Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu katika kulipongeza Jeshi letu kwa kazi kubwa wanayofanya, hasa kuhakikisha usalama wa nchi yetu na ulinzi wa nchi yetu tunakuwa salama sana.

Mheshimiwa Spika, leo ningeomba niongelee kipengele cha JKT, yapo mambo mengi yanatuumiza akili, tunachanganyikiwa hatujui tunafanya nini, kumbe tuna vyombo humu ndani ambavyo hatujavitumia sawa sawa na kama tungevitumia matatizo yetu makubwa yanayotukosesha usingizi, mambo kama ajira kwa vijana, mambo kama maadili kwenye Taifa letu, mambo kama uzalendo, mambo kama ukakamavu, tayari tungekuwa tumeweza kwa kiasi kikubwa sana kuyatatua.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amesoma utekelezaji wa Ilani kile kipengele (H) na wote hapa tupo kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, na Chama cha Mapinduzi kina viongozi makini wenye uelewa mkubwa wanaoona mbali sana. Wametuelekeza au wamekuelekeza Mheshimiwa Waziri katika utekelezaji wa Ilani (H), kuimarisha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) ili viwe vyombo vya kuwapatia vijana ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa na pia kuwa vyombo mahiri vya huduma na uzalishaji mali hasa katika ujenzi wa kilimo, ufugaji, uvuvi na maeneo mengine. (I) inasema hivi, ili uweze kutekeleza hilo (H) lazima sasa kupanua na kuongeza idadi ya Kambi za JKT na JKU. Ili kuwezesha vijana wengi zaidi, wakiwemo wahitimu wote kwa sababu JKT ina makundi mawili ya vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna vijana tunawachukua kwa mujibu wa sheria na tunao vijana tunaowachukua kwa kujitolea. Wale wa kwa kujitolea ndiyo Ilani inasema kuwawezesha wengi, wale wa mujibu wa sheria Kidato cha Sita ni wote. Utalitekelezaje hili lazima uhakikishe kwamba unapanua na kuongeza Kambi za JKT na JKU.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ukisimama hapa utuambie safari hii unafanya nini katika kuongeza makambi, tunataka vijana wote wanaomaliza Kidato cha Sita waende JKT. Tunataka uongeze idadi ya vijana walioko mitaani waende JKT, kwa sababu JKT kwanza ina majukumu, objectives zake iliyopewa. Objective ya JKT namba moja ni malezi kwa vijana wetu, objective nyingine ni kuzalisha mali, kuwafundisha vijana wetu kuondokana na mentality ya kufikiria kwamba kazi za ofisini ni bora kuliko kujiajiri, kuzalisha mali lakini ni ulinzi wa Taifa letu. Kutoa mafunzo ya uhakika kwa vijana wetu kuhakikisha kwamba wanakuwa wazalendo, wakakamavu, kuendelea kulinda Taifa letu. Malezi ya vijana, kuwa na vijana wenye nidhamu, wakakamavu, wenye kujitegemea, wenye uwezo wa kufanya kazi ili kuleta maendeleo kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumbe ni wakati muafaka sasa kama alivyosema kaka yangu Mheshimiwa Kingu, kumbe Wizara nyingine hizi zilitakiwa zifanye coordination na JWTZ na JKT kupeleka programu zao waseme sisi tunayo programu ya kuwafundisha vijana kupitia BBT hawa hapa. Kwa sababu Mheshimiwa Waziri kinachosumbua sasa hivi kwa vijana wetu, shule tumejenga nyingi, vyuo vingi ujuzi wanao, kinachosumbua ni ukakamavu, ni nidhamu na kujitegemea, hivi watavipata kule! Tunao Maafisa Kilimo yes, tumewadahili kwenye vyuo vya kilimo lakini Afisa Kilimo anaogopa nyoka, na nyoka wanaishi mashambani, akapate ukakamavu jeshini. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, tuna vijana tumewafundisha sasa hivi tumewapelea BBT watajifunza vizuri na mimi nashukuru nimetembelea kituo kimoja wanafanya vizuri lakini akishika jembe, akinyanyua tu jembe analiangusha lina mkata, ukakamavu haupo. Tunao vijana wengi tunawafundisha au tunawadahili wanakwenda vyuo vikuu wanamaliza form six, wanakuwa wasomi wazuri, madaktari wazuri lakini uzalendo hakuna. Mtu anaona bora mgonjwa afe yeye akimbie na dripu akauze. Kwa hiyo, kumbe mwarobaini wetu ni JKT na wazazi wetu waliliona hilo na ndio maana nikawa najiuliza ni kwa nini Waziri Mkuu Hayati Rashidi Kawawa aliamua kwenda JKT, ni kwa nini Mzee Aboud Jumbe aliamua kwenda JKT, ni kwa nini Mzee wangu mimi Adam Sapi, Spika wa kwanza wa Bunge hili aliamua kwenda JKT. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule ndiko alikopata uzalendo na ukakamavu, wakajifunza nidhamu, leo tuna vijana tumewaendeleza sayansi na teknolojia Mheshimiwa Nape alikua anazindua minara 700 tunaweka huko lakini wengine wanatumia tu kutukanana au kutukana viongozi wetu au kui - defend Serikali yetu. Tusipowapeleka hawa JKT kujifunza uzalendo haina maana uwekezaji tuliofanya.

Mheshimiwa Spika, Serikali lazima mkae kama kitu kimoja mkubaline kwamba chombo kilichopitishwa kisheria na Bunge Tukufu kwa ajili ya malezi rasmi ya vijana wetu ni JKT, hatuhitaji tu akili za darasani Intelligent Quotient, ukishamjengea mental structure tunahitaji physical structure yake kwenye performance. Ana akili nzuri ni Afisa Kilimo mzuri lakini kuna mahali atatakiwa a - demonstrate ashike jembe achimbe, amuoneshe mkulima namna ya kufanya lazima huyu awe mtu makini, awe mtu mkakamavu, awe mtu mzalendo, awe ni mtu mwenye nidhamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, JKT lazima iwezeshwe Waheshimiwa Wabunge, hiki ndiyo chombo kinachotuunganisha vijana wetu kama Taifa pekee yake. Huku kwingine tukiungana tunaungana kama Vyama vya Siasa, tunaungana kama CCM, tuna green brigade wetu, wanaungana kama CHADEMA wana red brigade. Huku ndiko tunakounganishwa kama Watanzania, tunaongea maslahi ya Watanzania, huku ndiko tunapelekwa bila ukabila, huku ndiko tunakopelekwa bila kujali itikadi za imani zetu. Tunakwenda kuambiwa sisi ni Watanzania we are blessed to be Tanzanians, tunaijenga Tanzania. Vijana wetu lazima wakue na mentality hiyo, wasifikirie tu kuona kwamba nchi zingine wanafanya vizuri, wanaishi vizuri natamani kutorekea huku, natamani kutorekea huku. Haina maana nchi hii, humu humu ndiyo nchi ya asali na maziwa hapa hapa.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana JKT, halafu kulala kule JKT namshukuru Mungu alinipa privilege nikaenda. Majengo ya JKT wala hayahitaji gharama kubwa wala is not a mansion kama hili Bunge letu. Wao wanapiga tu yale mahanga, bati na nini na nini, Waziri utuambie ukija hapa, CCM imekuelekeza hapa, wewe unajenga kambi ngapi? Vijana wengi tunataka kuona wanapungua mitaani unaniambia…

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Ninataka kuona unanimbia Mheshimiwa Jesca leta vijana toka Iringa tuwapeleke JKT, wakajifunze uzalishaji mali, uzalendo na jinsi ya kulitumikia Taifa na kujitegemea wao wenyewe.(Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Jesca Msambatavangu kengele ya pili imeshagonga.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)