Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Kwa niaba ya Wananchi wa Tarime Vijijini, Wananchi wa Tarime na Wananchi wa Mkoa wa Mara tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka shangwe kubwa katika Mkoa wa Mara, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Mungu ambariki sana aendelee kuwa na sikio la kusikia kilio cha wanyonge na hasa kutoka Mkoa wa Mara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Wizara ya Ardhi ina changamoto nyingi na niwe mkweli, mimi ni miongoni mwa watu ambao wana migogoro mingi yaani kule Mkoa wa Mara lakini na mikoa mingine. Kwa hiyo la kwanza nimwombe Mheshimiwa Waziri awe na ngozi ngumu katika eneo hili. Ameshikilia kura za Chama cha Mapinduzi, ameshikilia kura za Mheshimiwa Rais, ameshikilia kura za sisi Wabunge kurudi hapa Dodoma kuendelea kukalia kwenye viti hivi. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri ni lazima ajipange vizuri katika eneo hili. Huo ndiyo ukweli wa Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Katiba yetu ya Mwaka 1977, Toleo la Mwaka 2005 Ibara ya 8 naomba ninukuu Ibara ya 8(1).
“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo:-
(a) wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata mamlaka na madaraka yake toka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii;
(b) lengo kuu la Serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi;
(c) Serikali itawajibika kwa wananchi;
(d) wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hii ibara kuonyesha kwamba kitendo cha kutotatua migogoro vizuri ya ardhi kinawakwaza wananchi walio wengi na hao wananchi wanaipenda Serikali yao. Maendeleo yote ambayo yanafanyika na Mheshimiwa Mama Samia ni kwa ajili ya wananchi. Mheshimiwa Waziri katika eneo hili, lazima ibara ya 8 hii niliyosoma izingatiwe sana. Maana yake katika mipango yote ya Serikali ya ardhi lazima tuangalie haki za watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika maeneo mengi kule Tarime, Wizara ya Ardhi ndiyo inamiliki Mthamini Mkuu wa Ardhi. Akishafanya tathmini ya ardhi, wanawasiliana na Wizara ya Madini, halafu mgodi unaambiwa kwamba ulipe. Nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba, kitendo cha watu wa Tarime maeneo ya mgodi chini ya ardhi kuna dhahabu, wanalipwa ekari moja shilingi milioni tano, bei ambayo hata ukienda mtaani Tarime huwezi kununua ardhi ekari moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo hicho kinafanya tufikirie zaidi, kwa nini eneo ambalo chini kuna dhahabu unalipa ekari moja shilingi milioni tano sawasawa na ardhi ambayo unaweza kufidia ujenge choo au ujenge zahanati? Wizara haioni kuna sababu ya msingi sana kuangalia viwango vipya vya bei ya ardhi na hivyo ndiyo vinapelekea migogogro mingi kwa sababu wananchi wanajua ukishatoa ardhi yetu unaenda kuchimba dhahabu au vito vingine na unapata fedha nyingi zaidi. Hili ni vizuri pia likaangaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile migogoro ya ardhi, Waheshimiwa Wabunge nataka nishauri, ukisikiliza vizuri Hotuba ya Kamati yetu wanasema fedha zilizotengwa kwenda kutatua migogoro ni kidogo ukilinganisha na fedha ambayo imepelekwa kwenda kulipana posho, allowance, mafuta na vitu vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwashawishi Waheshimiwa Wabunge, katika eneo hilo Mheshimiwa Waziri lazima atuambie tubadilishe sisi hapa ndiyo Watanzania. Fedha nyingi iende kutatua migogoro ili uchaguzi ujao Chama Cha Mapinduzi kisiadhibiwe ili uchaguzi wa Mama Samia 2025 tupate ushindi wa kishindo. Hatuwezi kushinda vizuri uchaguzi kama watu wanaenda kwenye uchaguzi na vinyongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna taarifa, Kamati ilimwita Mheshimiwa Waziri na Mwenyekiti hapo yupo, wametusomea Waheshimiwa Wabunge, tusome Taarifa ya Kamati, tuunge mkono Waziri atueleze, kwa nini aliamua kupanga fedha kidogo ya kwenda kutatua migogoro kwenye majimbo yetu na fedha nyingi kwenye safari na posho? Hilo ni muhimu sana tukaambizana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme hii migogoro kwa mfano kule kwangu, leo tunapozungumza ukizungumza habari ya Komarela, Kewanja na Nyamichere, Mthamini Mkuu wa Serikali ameenda ametoa notisi kwamba watu eneo hili msiendeleze, halafu baada ya muda fulani anaambiwa kwamba usilipe. Wakati fulani wanafanya tathmini ambayo wanalalamikiana. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri akijipanga vizuri maana yake kwangu na Wabunge wengine migogoro ya fidia itakwisha. Kwa sababu watu wake ndiyo wanafanya kazi ya uthamini katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina migogoro ya ardhi ile ya Komarela na mgodi, nina mgogoro wa ardhi Mheshimiwa Waziri wa siku nyingi kwa Korutambe na Remagwe, nina mgogoro wa ardhi pale Kebweye na Kyoruba, nina mgogoro wa ardhi Mwito na Msege, nina mgogoro wa ardhi Mwito na Gibaso, nina migogoro mingi ambayo hii inapelekea amani isiwepo na watu wanapoteza imani. Mheshimiwa Waziri anayo kazi hiyo, Mheshimiwa Rais amempa kipande muhimu kweli kweli, awe mpole apokee maoni, awe humble, asikilize na atatue migogoro na timu yake aiambie kwamba kule kuna wananchi ambao lazima wasikilizwe vizuri ili kuondoa changamoto tulizonazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri, katika utatuzi wa migogoro wamesema kamati hapa, tunajua kuna Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999, lakini vile vile tuna Sheria ya Fidia ya Ardhi ya mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2018, lakini ushirikishwaji. Wasiende kusoma document kama zilivyo kwa wananchi wa kawaida, wanawaamrisha. Waende kwenye vijiji, waite Viongozi wa Vijiji, Wabunge na Madiwani watushirikishe tuwape maoni. Tukienda kutatua mgogoro hatumwachii Waziri peke yake, tunataka mgogoro ukitatulika, Serikali inufaike na wananchi wanufaike na amani itawale na maendeleo yapatikane katika eneo husika, tusiamrishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Kamati kwamba jambo hili wameliona na ndicho kilichofanyika katika maeneo mengi sana, lakini pia kamati imeomba kwa kuwa na mimi naunga mkono, Taarifa hiyo ya Mawaziri nane ije hapa Bungeni, kila mtu aone eneo lake walipitia wapi, GN inasema nini, tusome tuweze kuwashauri. Hatuwezi kuwa Wabunge tena sehemu ya kulalamika, wakati sisi ndiyo wasemaji kwa niaba ya Watanzania ambao walituamini kuja hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwombe Mheshimiwa Waziri, walipokuja Tarime kule, msoma ramani wake alisema ile GN ya mwaka 1968 ina ramani (surveyed map) ya mwaka 1968. Wakasema hii ramani kwa haraka haraka tumeacha kwenye gari, tukienda kwenye mkutano tutawapa. Inaombwa tangu siku ile mpaka juzi, mpaka jana, mpaka leo haipo. Tunahitaji Tarime pale kwenye ile migogoro ya ardhi tupate GN ile tunayo ya mwaka 1968, tupate ramani, (surveyed map) ya mwaka 1968 mjadala uanzie hapo ili kuweza kuondoa mzizi wa fitina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mapendekezo hapa kwa Mheshimiwa Waziri. Migogoro ya ardhi iliyopo, ukienda Nanyumbu kuna mgogoro, ukienda Kiteto kuna mgogoro, ukienda sijui wapi kuna mgogoro. Mkoa wa Mara kuna mgogoro wa ardhi pale Rorya, Serengeti, Bunda pale Nyatwali, Tarime Mjini na Vijijini. Hii migogoro huu ni Mkoa mmoja wa Mara. Sina taarifa nzuri ya mikoa mingine. Nataka nimwombe tena Mheshimiwa Waziri, shemeji yangu, mke wangu ni Msukuma, Waziri mwenye nguvu kubwa tunaomba sasa aonyeshe Udaktari wako kwenye kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani tunapoenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa atumalizie migogoro ya ardhi kwa watu wetu. Tunatamani uchaguzi wa mwakani tusihukumiwe kwa sababu ya migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuombe pia kwenye kiti hicho, ni vizuri Wabunge tusome Ripoti ya Kamati hii, tuisimamie Serikali, tuishauri vizuri. Mheshimiwa Rais ameshampa dhamana Mheshimiwa Angeline Mabula kutatua migogoro ya ardhi.Naomba Mheshimiwa Waziri avae kiatu kimtoshe afanye kazi ya kutatua migogoro hii. Tumechoka kulalamikiana na kuja kulia katika Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja hasa Ripoti ya Kamati ije Bungeni tujadili ili Watanzania wapate amani ya kwao. (Makofi)