Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuchangia Wizara ya Ardhi. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai tunachangia hii Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan kwa jinsi alivyoanza kushughulikia matatizo ya Wizara ya Ardhi, kwanza kwa kuunda ile Kamati ya Mawaziri Nane ili waende kushughulikia migogoro ya ardhi, lakini pili hapa juzi juzi aliweza kutoa msamaha wa riba kwenye pango la ardhi ili wananchi waweze kulipa pango lao la ardhi. Napenda pia nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa hilo, lakini niombe ikiwezekana atuongezee muda, awaongezee wananchi ili waendelee kulipa pango la ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri Angelina Mabula na Naibu wake kwa kutuletea watendaji wa Wizara ya Ardhi hapa Bungeni na sasa tunaweza kushughulikia masuala yetu ya ardhi kwa wepesi zaidi. Napenda niwapongeze watendaji wote wa Wizara ya Ardhi na hususan nitaanza na Kamishna wao Mheshimiwa Mathew kwa uwajibikaji wake wa kupokea simu haraka na kujibu message. Nampongeza pia, Mkurugenzi wa National Housing Mheshimiwa Hamad Abdallah kwa kasi mpya aliyokujanayo kwenye sekta ya national housing. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hizo pongezi ninayo masuala ya kuchangia kwenye Wizara hii. Kwanza kabisa naunga mkono hoja ya Kamati ya Ardhi, nikiwa kama Mjumbe naunga mkono mambo yote yaliyosomwa na Mwenyekiti wa Kamati yetu. Sisi kama kamati tuliona kwamba, Wizara ya Ardhi ina wajibu wa kupima ardhi na kusimamia ardhi ya Tanzania inapimwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Tume ya Mipango ya Ardhi. Tume ya Mipango ya Ardhi imekuwa ikipewa pesa ndogo sana za kupima ardhi na matokeo yake imekuwa ikishindwa kutimiza wajibu wake wa kupima ardhi na hatima yake ni uzalishaji wa migogoro kwenye masuala ya ardhi kwa wafugaji na wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana wakati tunapitisha bajeti hapa tuliomba tume iongezewe pesa shilingi bilioni nne, lakini suala hilo limechelewa kutekelezwa mpaka tumekuja kuingia kwenye bajeti nyingine. Tukiwa kama wajumbe wa Kamati tunaona kwamba, hii inaidhoofisha Tume ya Mipango ya Kupima Ardhi kuweza kutimiza wajibu wake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukiona migogoro ya mipaka ikiendelea, lakini pia tumeona wakulima hawajui mipaka yao ni eneo gani la kulima, pia tumekuwa tukiona wafugaji hawajui maeneo yao ya ufugaji na hii kusababisha migongano kati ya wakulima na wafugaji. Ombi langu kwenye Wizara ya Ardhi ni kuiongezea Tume ya Mipango ya Kupima Ardhi Nchini ili iweze kufanya kazi yake vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ninaomba kuzungumzia suala la pesa za mkopo ambazo Serikali yetu ya Tanzania imekopa mkopo huu ambao unaitwa Land Tenure Improvement Program. Pesa hizi ni dola 150, sawa na shilingi bilioni 350 za Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Kamati tuliona kwamba, fedha hizi zingeelekezwa zaidi kwenye upimaji wa ardhi. Kwa maana kwamba, tukiwa kama Kamati tulipendekeza zaidi pesa hizi ingepewa Tume ya Mipango ya Kupima Ardhi ili iweze kwenda kutekeleza wajibu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Mipango ya Kupima Ardhi ina uwezo wa kupima vijiji 826 kwa mwaka, lakini mradi huu unakwenda kupima vijiji 500 kwa muda wa miaka mitano. Ukiangalia uwiano ni kwamba, kutakuwa na uwiano wa vijiji 100 kupimwa kwa mwaka mmoja. Kitu ambacho tunaona kwamba, kwa mfano kama hii fedha Tume ya Mipango ingepewa ingeweza kupima vijiji 826 kwa mwaka, na matokeo yake kwa muda wa miaka mitano ingeweza kupima zaidi ya vijiji 4,131. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia unakuta kwamba, uwiano wa vijiji 500 kwa miaka mitano ni tofauti kubwa na uwiano wa vijiji 4,131 ambavyo vingeweza kupimwa na Tume ya Mipango ya Kupima Ardhi nchini Tanzania. Ombi langu kwa Serikali, ninaomba fedha hizi waweze kufanya utaratibu; Tume ya Mipango ya Kupima Ardhi ipewe fedha hizo ili iweze kupima hivi vijiji na ili iweze kuendana na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo imesema kwamba, kwa muda wa miaka mitano tungeweza kupima vijiji zaidi ya 4,131. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ambalo ningependa kulizungumzia hapa kwenye huo huo mradi; tunaomba ile mikoa ambayo inakwenda kujenga hizi ofisi kutokana na hizi fedha, kwanza tungeomba ofisi zijengwe kwa uwiano wa kufanana. Yaani kwamba, mikoa yote gharama ya ujenzi ilingane; kwa maana ya kwamba, hata kule Katavi waweze kupata ofisi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ambalo ningependa kulizungumzia hap ani suala la mipaka yetu ya nchi yetu ya Tanzania. Suala la mipaka ni tata kwa sababu gani, tumeona sehemu nyingine hazijawekewa mipaka, lakini pia sehemu ambazo zimewekewa mipaka ni wanajenga vi-box vidogo sana ambavyo ni kama mita moja. Mfano, tulikwenda pale Tunduma tukakuta mpaka, ni kitu kimetoka chini urefu wa mita moja mpaka hapa, ndio unaitwa mpaka wa Tanzania na zamabia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunataka kuboresha mipaka ya nchini kwetu Tanzania ninaomba Serikali iweke utaratibu, hususan Wizara ya Ardhi ambayo inaratibu hili jambo, ijenge mipaka ya kuonekana ambayo itakuwepo sasa na miaka 100 ijayo. Ujenzi wa mipaka ambao unaendelea sasahivi, mipaka ile ni midogo na sehemu nyingine hazionekani, haijulikani mpaka uko wapi, umeishia wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, fedha ambazo zinatolewa kwa ajili ya ujenzi wa mipaka ya nchi yetu ya Tanzania ni fedha chache. Hii inasababisha kwamba, huko baadaye sisi tutaishi na tutapotea, lakini tunataka kizazi kinachokuja kikute mipaka ya nchi yetu imeratibiwa vizuri na inaonekana. Kwa maana kwamba, kama unajenga urefu wa mita moja kutoka chini na unasema kwamba, huu ndio mpaka ina maana unahitaji baada ya muda labda miaka kama 20 utahitaji kujenga tena, kurudia zoezi lilelile la kujenga mipaka upya, kitu ambacho naona kwamba ni utumiaji wa fedha mara mbili. Kama tunaboresha mipaka yetu basi tungeboresha mipaka yetu vizuri na tujenge mpaka wa kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ambalo ningependa kulizungumzia, wananchi wengi wanakaa kwenye vijiji hawaelewi kwamba wanapaswa kupima ardhi zao. Matokeo yake ni nini? Matokeo yake mwekezaji anafika pale anachukua ile ardhi kwa sababu, yeye amewekeza na yule mwananchi ambaye amekaa pale kwa takribani muda wa miaka mingi anaondoka pale kwa sababu tu, alikuwa ahajapima ile ardhi na kwa sababu alikuwa hana hati. Ombi langu kwa Serikali, ninaomba Wizara ya Ardhi iwaelimishe wananchi waweze kupima ardhi zao kama ni shamba, ni kitu chochote waweze kukipima, ili kutoa huu usumbufu wa kunyang’anywa ardhi zao ambazo wanakuwa wamekaa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani mtu anakaa mahali takribani zaidi ya miaka 50 halafu unakuja kumwambia kwamba, hapa si nyumbani kwako kwa sababu huna hati. Kwa hiyo naomba wananchi waelimishwe waweze kupima ardhi zao, lakini pia waweze kutumia hizo hati zao kwa ajili ya kupata mkopo benki na sehemu nyingine. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)