu wa kuingia ubia na sisi tunaomba jambo hili liende kwa haraka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Mawaziri wote, tulikuwa wote Dubai mimi nilienda. Wameingia mikataba waendelee kufuatilia wapate wawekezaji ili nchi yetu izidi kupiga hatua. Jambo hili sio geni linafanyika dunia nzima, sio kwetu sisi tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie kitu, nikiwa Mjumbe wa Kamati ya Kilimo lilikuja suala kwamba mazao ya horticulture, mbogamboga na matunda yanasafirishwa kupitia Mombasa. Yanatoka Arusha, parachichi zinatoka Njombe, zinawekwa kwenye magari zinakwenda Mombasa, tukagombana na Waziri na Mkurugenzi wa TAHA tukawaambia kwa nini msisafirishe na Bandari ya Dar es Salaam? Dar es Salaam wakatuambia hakuna facilities za kusafirisha mbogamboga, ni aibu! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashindwa kutafuta wabia au kitu gani? Nashindwa kuelewa, lakini tunaona kwamba Mheshimiwa Rais ameifungua nchi ni sisi tu wenyewe. Leo hii parachichi zinatoka Njombe zinapelekwa Mombasa, Mombasa ndio wanapakia kutupelekea nje ya nchi, ndio maana wananchukua vitu wanavi-label Kenya, tunaonekana sisi hatuna kitu chochote, vitu vyote vinatoka Kenya. Niwaambie hivi, katika hili linalofanyika la kwenda kuingia ubia, tutakwenda kuweka heshima kubwa ya nchi yetu ambayo Mheshimiwa Rais ameitengeneza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii dunia nzima wanamuongelea Samia Suluhu Hassan, dunia nzima anaongelewa, anaonekana Rais mahiri, Rais mwanamke wa mfano, lakini leo tunachukua mazao tunapeleka Mombasa, hiki ni kitu gani? Tunaomba sana ikiwezekana huyo Mbia aingie na Tanga, Mtwara na Bandari ya Bagamoyo ijengwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa nchi hii utapanda lini ikiwa malighafi inasafirishwa kwenye vitu vya bei kubwa. Mtu akifikisha hapa malighafi ya kiwanda amefikisha kwa bei kubwa, akitengeneza kitu lazima akiuze kwa bei kubwa ili na yeye apate fidia na aweze kulipa kodi, lakini leo hii tukiingia ubia malighafi zetu zitafika kwa bei nzuri, wafanyabiashara wetu wakulima watasafirisha mazao yao kwa bei nzuri, watapafa faida kubwa lakini nchi itapata kodi, ikipata kodi mambo yatazidi kwenda vizuri zaidi. Nilikuwa napitia wanasema tukiweza kuingia ubia na hiyo kampuni ya DP tunaweza tukaingiza trilioni moja kwa mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuombe sana na baadaye sisi tulimbana Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe angekuwa hapa angesema. Tukamwambia je tukipata hizo facility wanaweza wakapita Tanzania badala ya Mombasa? Akasema haiwezekani. Tumefanya research wakipita Tanzania hata kama tungekuwa na hizo facility wangelipa asilimia ya faida yao ingeenda asilimia 25 zaidi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Tambwe, muda wako umeisha.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uniongeze dakika moja nimalizie jambo moja.

MWENYEKITI: Malizia sekunde 30, tafadhali.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongee kuhusu Tabora Manispaa. tunaomba barabara ya ringroad inayozunguka Tabora kuchepusha magari. Sasa hivi Tabora imefunguka magari yote yanayokwenda Kigoma, Rwanda, Congo, Sikonge, Mpanda, Mbeya yakipita katika ya mji utakuwa msongamano mkubwa. Tumekaa kama Board Road, tumekubaliana tuweke ringroad, magari haya yatachepushwa nje ya Mji wa Tabora Manispaa kuepusha ajali, lakini kuepusha msongamano mkubwa utakaojitokeza. Tunaishukuru sana Serikali kwa kutufungulia mkoa wetu, lakini tunaomba bado watusaidie hili ili kupunguza ajali na kupunguza misongamano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)