Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mimi leo nitajikita Jimbo la Kawe zaidi, kwa sababu naona kama Kawe kuna kaombwe hivi, sasa ninaomba Mheshimiwa Waziri unisikilize kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, katika ukurasa wako wa 78 umezungumzia miradi ya 711 na umesema kwamba utakamilisha miradi mikubwa iliyosimama ya Kawe 7/11 na Golden Premium Residence. Vilevile wataendeleza mradi wa Samia Housing Scheme Kawe. Sasa nilitaka unipe maelezo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu seven eleven one ilikuwa na thamani ya Shilingi bilioni 142, na Seven eleven two Shilingi bilioni 103. Nilitaka kufahamu ukamilishaji una lengo la kukamilisha asilimia 100 ama kiwango gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mwaka ulioishia Juni, 2018, alisema wazi kabisa kwamba kutokana na miradi hii kukwama likelihood 2018 nazungumza; likelihood ya Serikali kupata hasara ya Shilingi bilioni 99.9 kipindi kile, lakini kuna hasara nyingine ya Shilingi bilioni 2.6 kwa sababu kuna wananchi ambao tayari walikuwa wameshalipia yale majengo lakini hakuna kilichoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri akija naomba anijibu kwa ufanisi kabisa ili tuweze kujua ni hasara kiasi gani ambayo nchi na Serikali imepata kutokana na mradi huu kukwama toka mwaka 2017 mpaka sasa na hasa ukizingatia kwamba Shirika la Nyumba la Taifa lilikuwa linatumia mikopo ya kibiashara kwenda kukopa ili kufanya hii kazi. Uzembe huu na hasara hii kwa nchi imetokana na Serikali kuinyima kibali kwa miaka zaidi ya saba kwenda kukopa wakati ikijua hili jambio ni la kibiashara. Hilo ni la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni migogoro ya ardhi. Nashukuru leo amezungumza Mwenyekiti wa Kamati, naunga mkono hoja yake. Mwaka jana 2022 nilisema hapa, migogoro ya ardhi nchi hii, Mawaziri na watendaji wa Serikali, kwenu ninyi mnatuimia kama dili la kuzunguka kufanya ziara. Hamna dhamira hata kidogo ya kuhakikisha nchi yetu inapangiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi ili ifike kipindi tuachane na migogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2022 tuliambiwa kuna mkopo tukajinasibu sana. Leo Kamati inatuambia eti katika ule mkopo shilingi bilioni 47 ni ya posho na uratibu na kuzurura zurura huko, halafu Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi, wanapewa chini ya shilingi bilioni 10! This is nonsense! (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
Mheshimiwa Mwenyekiti, this is lack of seriousness. Haya mambo yanauma. Jimbo la Kawe Mheshimiwa ninakuomba sana, tuitatue migogoro ya ardhi kwa Mwenyekiti wa lile Jimbo. Nimeondoka siku mbili tatu, kunalipuka. Kata ya Mabwepande, Mtaa wa Mbopo, kwa ndugu yangu kule wa Kibamba, Tegeta A, Isumi, eneo lingine la Madale Jimbo la Kawe, kuna mgogoro unaofukuta wa huyu mdudu anaitwa DDC. [Neno “mdudu” Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina nyaraka hapa Mheshimiwa Waziri toka mwaka 1980 eneo ambalo DDC inadai ni la kwake lilikuwa ni eneo la Kijiji, nyaraka zote ziko hapa. Kijiji kiliwaambia kitawapa hekta 500 kwa masharti kadhaa. DDC wakaenda wakakaa kikao na Wizara ya Ardhi, wakatengenezea hati mezani, wakaja na hati ya hekta 5,000. Ndiyo maana leo tunatoka kwenye Kijiji cha Jimbo la Kawe cha Mabwepande, tunaenda kwenye mtaa mwingine wa Mabwepande wa Kata ya Kawe ambao…
Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani, napata mzuka yaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaenda kwenye kata nyingine ya Jimbo la Kawe inaitwa Kata ya Wazo Mtaa wa Madale. Mabwepande ilipo ni kata tofauti, Wazo ilipo ni kata tofauti. Tunaenda kwenye Jimbo la Kibamba la ndugu yangu kata ya Goba. Taasisi za Serikali, hiki kimdudu kinaitwa DDC toka mwaka 1980 waliambiwa tufanyieni hawa mje mlipe wananchi fidia, hawajaja. [Neno “kimdudu” Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2004 wakaja wakapiga sound. Wananchi wakawaambia makubaliano yetu yako wapi?
Juzi bahati mbaya sana wamekwenda na Mkuu wa Mkoa. Nina barua za toka mwaka 1980 hapa. Wameenda na Mkuu wa Mkoa Makala na maaskari Polisi na mitutu ya bunduki, wanatisha wananchi wa Jimbo la Kawe eti na kuwaambia tunawapora, tuwapimie ardhi upya. Yaani mimi nimeshanunua ardhi, nimejenga, unakuja kuniambia unipimie nyumba yangu nikulipe tena!
That is nonsense, that is nonsense. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge].
MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima, jaribu kutumia maneno ya Kibunge ambayo ni ya heshima.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, yanauma. Haya nafuta.
MWENYEKITI: Hata kama yanauma. Haya.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi vitu vinauma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa kaenda na jeshi lake, analazimisha wananchi, anaongea na wananchi lugha za kejeli, dharau na kiburi. Sasa nakuomba Mheshimiwa Waziri, kwanza kaa ukijua wananchi pale tumeshajipanga, hakilipwi kitu.
Pili, tunazungumza kwa eneo la Mabwepande peke yake, ni kaya zisizopungua watu 39,000. Hako kaeneo kamoja, sijamzungumzia ndugu yangu wa Kibamba, sijamzungumzia suala la kata ya Wazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shule za Umma ziko pale, kuna hospitali za Umma ziko pale, kuna miradi ya maji eneo la Tegeta A, limejengwa tanki kubwa la Umma linalohudumia Jimbo la Kibamba na Jimbo la Kawe. Leo kuna kajitu kamoja kalikuja kuomba shamba la mifugo, hajawahi kutuletea hata mbuzi, hajawahi kuleta hata kuku, miaka 40 baadaye mmempiga nyie sijui bili ya ardhi ya Shilingi milioni 4.5 anafikiria atakuja kuponea kwa wananchi? Over my dead body, hilo ni la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Bunda Mjini; Nyatwali. Ni hivi, sheria za nchi zinasema hivi, ukitaka kuchukua ardhi ya mwananchi, lazima ufidie kikamilifu na usimwache kwenye ufukara, umpeleke katika hatua aliyokuwanayo ama hatua ya juu ya zaidi. Ukisoma Katiba hiyo hapo, ibara ya 24(2) imesema, ukisoma Sheria ya Ardhi hapa part two imesema, ukija Sheria ya Utwaaji wa Ardhi imesema. Hivi kweli ni akili leo, wananchi wa Nyatwali wako pale zaidi ya miaka 700, Serikali mnakuja mnataka kutengeneza njia ya Wanyama, yaani jinsi ambavyo mnapenda wanyama kuliko watu. Mnahamisha kata nzima ya watu 13,000 unaenda unamwambia mwananchi ninakulipa fidia square meter moja shilingi 495! Halafu unasema kama una hati ninakulipa square meter moja shilingi 704! Halafu mbaya zaidi unatoa hayo makadirio yako…
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
TAARIFA
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba mchakato wa Nyatwali tunaenda kunusuru maisha ya wananchi ambapo kumekuwa na changamoto kubwa sana ya wanyama wakali na waharibifu. Kwa hiyo, wananchi wanaoondolewa pale, siyo kwa sababu eneo lile Serikali inalitaka, ni kwa sababu tunaokoa maisha ya Watanzania.
MWENYEKITI: Unapokea taarifa?
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema hivi, kwanza wananchi wa Nyatwali ni wastaarabu sana. Wamekaa pale miaka 700…
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima, umeipokea hiyo taarifa kwanza? Subiri kwanza. Mheshimiwa Halima umeipokea taarifa ya Mheshimiwa?
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja kwanza, dakika zangu zinahesabiwa kwake sasa.
MWENYEKITI: Najua. Umeipokea hiyo taarifa ya kwanza au hujaipokea?
MHE. HALIMA J. MDEE: Taarifa ya kwanza nimeipokea na reservations. Kwa nini nimeipokea? Nimeipokea kwa sababu kwa maelezo yao hao wenye meno, wananchi wanatakiwa wahame. Wananchi wamesema sawa, tumekaa hapa miaka 700, tutahama, lakini lipeni fidia kwa matakwa ya sheria za nchi yanavyosema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Nyatwali ni Bunda Mjini, halmashauri hiyo hiyo watu wanalipwa square meter kwa vipimo ni shilingi 6,000, halmashauri hiyo hiyo Kata ya jirani basi, tufanye sawa, kata nzima inaondoka. Huyu mwananchi hawezi kubaki kata hiyo, lazima anunue ardhi eneo la jirani. Eneo la jirani square meter moja ya ardhi ni shilingi 2,000 kwenda juu mpaka shilingi 3,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema ni hivi, ni bahati mbaya, halafu nasikia kuna jamaa mmoja sijui anaitwa mtathmini huyu; mtathmini mmoja anaitwa Sanga. Chief Valuer anapambana na wananchi wanafurahia sana Chief Valuer anavyopambana nao, lakini kuna haka kajitu huko kanaitwa Sanga, kanawapeleka wananchi mpera mpera. Sio Sanga wewe, siyo Sanga wewe, tulia. (Kicheko/Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima, muda wako umeisha. Malizia dakika moja.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa usahihi na kumalizia na kwa msisitizo, mmepewa dhamana. Ninarudia, ardhi ni mali ya Watanzania. Rais amepewa dhamana yaani ni trustee kwa niaba yetu. Sheria zizingatiwe, haki itendeke. Sitaki mjibu hili suala emotional. Don’t personalize matters. Don’t personalize issues. Jibuni kwa mustakabali mpana wa wananchi wa Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hayo tu. (Makofi)