Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nilipokuwa najiandaa kuchangia nilikuwa na mlolongo mrefu sana wa pongezi na shukrani. Nilitaka nianze na Waziri nikimlinganisha na msemo usemao wembamba wa reli unapitisha gari moshi, lakini nikarudi kwamba yupo Kasekenya yupo Atupele Mwakibete, wao wana uwezo pia wa kuongeza kidogo huku kwa Mheshimiwa Waziri. Nikataka niende kwa ma–DG ndugu zetu akina Kadogosa, akina Mbosa, akina Matibila mpaka kwa Meneja wangu wa TANROADS, Engineer Masige.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwisho wa siku nimejikuta pongezi hizi nazijumuisha sehemu moja tu kwa yule ambaye alipewa jicho na Mwenyezi Mungu la kuwatambua vipaji vya hawa watu na kuwapa kuendesha Serikali hii, naye siyo mwingine anaitwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pongezi nyingi sana na shukrani kwake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani hizi zinakuja pia kutoka kwa Wanakyela. Ni hapa juzi tu tulipata janga la kukatika daraja pale Nsesi. Nilipopiga simu moja tu kwa Mheshimiwa Waziri daraja pale tayari. Mheshimiwa Waziri nataka nikwambie daraja liko tayari Engineer Masige ameshafanya mambo, daraja lile mpaka wiki ijayo litakuwa limeanza kupitika, ahsante sana. Wananchi wa Ngonga, Katumba Songwe, na Ikolo wanakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya ni lazima nitoe shukrani kwa mambo makubwa yaliyofanyika Kyela. Barabara ya Ibanda - Itungi Port kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, imekuwa kuwekewa saini pale Kyela, na ndipo tulipoanzia. Hii ni historia kubwa Kyela kuanzisha na haya ni mapenzi ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kumtuma Waziri kuja hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi yanayoenda kufanyika. Tunaanza kujenga barabara ya Katumba – Songwe – Ileje ambayo tayari imeshaanzia upande wa Ileje inarudi huku; hii ni heshima kubwa. Vilevile kuna madaraja makubwa kama Daraja la Ipyana, Daraja la Bujonde pamoja na Daraja la Irondo; haya ni mambo makubwa ambayo tunafanyiwa shukrani nyingi sana. Pamoja na hayo nimeona leo nitoe pongezi kwa Waziri na Wizara yake kwamba kwa mara ya kwanza sasa nchi yetu inaanzisha mfumo mzuri sana wa ujenzi wa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nimeona leo nitoe pongezi kwa Waziri na Wizara yake kwamba, kwa mara ya kwanza sasa nchi yetu inaanzisha mfumo mzuri sana wa ujenzi wa barabara pamoja na sehemu nyingine za bandarini. Haya yote yanatokea kwenye mfumo wa PPP. Ningeomba hata hii EPC + Finance bado tuiache nyuma tukimbilie kwenye PPP, kwa sababu moja tu kwamba, huu ndio mfumo ambao uko duniani kote, yaani habari ya mjini, habari ya dunia ni PPP. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe Mheshimiwa Waziri mfano mmoja, Bandari ya Hamburg, Wajerumani wanaita Hamburg Hafen, ni bandari ambayo wao wenyewe kwa heshima wanaiita Das Tor zur Zukunft, maana yake ni lango la kwenda to the future, a door to the future. Pale yupo mtu mmoja anayeitwa CSCO (Chinese Shipping Company), wanaendesha terminal ya container pale, lakini ukienda Rotterdam pale CSCO wapo. Wajerumani walikuwa wanajiuliza hivi tumeuza bandari hii kwa Wachina?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujerumani wamesema hapana. Mfumo wa sasa ni wa kuendesha kwa pamoja Serikali na wawekezaji. Nataka nimwambie Waziri tunampigia makofi kwa kuingia kwenye mfumo huu, ataitoa Tanzania ilipo kwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunataka tutoke kwenye bandari twende kwenye barabara. Mfumo wa sasa wa ujenzi wa barabara kwa pesa tulizonazo hatutaweza kusonga mbele kwa kutumia pesa za nchi hii, ni lazima tuweke uwekezaji na tunashukuru tayari umeshaanza. pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri. Pamoja na pongezi hizi naomba sana baadhi ya mambo yafanyike kwa ufanisi na tuendelee kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mbeya ni Mkoa mkubwa sana, lakini ni Mkoa ambao mazingira yake ni tofauti kabisa na mikoa mingine. Ninachokiomba ni kwamba, tunapojadili na Mheshimiwa Waziri anapofikiria juu ya kutoa bajeti kwa Mkoa wa Mbeya, kwa barabara za Mkoa wa Mbeya, asiwaze jinsi ya kugawa, hebu afikirie mambo mawili tu makubwa, aangalie jiografia, lakini angalia terrain ya Mkoa wa Mbeya. Ukishuka kule Kyela, Kyela iko chini ya maji, ili ujenge barabara unahitaji ujaze mita mbili ndipo barabara ipitike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka Kyela kilometa 50 tu, ukipandisha Rungwe, ukifika Mbeya, barabara inahitaji ukate milima mita sita, haya hayatokei mahali pengine, yanatokea Mbeya na ndio maana nataka nimwombe Mheshimiwa Waziri, leo hii barabara imeshindwa kutoka Matema kwenda Ikombe na niliwahi kusema hapa, watu walishangaa kwamba, hii ni Tanzania au uongo na kuna watu walinifuata wakaniuliza unachokisema ni kweli?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwaambia Kijiji cha Ikombe tangu kuumbwa kwa dunia hawajawahi kuona gari, watu wakashangaa. Nataka niseme ni kweli hakuna gari, lakini kibaya zaidi tangu tumeanzisha dunia hii kila Mbunge anayeenda kule analiliwa kilio akifika, mimi naanza kuogopa kwenda; nimeenda mwezi juzi, wananchi badala ya kunipokea wakaanzisha misiba, hiyo misiba ni ya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni misiba ya akinamama ambao walishindwa kujifungua kwa sababu Ziwa lilichafuka wakashindwa kuja Matema, akinamama wamefariki na mimba. Hii ni nchi ya Tanzania ambayo inaendeshwa na mwanamke mwenye uchungu. Nataka niombe, Barabara ya kutoka Matema kwenda Ikombe, tafadhali sana wananchi wamelia wamechoka, hatutaki tuendelee na misiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ninayoyasema wananchi wanayasikia na Tanzania sasa iangalie. Kuna sehemu ambazo ni lazima ziwe za kipaumbele pamoja na kwamba, bajeti ni finyu, lakini wapo wananchi ambao wanahitaji huduma hii kwa umuhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naomba kuunga mkono hoja hii. (Makofi)