Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa. Kwanza nianze kwa kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuonesha mapenzi makubwa sana kwa Watanzania hasa pale alipoagiza migogoro yote ya ardhi nchini iende ikatatuliwe. Rais ameonesha mapenzi makubwa sana kwa Watanzania. Sisi Wabunge tunamuunga mkono, Watanzania wote wanamuunga mkono, wanasubiria kuona hatua za Serikali za kutatua migogoro hiyo mmoja baada ya mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, napenda kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Ngara walioniamini mwaka 2020 wakanituma nije hapa Bungeni kuweza kuwatetea na kuwasemea kuhakikisha kwamba Serikali inatatua changamoto mbambali zinazowakabili. Nitaendelea kuwa mwaminifu kwa wananchi wa Jimbo la Ngara, nitaendelea kuwasemea na kuwatetea kwa kadri Mwenyezi Mungu anavyoniwezesha. Niendelee kuwaomba waendelee kuwa na imani kubwa juu yangu, mambo yao ninayashughulikia moja baada ya lingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo langu la kwanza ambalo nachangia hapa ni mgogoro wa ardhi baina ya Kijiji cha Rusumo na Gereza la Rusumo, mgogoro ulioletwa na Afisa wa Ardhi ambaye mamlaka yake ya kinidhamu iko chini ya Wizara ya Ardhi. Afisa huyu kwa kushirikiana na viongozi wa Gereza la Rusumo walikwenda wakajifungia kwenye chumba wakachukua laptop na mouse wakaweka pale, wakaweka na software wakaanza ku-generate coordinates, wakapima eneo kwamba eneo linalomilikiwa na Gereza la Rusumo ni hili, wakapima kwa kutumia Computer.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya jambo hili walilofanya ni kwamba coordinates ya kwanza (majira ya nukta) yaliangukia kwenye noman’s land kwenye mto ambao tunaumiliki Tanzania na Taifa lingine. Hapa nimetumia neno la kidiplomasia kidogo. Coordinate nyingine ambayo walii-generate kwenye laptop, inanonekana sasa magereza wanamiliki eneo ambalo linamilikiwa pia na TANAPA. Wakati huo huo, coordinates nyingine wame-generate, Magereza wanamiliki barabara ya kimataifa ambayo ilikuwepo hata kabla ya gereza lenyewe kwenda pale. Sasa matokeo yake wametuletea matatizo makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Wilaya ya Ngara Kanali Mathias Kahabi, aliunda tume ya kwenda kuchunguza, nami nilishiriki tukatumia kifaa kinaitwa real time kinematics (RTK) kwa ajili ya ku-verify, tukakutana na madudu makubwa. Sasa wakati nawasubiria kwa hamu Wizara ya Mamabo ya Ndani, na kwa sababu wanajua walichokifanya mwaka 2022, Mheshimiwa Jenista Mhagama unakumbuka, lile swali langu la mgogoro wa Rusumo ulivyokuja hapa Bungeni, Magereza wakaidanganya Serikali kwamba hakujawahi kutokea mgogoro. Nikasema Mheshimiwa Jenista Mhagama tupilia mbali hilo, hayo majibu siyahitaji. Ukayatupilia mbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakati nawasubiria kwa hamu Wizara ya Mambo ya Ndani, na nimemwambia Mheshimiwa Masauni mara nyingi kwamba, wanampotosha Magereza. Naomba Wizara ya Ardhi mshughulike na huyu Afisa wa Ardhi ambaye ametuletea matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshazungumza na Katibu Mkuu, ninasubiria utendaji. Wananchi wa Rusumo wanasubiria kuona mnachokifanya, namna mnavyo mshughulikia huyo Afisa wa Ardhi ambaye ametuletea matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la 2025 limeshakaa vizuri maeneo mengi, naomba msiniharibie, naomba huu mgogoro muende muuondoe mara moja kwa sababu kitu kimeshakaa kibra 2025, nataka nipite kwa kuogelea. Sasa, nataka nikuombe Mheshimiwa Waziri, nenda kamalize ule mgogoro, shughulika na yule mtu wako, na mimi nitaendelea kuhangaika na watu wa Wizara ya Mambo ya Ndani nao waweze kufanya kwa upande wao. Ndiyo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nichangie ni namna ambavyo Wizara ya Ardhi inafanya utafiti wa kujua viwango vya fidia kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini. Kule Ngara kuna mchakato wa disclosure unaoendelea ambao Mthamini Mkuu wa Serikali ambaye yuko hapa Bungeni ameusimamia, mama mmoja Mrs. Zuhura Hiraly aliachiwa nyumba na baba yake mwaka 1943; hii nyumba wameenda kuifanyia uthamini wanataka kumlipa shilingi laki saba. Mama huyo pia aliachiwa nyumba na mme wake tena mwaka 1950 wanataka kumlipa shilingi milioni moja na laki mbili. Hiyo fedha haitoshi hata kujenga banda la kuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yule mama amesema nendeni mkabomoe lile eneo bomoeni majumba bomoeni kila kitu mkachukue hahitaji hiyo fedha kwa sababu haina uhalisia. Nimezungumza na Mthamini Mkuu wa Serikali, nikamwambia utaratibu huu wa kuibua viwango vya fidia vinavyo akisi thamani halisi ya majumba ya watu na ardhi za watu maeneo mbalimbali nchini vinatakiwa viangaliwe upya, viwe shirikishi na viweze kuakisi thamani halisi ya mali nyumba na viwanjanya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi viwango mnavyovitumia inawezekena na vyenyewe vime-expire kama ilivyo sera ambayo imepitwa na wakati, inawezekana vyote hivi vinatakiwa kwa pamoja viweze kupitiwa viangaliwe tuvi-set upya. Nimeambiwa wanamtafuta consultant anakwenda vijiini anakusanya mikataba anaandika ripoti anawasilisha kwa valuer wa Serikali. Sasa anayetaka kulipa hela ni Serikali anayefanya valuation ni Serikali katika ule mchakatohakuna stakeholders’ engagement ili muweze kupata second opinion kwamba hiki siyo sawa hiki ni sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ninataka niwaombe Wizara ya Ardhi, kwanza wananchi wangu wote wanaofidiwa kuanzia kule Mrusagamba kwenda Rurenge kwenda Tembonikeili kwenda Mrugarama kule mhakikishe mnatenda haki mmeenda kwa Diwani wa Kabanga Hafidhi Abdallah amechukua kiwanja amekinunua milioni tano mnataka kumpa laki saba, haiwezekani, haiwezekeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka niwaombe mwende mkapitie ule mchakato upya ndugu yangu government valuer, Waziri nendeni mkapitie mchakato upya, nendeni mkatende haki. Mtu anapewa shilingi 70,000 uliona wapi fidia ya mali ya shilingi 70,000? Naomba mwende mkapitie upya na mfanye haraka na msicheleweshe barabara yetu ya lami kwa sababu nyie ndio ambao mnaleta vitu ambavyo kwa kweli vinafikirisha. Kwa hiyo ninaomba eneo hili lifanyiwe kazi na wananchi wangu wote waweze kupata haki kwa wakati na barabara yetu isicheleweshwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ambalo nataka nichangie ni eneo la kuwezesha Wizara yenyewe ya Ardhi iweze kupima na kupanga maeneo mbalimbali ya kimkakati hapa nchini. Haiwezekani kwamba tunaongelea kwenda kupima vijiji tu badala ya kutafuta maeneo ya kimkakati, maeneo ya mpakani, miji inayokua, maeneo ambayo yanaweza yakarudisha fedha haraka haraka, maeneo yenye mzunguko wa hela ndiyo twende tukayapime ili Watanzania waweze kumiliki viwanja, waweze kupata hati, waweze kukopesheka na nchi yetu iweze kuendelea. Ifike mahali makusanyo yanayotokana na ardhi yaweze kutusaidia Watanzania kujiendesha kama Taifa. Eneo hilo halijatendewa haki vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasikitika kuona kinachoendelea. Shilingi bilioni 80 zina uwezo wa kupima viwanja 368,000 kwa mika mitano. Narudia, shilingi bilioni 51 zina uwezo wa kupima viwanja 368, 000 kwa mika mitano. Hii shilingi bilioni 51 ikitengwa itarejesha shilingi bilioni 80 katika kipindi kile, kwa sababu ardhi moja itakayopimwa, yaani kiwanja kimoja, average ya malipo ambayo mwananchi wa kawaida anatakiwa kulipa ni shilingi laki mbili hadi shilingi elfu ishirini. Ukizidisha fedha hizi utakuta kwamba upimaji wa ardhi unalipa kuliko kitu chochote kile. Unatumia bilioni 51.5 unarudisha bilioni 80. Ni kwa nini tusitenge fedha tukaenda kupima ardhi ya Watanzania? Ni sababu gani inasababisha tuwe na kigugumizi kutenga fedha? Tumetoa fedha kwa ajili ya kupunguza bei ya mafuta nchini ili iweze kushuka. Sasa, kule tulikokuwa tunatoa fedha zile tuchukue fedha nyingine tuweke kwenye ardhi tuwasaidie Watanzania kupima ardhi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu asubuhi watu wamesema, kwamba wale watu wa ardhi wanapima ardhi kule na fedha yote inakwenda Serikali Kuu, matokeo yake watu wanatembea hata mafuta ya kuweza kutoka eneo moja kwenda jingine hawana. Ofisi zile za ardhi zilizoko Serikali za Mitaa ambazo pia nyie mnawajibika hazina kabisa fedha kwa ajili ya kuendeshea shughuli za upimaji, matokeo yake hakuna kazi kule inayofanyika. Zile Ofisi zimegeuka kutegemea wapimaji binafsi ambao wanakwenda kupima maeneo madogo yasiyo tosheleza.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumalizia, ninaomba Serikali iwaachie asilimia 30 ya makusanyo yote yanayotokana na ardhi ili Ofisi zile ziweze kujiendesha na zifanye upimaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ahsante sana, naunga mkono hoja.