Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na mimi niungane na Wabunge wenzangu kutoa pongezi nyingi sana kwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Mawaziri wote kwenye sekta hii na wataalam wote kwa namna ambavyo wamejipanga katika kuhudumia uchumi wa nchi hii. Niwape hongera sana wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa Jimbo langu la Sikonge, nitoe shukrani za dhati kabisa. Mwaka 2022 Waziri alimleta Mheshimiwa Rais, kuzindua barabara ya Tabora hadi Mpanda. Wananchi wa Sikonge wanatoa shukrani kubwa sana kwa barabara ile, lakini kuna barabara nyingine ambayo mmetujengea kutoka Sikonge – Mibono hadi Kipili na barabara nyingine mmeendelea kuimarisha kutoka Tutuo hadi Usoke. Kwa hiyo, kwa kweli kwa Wizara hii tunatoa pongezi nyingi na shukrani nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi niseme kwamba wawekezaji, wafanyabiashara, wenye viwanda, wakulima wanaendelea kuitegemea sana Wizara hii kwa ajili ya kushusha gharama za usafiri na usafirishaji. Kwa hiyo, juhudi zote ambazo mnazifanya zina impact kubwa sana kwa Watanzania. (Makoifi)
Mheshimiwa Spika, nadhani hiyo ndio maana Serikali imekuwa ikiboresha miundombinu yake kwa mfano Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Mtwara, Bandari ya Tanga na Bandari za kwenye maziwa kama Mwanza na Kigoma. Hizi juhudi ambazo mnaendelea nazo mimi nawaungeni mkono na wananchi wangu wa Sikonge wanawaungeni mkono kwa ajili ya mafanikio ya uchumi wa nchi yetu. Tunategemea sana hizi bandari ziwe na ufanisi. Hatuwezi kuwa na ufanisi kwa kutegemea sekta ya umma peke yake. Kwa hiyo, ni muhimu sana kuchanganya sekta ya umma na sekta binafsi ili kupata matokeo bora zaidi. Hawa jamaa wa Dubai Port naamini watasaidia sana kuboresha utendaji kwa sababu wana uzoefu mkubwa sana duniani na nadhani kule ambako wamefanya kazi wameweka rekodi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile nipongeze uboreshaji wa viwanja vya ndege katika nchi hii unaonendelea, lakini vilevile ujenzi wa reli ya viwango vya Kimataifa hasa reli ya SGR ambayo itaongeza mzigo unaosafirishwa kutoka takribani tani 400,000 za sasa hivi mpaka tani zaidi ya milioni 10. Hiyo itakuwa ni faida kubwa sana kwa uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile ujenzi wa barabara za lami na madaraja makubwa. Hii ni mchango mkubwa sana kwenye uchumi wa nchi yetu. Maendeleo kwenye sekta hizo ukichanganya na maendeleo kwenye sekta nyingine, kwa mfano sekta ya umeme limekamilika Bwawa la Mwalimu Nyerere na LNG kwenye gesi. Vile vile, Mradi kama wa ujenzi wa VETA kwenye halmashauri zetu za wilaya ambao utachangia sana upatikanaji wa nguvu kazi yenye ujuzi kwenye viwanda ambayo itazidi kuvutia wawekezaji katika nchi hii. Kwa hiyo, nawapeni moyo endeleeni kuchapa kazi, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwa na maoni kwenye maeneo machache hasa kwenye eno la barabara. Kwa mujibu wa mpangilio wa barabara nchini ambao unatambulika kimataifa, barabara zetu za kiwango cha lami hizi ndefu zimepangwa katika herufi “T” zamani kulikuwa na herufi A, B, C lakini sasa hivi wamebadilisha ziko kwenye herufi “T” kwa maana ya trunk road.
Mheshimiwa Spika, barabara ambazo zimepangwa kwenye herufi “T” ziko zaidi ya 23 na mimi napenda kuzungumzia barabara ambazo zina matatizo makubwa na zimejengwa kwa muda mrefu na mpango wa kuzikamilisha hivi karibuni bado haujaonekana kwenye bajeti.
Mheshimiwa Spika, hapa nazungumzia barabara mbili; barabara ya kwanza ni barabara ambayo inajulikana kama (T – 8) kwa maana ya trunk road number 8 ambayo inaanzia Ziwa Victoria pale Mwanza, inapita Nzega inakwenda Tabora, Ipole, Rungwa, Makongorosi, Chunya, Mbeya inakwenda mpaka Tunduma kwenye mpaka wa Zambia. Barabara hii urefu wake ni kilometa zaidi ya 1000. Pia kwa miaka 40 iliyopita maana ilianza kujengwa kule Mwanza mwaka 1992, kwa miaka kama 40 iliyopita zimejengwa kilometa 549 tu kwenye barabara hii, ina maana kilometa 430 hazina mkandarasi yoyote mpaka sasa hivi. Sasa tunapanga kujenga barabara hii kwa miaka mingapi? Je, miaka 100? Miaka mia ngapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwa naomba barabara hii ipewe kipaumbele. Kumekuwa na vipaumbele vinawekwa kwenye barabara hii kwa mfano, tawi la kutoka Ipole – Mpanda limekwishajengwa, hongera sana Serikali, tawi la kutoka Mkiwa – Itigi mpaka Rungwa nalo tayari limeanzwa kwa kilometa 50... (Makofi)
Naomba barabara hii ipewe kipaumbele inaunganisha mikoa zaidi ya mitatu. Mimi naomba Serikali muipe kipaumbele barabara hii na kwa kweli kama hakutakuwa na maelezo ya kutosha kwa kweli mwishoni huko itabidi nishike mshahara wa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, barabara nyingine ambayo ningependa kuizungumzia ni barabara bamba T9; hii barabara inaanzia Biharamulo – Lusahunga – Nyakanazi – Kibondo – Kasulu - Kanyani ifika pale inakata kona inakwenda Uvinza - Mpanda, Sumbawanga - Tunduma mpakani mwa Tanzania na Zambia. Barabara hii nayo ni zaidi ya kilometa 1000, barabara hii vipande ambavyo havina mkandarasi kabisa ni viwili, kutoka Kanyani mpaka Uvinza kilometa 57 na kutoka Ruhafu mpaka Uvinza kilometa 134 jumla kilometa 191. Hii nayo ni barabara muhimu sana katika nchi hii. Wekeni vipaumbele kwenye hizi barabara ndefu ambazo zinashikilia uchumi wa, nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama barabara ya (T8) ingekuwa imejengwa, kiwanda cha nguo cha Mbeya Textile kisingekufa. Kwa sababu kingepata supply ya pamba kutoka Mwanza, kutoka Shinyanga. Kilikufa kiwanda kile kwa sababu namba T8 ilikuwa haijajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la kutokuwa na wakandarasi mpaka leo barabara hiyo, mimi nilikuwa naomba sana Serikali kwa ujumla wake iweke kipamubele kwenye hizo barabara ili kusudi wananhi wa nchi hii waweze kuhudumiwa vizuri kiuchumi. Kwa sababu sehemu zote hizo kuna shughuli za kiuchumi. Sio kwamba kule ambako kunajengwa tu ndiko kuna uchumi huku hakuna. Kote kuna shughuli za kiuchumi. Kwa hiyo, naomba sana na hayo ndiyo ya muhimu zaidi mimi mengine sina.
Mheshimiwa Spika, juzi nilikuwa Sikonge, wananchi wa Sikonge wakanituma nenda kapiganie barabara hii vinginevyo hatutakuelewa. Sio kwamba hawatanielewa mimi tu, hata Serikali hawataielewa. Mimi naomba sana ili tuelewane vizuri wekeni kipaumbele na naomba commitment kubwa. Mheshimiwa Waziri, anaposimama hapo naomba commitment kubwa kuhusiana na barabara hizi mbili T8 na T9. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)