Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nimshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia, lakini pia niipongeze Serikali kiujumla kwa kazi ambayo wamefanya tangu walipoingia madarakani mpaka leo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia upande wa TAMISEMI tunaelewa kabisa bajeti ya TAMISEMI ni trilioni sita ambayo ni wastani wa asilimia 20.4 ya bajeti nzima ya Serikali. Kwa hiyo, inaonesha ni jinsi gani TAMISEMI imebeba mambo mengi ambayo yanafanya huduma za jamii na mambo yote kwa karibu sana na wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuna mambo ambayo ningependa kuchangia katika kuishauri TAMISEMI. Jambo la kwanza upande wa kilimo; mwaka jana wakati wa kampeni Mheshimiwa Rais aliahidi kushughulikia masuala ya wakulima kulipwa fedha zao taslimu badala ya kuendelea kukopwa na Vyama vya Misingi na hawa mawakala wa mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuiombe sasa, kwa kupitia Wizara yetu hii wamkumbushe au Wizara yenyewe ichukue wajibu wa kuliona suala hili kwa kushirikiana kiujumla katika Serikali waone wanalichukulia vipi. Tumekuwa na matatizo ya ruzuku, Serikali imejitoa, kwa namna nyingine tunaweza kusema maana bei za pembejeo zilipanda karibu mara mbili, sasa watu wetu wanakwenda kufanikiwa vipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika masuala ya wakulima ni bajeti ambayo tunaomba iongezwe na mpango bora wa matumizi ya ardhi ili wakulima wetu waweze kupata maeneno mazuri yenye rutuba na kuweza kufanikisha masuala yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la elimu. Binafsi Jimbo langu la Nsimbo hatuna A-level, kwa hiyo, katika maombi yetu kwenye hii Bajeti tunahitaji tuwe na A-level maana shule za sekondari tunazo takribani tano. Kwa hiyo, tunaomba tupate hiyo sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba aliyotoa Mheshimiwa Waziri ameonyesha tuna vijiji vingi na vingi havina zahanati; mojawapo ni vijiji vilivyopo katika Jimbo la Nsimbo na tukizingatia kwamba Jimbo langu ni moja ya Jimbo ambalo lilikuwa lina makazi ya wakimbizi wanaotoka nchi jirani ya Burundi, kwa hiyo, huduma za kijamii zinahitaji kuboreshwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika yote hayo kuna jambo ambalo ni zuri sana na ni la muhimu katika maisha ya wananchi, ni kuhusu maji. Halmashauri yangu ilikuwa na bajeti mara ya kwanza shilingi bilioni 1.6 ya miradi ya maji. Serikali ilivyoshusha ceiling ikaenda shilingi milioni 703. Takribani wiki moja iliyopita ceiling imetoka shilingi bilioni 16 imeenda shilingi bilioni 14. Tumepewa ceiling mpya na ceiling hii inalingana na bajeti ya mwaka huu wa fedha 2015/2016. Maana yake hatuwezi kuajiri, hatuna miradi ya maendeleo ambayo mwaka huu haijatimizwa, imeingia kwenye bajeti mpya ya mwaka 2016/2017. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali bora tupunguze fedha za maendeleo katika maeneo kidogo kama ya barabara na sehemu nyingine, lakini sehemu muhimu ya maji tuweze kuongeza fedha ili wananchi wetu wapate maji kwa sababu maji ni muhimu sana na ukikosa maji hayana mbadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie suala zima ambalo lipo katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuhusu mawakala kuondolewa asilimia 100 muda siyo mrefu ujao. Naomba ni-declare interest kwamba nina uzoefu kidogo katika eneo hilo, mimi mwenyewe ni wakala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la dhana ya kuweka mawakala ilikuwa ni kudhibiti mapato ambapo watumishi wa Halmashauri zetu walikuwa wanayapoteza kwa njia mbalimbali; aidha, kwa kuwa na vitabu hewa au kubadilisha zile nakala kutoweka copy, ndiyo maana Serikali iliamua kuweka mawakala. Pia tumeona kwamba kuna tatizo katika kuweka mawakala hawa na kutumia hizi electronic machine, tumeona Mtwara na Arusha kulingana na kwa hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeonesha improvement kubwa kwamba mapato yameweza kuongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopo kuna baadhi ya aina ya ushuru zitaleta shida sana. Kwa mfano, ule ushuru mdogo mdogo kwenye masoko, utatuletea taabu sana, maana yake itabidi tuongeze rasilimali watu kwa ajili ya kukusanya. Tuna ushuru mwingine wa mazao ya asili ya misitu, mazao ya biashara, mazao ya chakula na movement ya yale mazao, ndiyo maana katika hizi Halmashauri kuna mageti yanayofanya kazi saa 24, siku saba kwa wiki, mwezi mzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maana yake, Halmashauri itabidi iajiri na tukiajiri zaidi watu tunaongeza gharama za staff, ndiyo hiyo mishahara na gharama nyingine ambazo zinahusiana na watumishi. Kwa hiyo, tuishauri Serikali, tunaunga mkono wazo hili, lakini tunaomba maeneo mengine ambayo kuna changamoto ya ukusanyaji, basi tuendelee kutumia mawakala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna mfano dhahiri; kuna baadhi ya maeneo tumepeleka watumishi wetu wamekwenda kukusanya, unakuta makusanyo yanakuja tofauti na wakala alivyokuwepo. Kwa hiyo, japokuwa tutatumia hizi electronic machine, lakini tuangalie namna ya kuimarisha udhibiti wetu wa ndani yaani internal control, lazima tuimarishe. Yawezekana ushuru wa shilingi 5,000 mtu akamkatia shilingi 2,000; lakini kwa sababu ni ya kielektroniki na imejisajili kule TRA, sasa sisi tutaona tumedhibiti lakini kumbe kuna njia nyingine ambayo tutaendelea kuporwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la kiutendaji katika Halmashauri. Mfumo wa kuandaa hizi bajeti kwenye Halmashauri yetu unatuongezea gharama na tunashindwa kuboresha huduma za jamii. Mfano mzuri, Halmashauri yangu mwezi Februari posho za kulala nje na movement zote katika kuandaa hii bajeti wametumia shilingi milioni 29. Sasa Serikali imewekeza katika Mkongo wa Taifa, tuangalie katika kutumia teknolojia na katika movement za Halmashauri zote 181 ambapo wote wanakuja Dar es Salaam ndiyo wapewe zile ceiling, wanaingia gharama kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama uongozi wa Mkoa ndiyo huo wenyewe ulete zile Bajeti na Serikali itoe zile ceiling ambazo ndiyo zenye ukomo. Maana leo inatoa ceiling ya kwanza, siku nyingine tena ceiling ya pili, kwa hiyo, tunakuwa na movement nyingi za watumishi wetu kuja Dar es Salaam. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali ikitoa ceiling iwe imetoa ili watu wasiwe wanakuja Dar es Salaam mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la kanuni za kudumu za Halmashauri, kwani zimekuwa zinakingana na miongozo inayotolewa na TAMISEMI. Kwa mfano, kuna mwongozo ulitoka takribani mwaka uliopita au mwaka juzi, unaelekeza Kamati za kudumu katika Halmashauri kama tatu, lakini kanuni inataja Kamati zote tano ni za kudumu. Sasa kipi kinafuatwa; kanuni za kudumu zilizopo au ni miongozo? Kwa hiyo, tuone ni jinsi gani iweze kuboreshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kuhusu fedha za majimbo zinagawanywa kwa kufuata masuala ya umaskini, idadi ya watu na ukubwa wa eneo. Kuna majimbo mengine ni makubwa lakini yana idadi ndogo ya watu, kwa hiyo, uwiano hapa hauendani kabisa. Bora tuondoe suala la ukubwa wa jimbo, tutumie idadi ya watu, hali ya umaskini ili kuwe na uwiano mzuri kwa kugawana hii rasilimali. Njia nzuri, tutumie hata ile weighted average ili Majimbo yetu yapate fedha kulingana na hali halisi iliyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na tunaomba sana bajeti yetu na kikubwa zaidi Halmashauri yangu ipandishwe bajeti yake kutoka shilingi bilioni 14 mpaka shilingi bilioni 18 ili tuweze kukidhi mahitaji katika Jimbo. Ahsante sana.